Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usalama wanyima chakula wahitaji Upper Nile, Sudan Kusini

Wanawake wakikagua msaada wa virutubisho vya lishe nchini Sudan Kusini.
© WFP/Eulalia Berlanga
Wanawake wakikagua msaada wa virutubisho vya lishe nchini Sudan Kusini.

Ukosefu wa usalama wanyima chakula wahitaji Upper Nile, Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu
  • Mapigano hasa jimboni Upper Nile yasababisha WPF kusitisha mgao wa chakula katika kaunti sita
  • Usafirishaji kwa njia ya mto umekwama kwa sababu ya mapigano
  • Eneo hilo hakuna barabara hivyo mkwamo kusafiiri kwa gari au lori
  • Mapigano yanachochea njaa sasa 

Ukata ukikabili operesheni za usaidizi wa kibinadamu nchini Sudan Kusini, hata kile kidogo kilichopo kwa ajili ya wahitaji kinakumbwa na mkwamo katika kufikia wahitaji, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la  Mpango wa Chakula duniani, WFP, likieleza bayana kuwa vizingiti vya kufikisha misaada vinatokana na ukosefu wa usalama.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, WFP inatolea mfano kuongezeka kwa mvutano na mapigano kando ya mito inayotumiwa na WFP kama njia za usambazaji kunakwamisha usafirishaji wa msaada wa chakula jimboni Upper Nile.

Matokeo yake WFP imelazimika kusitisha mgao wa chakula katika kaunti 6 za jimbo hilo kwa hofu ya usalama wa watumishi wake, wadau na watu wanaowahudumia.

“WFP na wadau wake wako tayari kuendelea na mgao wa chakula pindi tu mazingira yatakaporuhusu,” imesema taarifa hiyo.

Kutokana na hatua hiyo familia zilizo hatarini zaidi kwenye maeneo ya kaskazini-mashariki mwa Sudan Kusini yako katika hali tete zaidi wakati huu mapigano yanazidi kuongezeka jimboni Upper Nile, na viwango vya njaa vinakabiria kuvunja rekodi, limeonya shirika hilo.

Kauli ya Mkuu wa WFP Sudan Kusini

Wakati huo huo, akizungumza kutoka Juba, Mwakilishi wa WFP nchini Sudan Kusini Mary-Ellen McGroarty amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwamba “tunashuhudia madhara makubwa ya vita vinavyochochea njaa. Raia wamelazimika kukimbia wakiwa na virago vya nguo zao tu, wakiwa na mbinu kidogo za kujipatia kipato. Mbinu za msimu za kujipatia kipato zimetelekezwa.”

Bi. McGroarty amesema haya ni  baadhi ya maeneo yaliyoko ndani mno nchini Sudan Kusini. Kuyafikia ni kazi kubwa, na mapigano yakiwa yanaendelea WFP haiwezi kwenda kwa kutumia usafiri wa boti.

“Maeneo haya hayana barabara, magari, malori. Na tunapopeleka chakula, tunahitaji kutumia mto au kutumia njia ya anga,” amesisitiza.

“Msimu wa mwambo  ukianza Sudan Kusini, takribani watu milioni 7.7 wanakabiliwa na njaa, kiwango cha njaa kikitajwa kuwa ni janga, ambapo kati yao yao milioni 3.1 wako Eneo Kuu la ukanda wa Upper Nile, likijumuisha jimbo la Upper Nile,” imesema WFP.

Tayari kipindupindu kimelipuka Upper Nile na WFP imepeleka tani za ujazo 35 za dawa na vifaa vya kujisafi , huku tani nyingine tatu zikisubiri kusafirishwa.

Kuhusu ufadhili, WFP inasema inakabiliwa na pengo la dola million 396 kwenye ombi lake la ufadhili wa operesheni za kibinadamu Sudan Kusini kwa mwaka huu wa 2025.

Soma taarifa kamili hapa.