KINNAPA Development Programme yaleta mapinduzi ya kijamii kwa kuinua wanawake na wasichana wamasai
KINNAPA Development Programme yaleta mapinduzi ya kijamii kwa kuinua wanawake na wasichana wamasai
“Tunaingia katika jamii kwa nyanja tofauti kama kilimo, mifugo, elimu, afya, maji na usafi wa mazingira, pamoja na rasilimali za asili. Katika nyanja hizi zote, kuna miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa hadi sasa,” anaeleza Paulina Peter Ngurumwa akiongea na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alipohudhuria Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake, CSW69 jijini New York, Marekani anapofafanua jinsi shirika lisilo la kiserikali la KINNAPA Development Programme inavyofanya kazi kwa karibu na jamii za wafugaji, wakulima wadogo wadogo, wawindaji, na waokota matunda katika nyanja mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania.
Mafanikio baada ya CSW68 – kurejesha wasichana shuleni na kuimarisha uwezeshaji
Baada ya ushiriki wao kwenye Mkutano wa CSW68 mwaka jana 2024, Mpango wa Maendelo wa KINNAPA ulirudi nyumbani na kufanikisha mabadiliko makubwa.
“Tulirejea nyumbani na juhudi za kushughulikia changamoto tulizoziona katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mila na desturi kandamizi zinazomkandamiza mtoto wa kike na mwanamke. Tulianza kwa kuwahamasisha malaigwanani (viongozi wa jamii ya kimaasai) ili kuona jinsi wanavyoweza kusaidia mtoto wa kike kupata elimu na kuhakikisha wanawake wanakuwa na sauti na haki ya kumiliki rasilimali,” anafafanua Bi Ngurumwa.
Kupitia juhudi hizo, wasichana waliokatiza masomo walipewa mafunzo ya kurejea shuleni na wengine kupewa nafasi ya kujifunza stadi za maisha kupitia miradi ya cherehani. “Leo hii, tunajivunia kuwa baadhi ya wasichana waliorejea shule sasa wameshafika vyuo vikuu,” anasema kwa furaha.
Kuimarika kwa haki za ardhi kwa wanawake wa kimasai
Shirika hilo pia limefanikiwa kuwawezesha wanawake wa Kimaasai kudai haki zao za kumiliki ardhi, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa muda mrefu. Paulina ameeleza, “Wanawake wa Kimaasai katika maeneo yetu sasa wanaweza kwenda kwenye ofisi za serikali za vijiji kudai hati miliki za ardhi yao badala ya ardhi kumilikiwa na wanaume peke yao. Mwanamke wa Kimaasai anamwambia mwanaume, ‘Sisi ni wake 10 kwako, wewe si umetuoa wanawake 10. Basi usiseme ardhi yangu ndiyo ya kijana wangu. Hapana, mpe kijana wangu sehemu yake na unipe mimi pia sehemu yangu.’”
Majukwaa ya wanawake: Kupinga ndoa za utotoni
Kwa kutumia mfumo wa Joint Village Land Use Planning (JVLUP), Shirika la KINNAPA liliwawezesha wanawake kushiriki katika uamuzi muhimu, ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria za kukomesha ndoa za utotoni. “Mila ya kuoza wasichana wakiwa na umri mdogo wa miaka 8 hadi 11 na hata wa umri wa miaka 4 imepata upinzani mkubwa sasa. Wanawake wanasema kwa kauli moja, ‘Mtoto wangu kwanza aende shule, ndipo aolewe.’” anasema.
Changamoto zinazokwamisha mafanikio
Pamoja na mafanikio haya makubwa, Shirika la KINNAPA bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa rasilimali na ufadhili wa haraka. Paulina alieleza kuwa wengi wa wanawake na wasichana wanaohitaji msaada wa miradi ya uzalishaji mali bado hawajapata msaada wa kutosha. “Wanawake hawa wanaendelea kuanzisha miradi midogo midogo kwa kutumia mtaji mdogo walionao, lakini bado wanahitaji msaada mkubwa ili miradi hiyo iwe endelevu,” ameeleza.
Wito kwa wadau wa maendeleo
Anatamatisha kwa kutoa wito kwa wadau wa maendeleo na wafadhili kusaidia juhudi zao za kuwainua wanawake na wasichana katika jamii zao akisema, “tunaomba wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa msaada wa kifedha na rasilimali zinazohitajika ili kuwasaidia wanawake hawa kujikwamua kiuchumi,”