Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa amani uko njiapanda: Simulizi ya changamoto na mabadiliko

Walinda amani wa Guatemala na Bangladesh kutoka MONUSCO wakielekea kwenye helikopta kwenye barabara ya vumbi huko Bunia, Mkoa wa Ituri, DR Congo, wakijiandaa kwa Operesheni Uppercut.
MONUSCO Wanavikosi wa MONUSCO wakipiga doria mkoa wa Ituri nchini DRC. (Maktaba)

Ulinzi wa amani uko njiapanda: Simulizi ya changamoto na mabadiliko

Amani na Usalama

Mkuu wa Operesheni za Umoja wa Mataifa za Ulinzi wa Amani, Jean-Pierre Lacroix amesema zama za sasa walinda amani  hawasimamii tu maeneo ya mapigano bali wanakabiliana na migogoro mchanganyiko, kampeni za habari za uongo na potofu, vitisho vya mtandaoni na mienendo isiyotaribika kutoka vikundi vilivyojihami.

Lacroix amesema  hayo akihutubia Baraza la Usalama lililokutana leo kujadili Operesheni za Umoja wa Mataifa za Ulinzi wa amani akiongeza kuwa kutokana na mazingira hayo ni lazima misheni hizo nazo zibadili utendaji wake wakati huu ambapo bado ufuatiliaji na usimamizi wa sitisho la mapigano kati ya pande kinzani bado ni jukumu la msingi la misheni hizo.

Amesema “leo hii uwepo kwenye eneo la tukio haitoshelezi. Lazima tuelewe na tuchukue hatua mara tu tukio linapojitokeza,” huku akitolea mfano misheni ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa amani Lebanon, UNIFIL na ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO.

“Nchini Lebanon, UNIFIL imelazimika kurekebisha msimamo wake kwa kiasi kikubwa kufuatia sitisho la mapigano mwezi Novemab kati ya Israeli na wanamgambo wa Hezbollah. Nchini DRC, MONUSCO inasubiri uwezekano wa kuongezwa jukumu lake katika kutekeleza usimamizi wa sitisho la mapigaon ambalo kwa sasa bado ni tete na hakuna uhakika.”

Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani, akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama UN huko New York.
UN Photo/Eskinder Debebe Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Changamoto zinazokabili ulinzi wa amani

Kwa mujibu wa Lacroix, ulinzi wa amani unakabiliwa na changamoto zifuatazo :

  1. Ukata : Huu unakwamisha uwezo wa misheni kufikia maeneo husika na hata utayari wa kuchukua hatua.
  2. Mgawanyiko wa kisiasa : Kuweko kwa mgawanyiko wa kisiasa miongoni mwa nchi wanachama kunamomonyoa utangamano wa misheni husika.
  3. Habari potofu, za uongo na ulaghai wa kimtandao: Vitendo hivi vinapanda mbegu ya sintofahamu na chuki baina ya jamii na walinda amani wenye jukumu la kulinda raia.
  4. Pengo la mafunzo : Kuna nyakati walinda amani wanapelekwa kuhudumu kwenye misheni za ulinzi wa amani bila mafunzo sahihi ya kuendana na changamoto za sasa.

Mwelekeo mpya

Bwana Lacroix amesema katikati ya changamoto hizo, nuru inaanza kuonekana ikisongeshwa na ugunduzi, ujumuishaji na ushirikiano.

Ametaja Mkakati wa Mabadiliko ya Kidijitali, uliozinduliwa chini ya mpango wa Hatua kwa Ulinzi wa Amani au A4P kuwa unabadilisha jinsi misheni zinavyofanya kazi.

“Nchini Cyprus, jukwaa la Unite Aware limewawezesha walinda amani kubadilika kutoka msimamo wa kusubiria kuchukua hatua na badala yake kuzuia—kudhibiti ukiukaji kabla ya matukio kuongezeka na hivyo kutumia rasilimali kwa njia ya kimkakati zaidi.”

Halikadhalika ulinzi wa amani unakumbatia nyanja mpya. Operesheni za ushawishi na mashambulizi ya mtandao si tena masuala ya pembeni; ni uwanja wa vita wa kati.

Mwonekano mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama UN huko New York, huku skrini kubwa ikimuonyesha Kamanda wa Kikosi Ulisses De Mesquita Gomes kwenye kiungo cha video.
UN Photo/Eskinder Debebe Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la UN lilipokutana Aprili 7, 2025 kujadili operesheni za ulinzi wa amani za UN

Amesema “misheni za ulinzi wa amani lazima ziwe na vifaa sio tu magari ya kivita bali pia wachambuzi wa data, wataalamu wa mtandao, na waandishi wa kimkakati waliofunzwa kupambana na habari za uongo na potofu ili kujenga imani ya jamii.”

"Msingi wa mabadiliko haya ni ukweli mmoja: ulinzi wa amani lazima ubaki katika mchakato wa kisiasa. Teknolojia, mafunzo, na zana ni bora tu ikiwa kuna utashi wa kisiasa miongoni mwa pande zinazohusika kwenye kusaka amani. "Ulinzi wa amani," Bwana Lacroix amekumbusha, "hauwezi kuchukua nafasi ya amani. Unaweza tu kuunga mkono."

Utekelezaji wa azimio namba 1701 kati ya Lebanon na Israeli wahitaji utashi wa kisiasa

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha UNIFIL, Meja Jenerali Aroldo Lázaro amelieleza Baraza kwamba  "ufuatiliaji wa sitisho la mapigano ni jukumu muhimu katika mamlaka ya UNIFIL kama ilivyoelezwa katika azimio la Baraza la Usalama namba 1701. Na hili lilikuwa muhimu zaidi baada ya mapigano ya kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi mwezi Novemba 2024."

Hata hivyo Meja Jenerali Lázaro amesema "mchakato wa kisiasa kuelekea usitishaji wa kudumu wa mapigano unapaswa kuwa kipaumbele cha juu zaidi. Ushiriki wa Marekani na Ufaransa ulisaidia kupunguza mapigano mwezi Novemba 2024. Mfumo wa ufuatiliaji umeanzishwa, lakini huu bado ni mchakato dhaifu na hadi sasa, kilichofanyika ni mawasiliano kati ya majeshi ya pande husika.”

Amesisitiza kuwa upande wa kisiasa ni muhimu sana kuhusika ili kutekeleza kikamilifu azimio namba 1701 na kuwezesha majadiliano ya wazi juu ya mchakato wa uwekaji mipaka ambao unaweza kuwa na utata."

Luteni Jenerali Ulisses de Mesquita Gomes, Kamanda wa Kikosi cha MONUSCO, akitoa taarifa kwa Baraza la Usalama UN kuhusu shughuli za kulinda amani kupitia kiungo cha video.
UN Photo/Loey Felipe Kamanda wa MONUSCO Luteni Jenerali Ulisses de Mesquita Gomes, ambaye akihutubia kutoka Beni, mji mkuu wa sasa wa jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki kwa DRC

Nafasi ya teknolojia katika kuimarisha majukumu ya MONUSCO

Wajumbe pia walipata maoni kutoka kwa Kamanda wa MONUSCO Luteni Jenerali Ulisses de Mesquita Gomes, ambaye akihutubia kutoka Beni, mji mkuu wa sasa wa jimbo la Kivu  Kaskazini, mashariki kwa DRC amesema "MONUSCO ina teknolojia za ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani, (UAVs) kwa ajili ya uchunguzi wa anga, na mifumo ya rada ya ardhini kwa ajili ya usalama wa mipaka."

Amesema teknolojia hizo zimeongeza kwa kiasi kikubwa ufahamu wa hali na ufanisi wa operesheni, kupunguza hatari kwa walinda amani na pia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya ujumbe huo.

Vifaa hivi, kwa mujibu wa Luteni Jenerali de Mesquita Gomes "vinaweza pia kutumika kwa ajili ya ufuatiliaji wa usitishaji mapigano."

Hata hivyo ameongeza "ili kuhakikisha uwezo kamili wa teknolojia hizi, tunahitaji kuhakikisha kuwa zimeunganishwa kikamilifu katika mifumo na majukwaa yetu ya takwimu."