Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usonji ni nini? - WHO

Siku ya Uelewa kuhusu Usonji Duniani huadhimishwa na UN kila mwaka tarehe 2 Aprili.
© Unsplash/Annie Spratt Siku ya Uelewa kuhusu Usonji Duniani huadhimishwa na UN kila mwaka tarehe 2 Aprili.

Usonji ni nini? - WHO

Afya

Usonji, ugonjwa ambao pia inajulikana tatizo la ukuaji waubongo (ASD), ni muunganiko wa  hali zinazohusiana na ukuaji wa ubongo. Usonji unajulikana kwa changamoto katika mwingiliano wa kijamii, mawasiliano, na tabia za kujirudia. Uwezo na mahitaji ya watu wenye Usonji hutofautiana sana, ambapo baadhi yao wanaweza kuishi kwa kujitegemea, huku wengine wakihitaji msaada kwa maisha yao yote.

Takiwmu kuhusu Usonji

Kwa mujibu wa takiwmu za Shirika la Umoja wa Mataifa la afya Duniani WHO, Usonji huathiri takriban mtoto 1 kati ya 100 ulimwenguni kote. Ingawa dalili za Usonji zinaweza kuonekana mapema utotoni, mara nyingi utambuzi hufanyika baadaye. WHO inasema ugunduzi wa mapema na uingiliaji kati unaweza kuboresha mawasiliano na mnepo wa kijamii dhidi ya ugonjwa huo, na hivyo kuimarisha ustawi wa watu wenye Usonji pamoja na walezi wao.

Kutambua tatizo la Usonji kwa kawaida kunategemea vyanzo viwili vikuu vya taarifa: maelezo ya wazazi au walezi kuhusu maendeleo ya mtoto wao na uchunguzi wa kitaalamu wa tabia ya mtoto

Licha ya kwamba ana usonji, wazazi wa Chadron (pichani) wanahakikisha kuwa anapata vifaa vinavyomwezesha kujifunza.
UN News Video Licha ya kwamba ana usonji, wazazi wa Chadron (pichani) wanahakikisha kuwa anapata vifaa vinavyomwezesha kujifunza.

Hali zinazoambatana na Usonji

Watu wenye Usonji wanaweza kupata ugumu wa kuhama kutoka shughuli moja hadi nyingine, kuzingatia maelezo madogo madogo, na kuwa na hisia za kipekee kwa masuala mbalimbali. Zaidi ya hayo, mara nyingi wanakumbana na hali zingine kama vile kifafa, msongo wa mawazo, wasiwasi, ADHD, na matatizo ya usingizi. Uwezo wa kiakili miongoni mwa watu wenye Usonji hutofautiana sana, kuanzia upungufu mkubwa wa uelewa hadi viwango vya juu vya uwezo wa kiakili.

Chanzo na dhana potofu

WHO inasema utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa Usonji husababishwa na mchanganyiko wa sababu za kijenetiki na kimazingira. Ni muhimu kupinga dhana potofu kuwa chanjo husababisha Usonji kwani tafiti zimepinga kabisa uhusiano huo. Chanjo, zikiwemo zile zenye thiomersal au alumini, haziongezi hatari yakupata Usonji.

Umuhimu wa huduma na msaada unaopatikana

Watu wenye Usonji wanahitaji huduma mbalimbali za afya na msaada wa kijamii unaoendana na mahitaji yao yanayobadilika. Uingiliaji wa hatua mapema na wa kisaikolojia unaotegemea ushahidi unaweza kuboresha sana kiwango cha maisha ya watu wenye Usonji. Ushirikiano kati ya sekta za afya, elimu, na kijamii ni muhimu ili kuhakikisha huduma sahihi na ujumuishwaji.

Teresita (kushoto), daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, anaona michezo kama njia ya kukuza ujuzi wa kimwili na kitabia kwa watoto wenye usonji.
UNIC Cuba Teresita (kushoto), daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, anaona michezo kama njia ya kukuza ujuzi wa kimwili na kitabia kwa watoto wenye usonji.

Msaada wa Jamii na Kijamii

Kuunda jamii jumuishi kunahitaji hatua za jamii na serikali ili kukuza fursa za ufikiaji wa watu wenye Usonji, kukubalika, na msaada kwa watu wenye Usonji pamoja na walezi wao. Juhudi zinapaswa kuelekezwa katika elimu, fursa za ajira, na uhamasishaji wa umma ili kukuza mazingira yenye uelewa na yanayojali.

Ahadi ya WHO kwa uhamasishaji kuhusu Usonji

Shirika la WHO limejitolea kuboresha maisha ya watu wenye Usonji kwa:

  • Kuhimiza serikali kutilia maanani msaada na sera zaUsonji.
  • Kutoa mwongozo kuhusu sera za afya na ulemavu.
  • Kuimarisha huduma za afya ili kutoa huduma zinazofaa na madhubuti.
  • Kukuza mazingira jumuishi na msaada kwa walezi.

Chukua hatua leo

WHO inasema unaweza kusaidia watu wenye Usonji kwa kutetea ujumuishaji, kuchagiza uingiliaji wa mapema, na kuhimiza uelewa katika jamii yako.  Kwani pamoja, tunaweza kuunda dunia inayothamini na kusaidia watu wenye autism kufikia uwezo wao kamili.