Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF, NORAD na wadau Kenya waelekea kufanikisha ndoto ya Sharlyne kuwa mwandishi wa habari

Sharlyne Kapua, Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya.
UNICEF
Sharlyne Kapua, Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya.

UNICEF, NORAD na wadau Kenya waelekea kufanikisha ndoto ya Sharlyne kuwa mwandishi wa habari

Utamaduni na Elimu

Kutana na Sharlyne Kaputa, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 kutoka kaunti ya Turkana, Kaskazini-Magharibi mwa Kenya. Tofauti na shangazi yake, ambaye hakuweza kuendelea na elimu  yake kutokana na kukosa karo, yeye anasoma elimu ya sekondari sasa ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa mwandishi wa habari. Yote yanawezekana kutokana na mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa msaada wa shirika la Norway la Maendeleo NORAD na wadau wengine. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Kenya, inatupeleka kaunti ya Turkana, iliyoko kaskazini magharibi mwa taifa hili la Afrika Mashariki. Ni kaunti ambayo imekuwa ikigubikwa na matukio mazito ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi! Ukame! Mafuriko! na hivyo kuvuruga mbinu za watu kujipatia kipato na vile vile familia kulazimika kuhama.

Kuhama kwa familia kunamaanisha watoto nao wanalazimika kuacha shule na kuambatana na familia zao na  hata kujikita kwenye shughuli za kuhudumia familia zao! Hali hii inaweka mashakani fursa yao ya kupata elimu kwani wanakumbana na changamoto zingine.

Shangazi asema Sharlyne  ndio 'jicho' lake sasa

Sharlyne Kapua anajitambulisha akiwa kwenye shule hiyo ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana. Yeye ana umri wa miaka 16 na ni yatima kwani wazazi wake walifariki dunia akiwa na umri mdogo. Anataja changamoto hizo zinazokumba watoto wa kike kwenye jamii yao kuwa ni pamoja na utoro shuleni, ndoa za mapema na ujauzito katika umri mdogo.

Sharline Kapua, Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya, na Sopia Akuyoit (kushoto), shangazi ambaye sasa ndiye mlezi wa Sharlyne.
UNICEF
Sharline Kapua, Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya, na Sopia Akuyoit (kushoto), shangazi ambaye sasa ndiye mlezi wa Sharlyne.

Changamoto hizi zinawekwa  bayana zaidi na Sopia Akuyoit shangazi ambaye sasa ndiye mlezi wa Sharlyne.

“Miaka 15 iliyopita matatizo ambayo mimi niliona wasichana kwenye hiki kijiji wanapitia ni ile hali ya kukosa elimu, na wengine kuingia kwenye kuolewa.”

Lakini ni kwa vipi Sharlyne mwenye umri wa miaka 16 sasa aliweza kuepuka matatizo hayo?

“Nimeweza kuepuka vyote hivyo kupitia mwongozo wa karibu kwa wazazi wangu, vijana wa rika langu na pia walimu wangu.”

Sababu ya Sharlyne kuruka viunzi vinavyoangusha wasichana

Je hilo liliwezekana vipi? Ni kwamba UNICEF kupitia video yake inasema kuwa shirika la kimataifa la maendeleo la Norway, NORAD pamoja na UNICEF na wadau wameweze kutekeleza programu za kuwezesha mtoto wa kike kwenye maeneo yenye dharura kama zile za tabianchi, sio tu kuandikishwa shule bali pia kusalia hadi kuhitimu masomo yake.

Margaret Njayakio, Afisa Elimu wa UNICEF Kenya anasema wanatekeleza programu hizo sambamba na zile za kuwashawishi watoto wa kike kusoma STEM, yaani Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati. Vile vile wanawapatia elimu ya kidijitali na stadi za maisha.

Programu nyingine ni kama zile za usafi na kujisafi wakati wa hedhi kwa kuwawekea maji safi na salama shuleni na pia kuwapatia vifaa vya kujifunzia.

Sharlyne Kapua (kulia), Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya.
UNICEF Kenya
Sharlyne Kapua (kulia), Msichana mwenye umriwa miaka 16 akiwa kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Katilu hapa Turkana nchini Kenya.

Nataka watoto wote wa kike wapate elimu

Video inatupeleka darasani, Sharline anasikiliza na kufuatilia kwa makini mwalimu na kisha anafunguka ndoto yake.

“Nitakapokuwa mtu mzima, nataka kuwa mwandishi wa habari ili nisafiri duniani ili nisimulie kuhusu watoto wa kike wanaopitia uzoefu kama huu.”

Na sasa ni fursa ya shangazi yake Sharlyne, Sophia akisema, “wakati nilipokuwa na umri wa miaka 15 matarajio yangu  yalikuwa nisome, nihitimu ili niweze kusaidia wadogo zangu. Nilikosa fedha ya kuendelea mbele kwani niliishia kidato cha 4. Nikiangalia Sharlyne sasa hivi kile kiwango amefika niña furaha kubwa sasa kwa sababu gani? Kwa sababu yeye ndiye macho yangu sasa hivi.”

Na Sharlyne anaona kuna mabadiliko makubwa Turkana na anazungumza kwa kujiamini akiwa amevalia sare yake ya shule, shati jeupe, sketi ya buluu, tai ya buluu, soksi nyeupe na viatu vyeusi akisema, “kitu kimoja kilichobadilika ndani ya miaka 15 kwenye kaunti hii ni kwamba elimu. Kama nikipatiwa fursa ya kubadili jambo moja kwenye jamii yangu ni kuwapatia fursa ya watoto wote wa kike elimu, waweze kwenda shuleni. Mimi na wanarika wenzangu tunaweza kwenda shuleni kupata elimu tofauti na zamani.”

Soundcloud

Video inatamatika Sharlyne akiwa na shangazi yake wote wakitabasamu!