Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kina mama wajawazito wanaweza kuishi na kujifungua salama sasa kuliko wakati mwingine wowote: UN Ripoti

Mwanamke mmoja huko Udaipur, India, anaelekea kliniki na mwanae kwa ajili ya uchunguzi wa ujauzito. Wanawake wajawazito, watoto na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya hali ya hewa ambayo yanahitaji tahadhari ya haraka. (M…
© UNICEF/Ruhani Kaur
Mwanamke mmoja huko Udaipur, India, anaelekea kliniki na mwanae kwa ajili ya uchunguzi wa ujauzito. Wanawake wajawazito, watoto na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya hali ya hewa ambayo yanahitaji tahadhari ya haraka. (Maktaba)

Kina mama wajawazito wanaweza kuishi na kujifungua salama sasa kuliko wakati mwingine wowote: UN Ripoti

Afya

Wanawake siku hizi wana uwezekano mkubwa kuliko wakati mwingine wowote wa kuishi wakati wa ujauzito na kujifungua, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa sanjari na sikuhii ya Afya Duniani.

Hata hivyo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuhusu hatari ya kurudi nyuma kwa mafanikio haya, huku kukiwa na upungufu wa msaada wa kibinadamu usio na kifani kote duniani.

Ripoti hiyo, “Mwendendo wa vifo wakati wa kujifungua” inaonesha kuwa kumekuwa na upungufu wa asilimia 40 wa vifo vya kina mama duniani kati ya mwaka 2000 na 2023 mafanikio yaliyotokana zaidi na kuboreshwa kwa upatikanaji wa huduma muhimu za afya.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kwamba kasi ya maendeleo hayo imepungua sana tangu mwaka 2016, na inakadiriwa kuwa takribani wanawake 260,000 walifariki mwaka 2023 kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito au kujifungua sawa na kifo kimoja cha mama kila dakika mbili.

Mitindo ya uwiano wa vifo vya uzazi (MMR) kulingana na eneo.
Chanzo: WHO/UNICEF/UNFPA/World Bank/UN Population Division
Mitindo ya uwiano wa vifo vya uzazi (MMR) kulingana na eneo.

Uhaba wa ufadhili ni mwiba kwa huduma

Ripoti hii imetolewa wakati ambapo upungufu wa ufadhili wa kibinadamu unaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma muhimu za afya katika sehemu nyingi duniani, na kulazimisha nchi kuacha au kupunguza huduma muhimu za afya kwa mama, watoto wachanga na watoto kwa ujumla.

Kwa mujibu wa WHO upungufu huu wa ufadhili umesababisha kufungwa kwa vituo vya afya, kupotea kwa watumishi wa afya, pamoja na kukatizwa kwa mnyororo wa usambazaji wa dawa na vifaa vya kuokoa maisha kama vile matibabu ya kutokwa damu nyingi, shinikizo la juu la la damu wakati wa mimba  au pre-eclampsia, na malaria  ambazo zote ni sababu kuu za vifo vya kina mama wajawazito.

Mashirika hayo yameonya kuwa Bila hatua za haraka wanawake wajawazito katika nchi nyingi, hasa zile zilizoko katika mazingira magumu ya kibinadamu, watakumbwa na athari kubwa ambapo tayari viwango vya vifo vya kina mama ni vya kutisha.

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema “Ingawa ripoti hii inaonesha mwanga wa matumaini, takwimu pia zinaangazia hatari kubwa ya ujauzito katika maeneo mengi duniani licha ya kuwepo kwa suluhisho la kuzuia na kutibu matatizo yanayosababisha vifo vingi vya kina mama.”

Ameongeza kuwa “Mbali na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za uzazi, ni muhimu pia kuimarisha haki za msingi za afya na uzazi kwa wanawake na wasichana mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika matokeo bora ya kiafya wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.”

Wakunga na wataalamu wengine wa afya katika Hospitali ya Uzazi ya Khartoum, Sudan.
© UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mouty
Wakunga na wataalamu wengine wa afya katika Hospitali ya Uzazi ya Khartoum, Sudan.

Athari za COVID-19 na changamoto zinazoendelea kwa afya ya mama

Ripoti hii pia inatoa kwa mara ya kwanza tathmini ya kimataifa kuhusu athari za janga la coronavirus">COVID-19 kwa maisha ya akina mama wajawazito.

Mwaka 2021, inakadiriwa kuwa wanawake 40,000 zaidi walifariki dunia kutokana na ujauzito au kujifungua na idadi hiyo iliongezeka hadi 322,000 kutoka 282,000 mwaka uliotangulia.

Kuongezeka huku kulitokana si tu na matatizo ya moja kwa moja yaliyoletwa na COVID-19, bali pia kutatizika kwa huduma za uzazi kote duniani limesema shirika la WHO.

Hii inaonyesha umuhimu wa kuhakikisha huduma za uzazi zinapatikana hata wakati wa majanga kama vile milipuko ya magonjwa limeongeza.

Wanawake wajawazito wanahitaji huduma za kawaida za uchunguzi, pamoja na huduma za dharura zinazopatikana saa ishirini na nne.

Kukata ufadhili kunaweka rejhani maisha ya mama na mtoto

Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF akiongeza sauti yake katika tripoti hiyo amesema “Mama anapofariki dunia wakati wa ujauzito au kujifungua, maisha ya mtoto wake pia huwa hatarini. Mara nyingi, wote hupotea kwa sababu ya matatizo tunayojua jinsi ya kuyazuia,”

Ameendelea kusema kuwapia “Kupunguzwa kwa ufadhili wa huduma za afya duniani kunawaweka wanawake wajawazito wengi zaidi hatarini, hasa katika maeneo yasiyojiweza kwa kuwanyima huduma muhimu wakati wa ujauzito na msaada wanaouhitaji wanapojifungua. Dunia inapaswa kuwekeza kwa dharura kwa wakunga, wauguzi na wahudumu wa afya wa jamii ili kuhakikisha kila mama na mtoto wana nafasi ya kuishi na kustawi.”

Mwanamke mjamzito anakaguliwa katika kliniki tembezi kusini mwa Madagaska.
UN News/Daniel Dickinson
Mwanamke mjamzito anakaguliwa katika kliniki tembezi kusini mwa Madagaska.

Usawa na tofauti za Kikanda

Ripoti inaonyesha tofauti kubwa za maendeleo kati ya kanda na nchi mbalimbali. Ingawa vifo vya kina mama wajawazito vilipungua kwa karibu asilimia 40 kati ya mwaka 2000 na 2023, kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ilipata mafanikio makubwa ikiwa miongoni mwa kanda tatu za Umoja wa Mataifa pamoja na Australia na New Zealand, na Asia ya Kati na Kusini zilizoonesha upungufu mkubwa wa vifo baada ya mwaka 2015.

Hata hivyo, kutokana na umasikini uliokithiri na mizozo mingi, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara bado ilibeba takriban asilimia 70 ya vifo vyote vya kina mama duniani mwaka 2023.

Katika kanda tano, maendeleo yalisimama baada ya mwaka 2015, Afrika Kaskazini na Asia ya Magharibi, Asia Mashariki na Kusini Mashariki, Oceania isipokuwa Australia na New Zealand, Ulaya na Amerika Kaskazini, pamoja na Amerika ya Kusini na Karibea.

Huduma bora za afya ni haki sio anasa

“Upatikanaji wa huduma bora za afya ya uzazi ni haki ya kila mtu, siyo anasa,” amesema Dkt. Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA.

Ameongeza kuwa “Kwa kuimarisha minyororo ya usambazaji wa vifaa, nguvu kazi ya wakunga, na ukusanyaji wa takwimu zenye maelezo ya kina kuhusu walioko hatarini zaidi, tunaweza, na lazima kumaliza janga la vifo vya kina mama vinavyoweza kuzuilika.”

Mwanamke mjamzito akipokea huduma katika kituo cha Jumuiya ya Usaidizi ya Kimatibabu ya Palestina katika Jiji la Gaza.
© UNFPA Palestine/Yasmeen Sous
Mwanamke mjamzito akipokea huduma katika kituo cha Jumuiya ya Usaidizi ya Kimatibabu ya Palestina katika Jiji la Gaza.

Wanawake katika mazingira ya dharura

Wanawake wajawazito walioko kwenye mazingira ya dharura wanakabiliwa na hatari kubwa duniani kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Takribani theluthi mbili ya vifo vyote vya kina mama hutokea katika nchi zilizoathiriwa na migogoro au hali ya hatari.

Kwa wanawake hawa, hatari ni ya kutisha:

  • Msichana wa miaka 15 katika mazingira haya ana uwezekano wa mtu 1 kati ya 51 kufariki dunia kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi katika maisha yake, ikilinganishwa na mtu1 kati ya 593 katika nchi zenye utulivu.

Nchi zilizo na hatari kubwa zaidi ni:

  • Chad mtu 1 kati ya 24
  • Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR mtu 1 kati ya 24
  • Nigeria mtu 1 kati ya 25
  • Somalia mtu 1 kati ya 30
  • Afghanistan mtu 1 kati ya 40
WHO Tanzania kupitia huduma za dharura za afya yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua. (Maktaba)
WHO
WHO Tanzania kupitia huduma za dharura za afya yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua. (Maktaba)

Mbali na huduma za uzazi

Ripoti inaeleza kuwa kuboresha afya ya wanawake kwa ujumla ni muhimu kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, kuzuia magonjwa kama vile upungufu wa damu au anemia, malaria, na magonjwa yasiyoambukiza ambayo huongeza hatari ya vifo wakati wa ujauzito.

Vilevile, imesema ni muhimu kuhakikisha wasichana wanamaliza shule, na wanawake na wasichana wana maarifa na rasilimali za kulinda afya yao.

Ripoti imeonya kwamba“Dunia haipo kwenye njia sahihi ya kufikia lengo la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa kuhusu kuokoa maisha ya kina mama wajawazito ifikapo mwaka 2030. Ili kufikia lengo hilo, uwiano wa vifo vya uzazi duniani unapaswa kupungua kwa asilimia 15 kila mwaka, ikilinganishwa na kiwango cha sasa cha upungufu wa takribani asilimia 1.5 kwa mwaka.”

Pia ripoti imesisitiza kuwa Uwekezaji wa haraka na wenye mashiko unahitajika sio kwa sababu tu ya afya ya mama, bali kwa ajili ya ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.