Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Gaza ni uwanja wa mauaji" aonya Mkuu wa UN akitaka usitishaji mapigano, upatikanaji wa msaada, na uwajibikaji

Wafanyakazi wa uokoaji wakitoa kutoa miili ya wafanyakazi wa misaada kutoka kwenye kaburi la pamoja lisilo na kina, akiwemo mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Tal Al Sultan.
© UNOCHA
Wafanyakazi wa uokoaji wakitoa kutoa miili ya wafanyakazi wa misaada kutoka kwenye kaburi la pamoja lisilo na kina, akiwemo mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Tal Al Sultan.

"Gaza ni uwanja wa mauaji" aonya Mkuu wa UN akitaka usitishaji mapigano, upatikanaji wa msaada, na uwajibikaji

Amani na Usalama

Katika tamko lake kali zaidi hadi sasa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa onyo leo kuhusu janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya huko Gaza. Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani Guterres amesema “zaidi ya mwezi mzima umepita bila hata tone moja la msaada kufika Gaza.”

Ameongeza kuwa “hakuna chakula. Hakuna mafuta. Hakuna dawa. Hakuna bidhaa za kibiashara.”

Amelitaja eneo la Ukanda wa Gaza lililozingirwa kuwa ni “uwanja wa mauaji,” na ametoa wito wa kusitisha mapigano mara moja na ya kudumu, kuruhusu msaada wa kibinadamu bila vizuizi, na kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia bila masharti.

Kijana mmoja amesimama karibu na makazi ya muda huko Gaza.
© UNRWA
Kijana mmoja amesimama karibu na makazi ya muda huko Gaza.

Mzunguko usioisha wa vifo unaendelea

Guterres ameelezea kwa kina hali ya kusikitisha ya Gaza inayozidi kuporomoka katika machafuko na kukata tamaa.

“Kadri msaada unavyokoma, mlango wa hofu umefunguliwa tena,” amesema na kuongeza kuwa “Gaza ni uwanja wa mauaji  na raia wako katika mzunguko usioisha wa kifo.”

Amesisitiza kuwa ingawa mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas yalikuwa ya kigaidi, mateso ya raia wa Gaza hayawezi kupuuzwa wala kuhalalishwa.

Ameonya kuwa madhara ya kuvunjika muafaka wa usitishaji wa mapigano yanawabebesha mzigo mkubwa zaidi wanawake, watoto, na familia zisizo na msaada.

Usitishaji mapigano uliokoa maisha  mpaka uliposambaratika

Akikumbusha kuhusu kipindi kifupi cha usalama, Guterres amesisitiza nguvu ya diplomasia.

“Usitishaji mapigano uliwezesha kuachiliwa kwa mateka. Uliruhusu usambazaji wa msaada wa kuokoa maisha. Ulihakikisha kuwa jamii ya misaada inaweza kufanikisha kazi yake.”

Ameendelea kusema kuwa Katika kipindi hicho, mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliweza kufika karibu kila sehemu ya Gaza.

Lakini tangu usitishaji huo wa mapigano ulipovunjika, matumaini na misaada vyote vimeyeyuka.

“Matumaini yamezama kwa familia za Wapalestina Gaza na familia za mateka huko Israel,” amesema, akirejea mkutano wake wa hivi karibuni na familia za mateka.

Timu ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA imesaidia watendaji wa shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, pamoja na kikosi cha ulinzi wa raia cha Palestina kufukua miili ya wahudumu 15 wa kiutu iliyokuwa imefukiwa kando mwa m…
UNOCHA
Timu ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA imesaidia watendaji wa shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, pamoja na kikosi cha ulinzi wa raia cha Palestina kufukua miili ya wahudumu 15 wa kiutu iliyokuwa imefukiwa kando mwa magari yao huko Rafah, Gaza Machi 31, 2025.

Sheria za kimataifa si hiyari

Katika mkutano huo na wanahabari Katibu Mkuu amenukuu kwa umakini sheria za kimataifa za kibinadamu, akitaja vifungu vya 55, 56, na 59 vya Mkataba wa Nne wa Geneva. 

Akifafanua vifungu hivyo amesema Kifungu cha 55, aya ya 1, cha Mkataba wa Nne wa Geneva kinabainisha kwamba Mamlaka ya kuvamia inawajibika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na vifaa vya matibabu kwa idadi ya watu.”

Kifungu cha 56, aya ya 1, cha Mkataba wa Nne wa Geneva kinabainisha kwamba Mamlaka ya inayovamia inawajibika kuhakikisha na kudumisha taasisi na huduma za matibabu na hospitali, afya ya umma na usafi wa mazingira katika maeneo yaliyovamiwa.”

Kifungu hiki kinaongeza kuwa “Wahudumu wa afya wa aina zote wanapaswa kuruhusiwa kutekeleza majukumu yao.”

Na Kifungu cha 59, aya ya 1, cha Mkataba wa Nne wa Geneva kinabainisha kwamba “Iwapo watu wote au sehemu ya watu katika eneo lililovamiwa hawapati mahitaji ya msingi kwa kiwango cha kutosha, mamlaka iliyovamia inapaswa kukubali mipango ya misaada kwa ajili ya watu hao, na iwe tayari kusaidia kwa njia zote ilizonazo.”

Akieleza kwa ukali amesema “Hakuna hata moja ya hayo yanayotendeka leo.”

Amesisitiza kuwa “Kama taifa lenge nguvu linalokalia eneo hilo, Israel ina wajibu usio na masharti.”

Amelaani vikali vizuizi vya misaada na hali ya kukwama kwa magari ya msaada kwenye mipaka.

Amesema “Usalama umedorora, na uwezo wetu wa kufikisha msaada umebanwa kabisa.” Hivyo imekuwa changamoto kuwafikia wenye uhitaji.

Misingi ya kibinadamu iko hatarini

Katibu Mkuu Guterres ameonya juu ya “utaratibu mpya wa idhini uliopendekezwa na Israel kuhusu usambazaji wa misaada”, akisema unaweza kuufanya msaada huo kudhibitiwa “kwa ukatili hadi kwa punje ya unga.”

Ameoengeza kuwa “Hatutashiriki katika mpango wowote ambao hautaheshimu kikamilifu misingi ya kibinadamu, ubinadamu, kutotenga, uhuru na kutoegemea upande wowote”.

Pia amewapongeza wahudumu wa misaada walio mstari wa mbele akisema “Wako katika hatari ya kushambuliwa lakini bado wanaendelea kusaidia watu ndicho walichochagua kufanya.”

Hospitali ya uzazi ya Palestinian Red Crescent huko Rafah iko magofu baada ya kushambuliwa kwa bomu.
© WHO
Hospitali ya uzazi ya Palestinian Red Crescent huko Rafah iko magofu baada ya kushambuliwa kwa bomu.

Ulimwengu huenda inakosa maneno

Akihitimisha mkutano wake na waandishi wa habari kwa kauli ya maadili ya juu, Guterres ametoa wito wa haki, uwajibikaji, na ujasiri kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

“Huenda ulimwengu unakosa maneno ya kuelezea hali ya Gaza, lakini kamwe hatutakimbia kutoka kwenye ukweli,” amesema.

“Njia ya sasa ni imekufa isiyokubalika kabisa kwa macho ya sheria za kimataifa na historia.”

Akionya kuhusu hatari ya Ukingo wa Magharibi kuwa Gaza nyingine, amesema “Ni wakati wa kumaliza unyanyasaji, kuwalinda raia, kuwaachilia mateka, kuhakikisha msaada wa kuokoa maisha unafikishwa, na kurejesha usitishaji mapigano.”