Mapito ya wajawazito huko Goma, DRC; UNFPA ni mkombozi
Mapito ya wajawazito huko Goma, DRC; UNFPA ni mkombozi
Chance Azina alitembea polepole katika mitaa ya Goma, jimboni Kivu Kaskazini, mwili wake ukiwa umeelemewa na joto kali akiwa na ujauzito wa miezi saba. Kama wengine wengi, alikuwa anajaribu kuendeleza hali ya kawaida ya maisha licha ya kuwa amepoteza makazi mara kadhaa kutokana na mapigano makali yaliyoshamiri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kupitia chapisho kwenye wavuti wake, UNFPA ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya uzazi, kile Bi. Azina hakukijua ni kwamba bila huduma ya haraka ya afya, ujauzito na kujifungua kwake vinaweza kuwa na madhara ikiwemo kifo.
Akiwa anatembea, kwenye kona iliyofuata alikutana na Amani, mfanyakazi wa kuelimisha jamii kutoka kituo cha afya cha Kyeshero Christian Centre for the Light. Amani alikuwa akizungumza na wapita njia ili kutoa elimu kuhusu huduma za afya ya uzazi zilizopo.
“Aliponiuliza kuhusu maumivu ya kichwa na miguu, nilihofia. Hivyo ndivyo nilivyokuwa nikihisi,” Bi. Azina ameiambia UNFPA.
Alienda haraka kupimwa, akipokea huduma ya bure kutoka kwa wakunga waliopatiwa mafunzo na msaada wa UNFPA.
“Alikuwa na maumivu makali ya kichwa na miguu, lakini hakuwa ameonana na mtoa huduma ya afya tangu mwanzo wa ujauzito wake,” ameeleza Justine, mmoja wa wakunga kwenye kituo hiki akiongeza kuwa, “tulifanya vipimo mara moja ili kuondoa uwezekano wa kifafa cha mimba.”
Baada ya kuondoka kambini amejisitiri kwa wenyeji
Huduma ya kabla ya kujifungua ilikuwa haiwezekani kupatikana katikati ya ghasia ambazo zimelazimisha mamia kwa maelfu ya watu mjini Goma, mashariki mwa DRC kukimbia kwa hofu.
Kijiji chake cha Kanihi, wilayani Masisi, kilishambuliwa mwezi Desemba mwaka 2024, na Bi. Azina pamoja na watoto wake wanne walitembea zaidi ya kilomita 90 hadi kufika kambi ya wakimbizi ya Bulengo mjini Goma.
Lakini walifukuzwa baada ya maeneo mengi yaliyokuwa yakiwahifadhi wakimbizi kufungwa na waasi wa M23 mwezi Februari, wakitaka raia warejee kwenye vijiji vyao.
Familia hiyo ilihamia katika kambi nyingine pamoja na maelfu ya watu wengine. Hatimaye, familia mwenyeji ilimruhusu yeye na watoto wake kuishi pamoja kwenye chumba chao kidogo huko Kyeshero. Na tangu mumewe atoweke miezi michache iliyopita, amekuwa akikabiliana na ujauzito wake wa hatari peke yake.
Hali halisi inayowakumba maelfu ya wanawake
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huduma za afya ya uzazi zilikuwa haba hata kabla ya mzozo huu wa karibuni, na nchi hii ina viwango vya juu sana vya vifo vya akina mama wajawazito.
Sasa, huko Kivu Kaskazini na Kusini, hospitali tatu tu ndizo zinazofanya kazi, zote zikiwa zimelemewa na uhaba wa vifaa muhimu, wafanyakazi, umeme na mafuta ya magari ya wagonjwa. Hii ina maana kuwa wanawake wengi wanalazimika kujifungua nyumbani bila msaada wowote.
Wajawazito huchelewa kuanza huduma ya kliniki
Ripoti zinaonesha kuwa chini ya nusu ya wanawake wajawazito kabla ya kujifungua wanaweza kuhudhuria kliniki mara 4, idadi inayopendekezwa; na kati yao, wengi huenda kwa mara ya kwanza wakiwa tayari wamechelewa mno kuzuia matatizo. Wengi zaidi hawana elimu kuhusu dalili hatarishi kama vile uzito mdogo, upungufu wa damu, shinikizo la juu la damu, na maumivu makali ya kichwa – yote yakiwa ishara za matatizo ya afya yanayoweza kuhatarisha maisha.
Kabla ya kukutana na Amani, Bi. Azina hakujua kuwa maumivu aliyokuwa nayo yangeweza kuhatarisha maisha yake na ya mtoto wake.
“Wanawake wengi huhisi hawawezi tena kusaidiwa baada ya kutoka kambini,” ameeleza Dkt. Solange N. Ngane, anayefanya kazi na UNFPA huko Kivu Kaskazini. “Wafanyakazi wetu wa jamii wana jukumu muhimu la kutoa elimu na mwongozo kwa wanawake walioko hatarini zaidi.”
Wahudumu wa kijamii wanaofadhiliwa na UNFPA, hutoa elimu, na kuwaelekeza wanawake wajawazito kwenye vituo vya afya washirika kwa ajili ya huduma za kabla ya kujifungua, upangaji uzazi, na matibabu kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia. Hii huwezesha waliotengwa kabisa kurejeshwa kwenye mfumo wa huduma za afya, hata nje ya kambi za wakimbizi.
Majawabu endelevu ya kunusuru wajawazito na watoto
Tangu mwezi Februari mwaka huu wa 2025, UNFPA imetuma wakunga 120 na wafanyakazi wa jamii 360 kote Goma kuhakikisha huduma hazikatizwi na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.
Sasa Bi. Azina sasa anaendelea na uchunguzi wa mara kwa mara na ana uelewa zaidi wa hatari na mahali pa kupata msaada wakati wa dharura. “Nilifikiri ningejifungua peke yangu, kama nyakati zilizopita,” amesema. “Sikujua kama msaada bado ulikuwepo – ni yule kijana niliyemkuta barabarani ndiye aliyeniokoa.”
Bi. Azina ni ushahidi kwamba hata wakati mgogoro unavyozidi, taarifa moja au sikio la kusikiliza linaweza kuokoa maisha. Kote nchini DRC, UNFPA inaendelea kutoa elimu, kusambaza vifaa vya afya ya uzazi, kuimarisha mifumo ya uhamisho kwa dharura za uzazi, na kuendesha maeneo salama kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia.
Madhara ya kukatwa kwa usaidizi kutoka Marekani
Marekani imekuwa mfadhili muhimu na mkarimu kwa programu hizi, lakini kusitishwa kwa ufadhili hivi karibuni kutawaathiri watu takribani milioni 11 – zaidi ya milioni 3 huko Kivu Kaskazini pekee – huku washirika wakilazimika kupunguza shughuli katika moja ya migogoro isiyofadhiliwa vya kutosha duniani.
Kliniki tembezi za afya pia zimesitishwa katika maeneo kadhaa kutokana na hali ya usalama, na viwango vya juu kabisa vya njaa kali vilivyowahi kurekodiwa nchini vinamaanisha kuwa wanawake na wasichana – hasa wajawazito na akina mama wapya – wanakabiliwa na vitisho vikubwa zaidi kwa maisha yao.
UNFPA sasa inatoa wito wa dharura wa dola za Kimarekani milioni 18 za kutumiwa kuanzia Februari hadi Agosti 2025 ili kuendeleza huduma za kuokoa maisha na kulinda watu walioko hatarini zaidi huko jimbonk Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.