Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bunju Women Tanzania: Mfano wa mafaniko ya Mfuko wa CRDB katika kutekeleza SDGs

Wanachama wa Kikundi cha Wanawake cha Bunju Women nchini Tanzaina wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa CRDB Tully Esther Mwambapa wakiwa katika picha ya pamoja jijini Dar Es Salaam.
CRDB Tanzania
Wanachama wa Kikundi cha Wanawake cha Bunju Women nchini Tanzaina wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa CRDB Tully Esther Mwambapa wakiwa katika picha ya pamoja jijini Dar Es Salaam.

Bunju Women Tanzania: Mfano wa mafaniko ya Mfuko wa CRDB katika kutekeleza SDGs

Wanawake
  • Mfuko wa CRDB Tanzania wawezesha wanawake kupata mikopo nafuu
  • Wanawake wamejikomboa kiuchumi na sasa wanakomboa vijana
  • Mfuko unawaunganisha wanavikundi na masoko ya bidhaa zao

Mfano wangu ni Jackline Mkina, kiongozi wa kikundi cha Wanawake Bunju. Kupitia umoja wao wamekuza biashara zao ambapo awali waliendesha biashara za ndani lakini sasa wanasafiri mpaka nje ya Tanzania kwenda kununua bidhaa na kuuza nchini."

Audio file

Utajiuliza ni jambo gani linazungumziwa hapa! Ni suala la uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi nchini Tanzania kupitia Mfuko wa CRDB unaoongozwa na Tully Esther Mwambapa aliyetoa kauli hiyo kuhusu mafanikio ya kampuni hiyo tanzu ya Benki ya CRDB nchini Tanzania.

Bi. Mwambapa alikuweko makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kushiriki mkutano wa 69 wa Hali ya Wanawake duniani, CSW69 ambapo Assumpta Massoi alizungumza naye kuweza kufahamu ni kwa vipi wanasongesha Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji vilivyopitishwa mwaka 1995 huko Beijing nchini China, ambavyo vilikuwa maudhui ya mkutano wa CSW69.

Tweet URL

Ndipo alipotoa mfano wa Bi. Mkina mnufaika wa mafunzo na mikopo inayotolewa na Mfuko wa CRDB kwa vikundi vya wanawake na vijana.

“Kupitia Mfuko wa CRDB. tumejikita katika kuwapatia wanawake na vijana mafunzo ya kifedha na biashara, pamoja na kuwawezesha kujiunga na vikundi vya kiuchumi ili kupata mitaji wezeshi. Mpango huu, unaojulikana kama IMBEJU umenufaisha wanawake takriban 800,000  katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu,” amesema Bi. Mwambapa.

Riba inayoingia pia kwenye bima ya maisha

Kati yao hao, 300,000 wamepokea mikopo yenye riba nafuu ya 7%,  ambapo 1% inatumika kwa bima ya maisha.

Kwa mujibu wa Bi. Mwambapa, mfumo wa bima umeundwa kuhakikisha kuwa mkopo unalipwa endapo mkopaji atapata ulemavu wa kudumu au kufariki dunia, hivyo kuondoa mzigo kwa familia yake.

“Mpango huu unalenga wanawake na vijana wanaojihusisha na kilimo, biashara ndogondogo na shughuli nyingine za kiuchumi, kwa kushirikiana na maafisa maendeleo wa serikali,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mfuko wa CRDB.

Kutafutia wanavikundi masoko ya mazao

Katika kufanikisha mipango yao, Mfuko wa CRDB hushirikiana na kampuni kutafutia wanakikundi masoko ya bidhaa zao ikiwemo za kilimo.

“Tunashirikiana na kampuni kubwa kama Tanzania Breweries ili kuwasaidia wakulima wa shayiri katika maeneo ya Mbulu, West Kilimanjaro na Monduli. Ushirikiano huu unahusisha utoaji wa mbegu bora, mafunzo ya kilimo, na mikopo yenye masharti nafuu, ambayo mkulima huanza kulipa baada ya kupata malipo kutoka kwa wanunuzi wakuu kama Tanzania Breweries,” amesema Bi. Mwambapa.

Bunju Women: Kutoka kuwezesha wanawake hadi vijana

Alipoulizwa iwapo kuna mfano wa mafanikio, Bi. Mwambapa amesema ni mingi kati ya hao 800,000 walionufaika, “lakini naweza kumtaja mmoja kwa sababu ya muda.”

Mfano wa mafanikio ya mpango huu ni Bi. Jackline Mkina wa Bunju, ambaye kupitia umoja wao wameweza kukuza biashara zao kutoka kununua na kuuza bidhaa ndani ya Tanzania hadi kufanya biashara za kimataifa.

“Bi. Mkina na kundi lake walianza kwa kuchukua mikopo ya milioni 5, lakini sasa wamefikia kiwango cha mikopo ya hadi milioni 50. Mbali na mafanikio yao binafsi, wamepanua mpango huu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kifedha na biashara,"  amesema Bi. Mwambapa.

Ametamatisha kwa kusema kuwa hatua hii inaonesha mafanikio makubwa ya programu ya IMBEJU na jinsi inavyowezesha wanawake na vijana wa Tanzania kuwa huru kiuchumi na kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa taifa.