Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa kuhusu Zama Zijazo za Nchi Zenye Maendeleo Duni (LDCs) 2025 lafanyika Zambia

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF unasaidia kuwawezesha kiuchumi wanawake katika nchi 46 zinazoendelea, (LDCs)
UNCDF
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF unasaidia kuwawezesha kiuchumi wanawake katika nchi 46 zinazoendelea, (LDCs)

Jukwaa kuhusu Zama Zijazo za Nchi Zenye Maendeleo Duni (LDCs) 2025 lafanyika Zambia

Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa la tatu Kuhusu Zama Zijazo za LDCs yaani Nchi Zenye Maendeleo Duni limeanza leo jijini Lusaka, Zambia, likikusanya watunga sera, watafiti, sekta binafsi, na wadau wengine ili kuandaa njia kuelekea maendeleo endelevu na ustahimilivu kwa mataifa yaliyo hatarini zaidi duniani.

Taarifa iliyotolewa leo Aprili Mosi jijini New York, Marekani na Lusaka, Zambia imeeleza kuwa maafisa waandamizi wa serikali na wataalamu kutoka nchi 44 zilizo na maendeleo duni (LDCs) wamekusanyika kwa ajili ya jukwaa hili la siku tatu (1-3 Aprili) kubadilishana suluhu bunifu na mapendekezo ya sera za vitendo zinazolenga kuimarisha mnepo wa LDCs.

Jukwaa hili la tatu baada ya mawili yaliyofanyika nchini Finland (mwaka 2021 na 2024) kaulimbiu yake ya sasa ni "Kuimarisha Ustahimilivu: Suluhisho Bunifu kwa Kuimarisha Uwezo wa LDCs Kukabiliana na Mitikisiko ya Kisekta," na linahusiana na Kipaumbele cha 5 cha Mpango wa Utekelezaji wa Doha (DPoA), ambacho kinajikita katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, kupona kutokana na janga la coronavirus">COVID-19, na kujenga ustahimilivu dhidi ya changamoto za siku zijazo kwa maendeleo endelevu yanayozingatia hatari zote.

Likiwa limeandaliwa na UN-OHRLLS, Serikali ya Finland, na Serikali ya Zambia, kwa kushirikiana na UNU-WIDEROECD na Ferdi, jukwaa hili litajumuisha Mazungumzo ya Ngazi ya Juu yatakayosisitiza haja muhimu ya ufadhili ili kuimarisha ustahimilivu wa LDCs dhidi ya changamoto mbalimbali.

Changamoto za LDCs 

LDCs mara nyingi zinakabiliwa na rasilimali za ndani zisizotosha, hali inayozuia uwezo wao wa kustahimili mdororo wa uchumi, majanga ya asili, na dharura za kiafya. Aidha, kupata masoko ya kimataifa ya mitaji ni changamoto kwao kutokana na ukosefu wa uaminifu wa kifedha na hatari zinazodhaniwa kuwapo. Ushiriki wa wanawake na wasichana katika mijadala hii utakuwa muhimu kwa kuendeleza suluhisho shirikishi na jumuishi.

Maoni ya Viongozi

Bi. Rabab Fatima, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Juu wa Nchi Zenye Maendeleo Duni, Nchi Zisizopakana na Bahari, na Nchi Ndogo za Visiwa Zinazoendelea, anasisitiza umuhimu wa jukwaa hili akisema: "Jukwaa la Zama Zijazo za LDC linakutana kwa mara ya kwanza katika moja ya nchi zilizo na maendeleo duni, likitoa fursa ya kipekee kuhamasisha msaada wa kimataifa kwa mataifa yaliyo hatarini zaidi duniani katika kukabiliana na mazingira yanayobadilika kila wakati. Kwa kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali, jukwaa hili linapania kuunda njia za utekelezaji zinazolenga kuimarisha ustahimilivu wa LDCs dhidi ya mitikisiko ya kimfumo."

Ville Tavio, Waziri wa Biashara ya Nje na Maendeleo wa Finland, anasisitiza dhamira ya Finland kusaidia LDCs kupitia juhudi za pamoja akisema:  "Jukwaa hili ni fursa nzuri kwa wadau mbalimbali kushiriki suluhisho madhubuti na mapendekezo ya sera za vitendo ili kuboresha ustahimilivu wa LDCs. Kwa msisitizo maalum juu ya usawa wa kijinsia, majadiliano haya yatachangia katika kuunda suluhisho jumuishi na endelevu. Finland inajivunia kushirikiana kuandaa jukwaa hili hapa Lusaka, na ninafurahia kushiriki pamoja na wawakilishi wengi wa Kifini."

Mulambo Haimbe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, anasema:  "Uenyeji wa Jukwaa la Zama Zijazo zaLDCs hapa Lusaka ni uthibitisho wa dhamira ya Zambia katika kusukuma mbele maslahi ya nchi zilizo na maendeleo duni. Jukwaa hili litatoa jukwaa la kuandaa suluhisho linalowawezesha wananchi wetu, kuimarisha uchumi wetu, na kujenga ustahimilivu dhidi ya changamoto za baadaye."

Dkt. Situmbeko Musokotwane, Waziri wa Fedha wa Zambia, anaongeza kwamba:  "Jukwaa hili ni mwito wa kuchukua hatua kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia LDCs kufanikisha matarajio yao ya maendeleo. Kwa kuhimiza uvumbuzi, ushirikiano, na ufadhili endelevu, tunaweza kujenga uchumi imara unaostahimili mitikisiko ya kimfumo na kuunda fursa kwa wote."

Lok Bahadur Thapa, Mwakilishi wa Kudumu wa Nepal katika Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la LDCs, yeye anasema: "Jukwaa hili ni fursa ya kipekee ya kuimarisha ushirikiano, kushiriki suluhu bunifu, na kuongeza sauti ya pamoja ya LDCs katika ngazi ya kimataifa. Pamoja, lazima tuhakikishe kuwa changamoto zinazowakabili walio hatarini zaidi zinashughulikiwa kwa ahadi madhubuti na mikakati ya utekelezaji, bila kumwacha yeyote nyuma katika safari yetu ya mafanikio na ustahimilivu."

Mambo muhimu katika Jukwaa

Jukwaa hili litakuwa na vikao vinne vya mada vinavyoangazia maeneo muhimu yafuatayo:

1. Kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi ili kuboresha uhakika wa chakula na kuhakikisha maendeleo endelevu ya kilimo.

2. Suluhu endelevu za maji na nishati kwa ajili ya kuimarisha ustahimilivu.

3. Uchumi wa mzunguko na viwanda vinavyozingatia mazingira ili kukuza utofauti wa uchumi na mnepo.

4. Mipango ya ulinzi wa kijamii yenye malengo mahsusi ili kuimarisha ustahimilivu dhidi ya changamoto nyingi.

Pia, Mazungumzo ya Ngazi ya Juu yataangazia mikakati ya ufadhili kwa ajili ya kusaidia uchumi thabiti katika LDCs, na kushughulikia hitaji muhimu la rasilimali kukabiliana na mdororo wa uchumi, majanga ya asili, na dharura za kiafya.

Zaidi ya hayo, Mazungumzo ya Wazi na Sekta Binafsi yatachunguza jinsi biashara zinaweza kusaidia mpito kuelekea uchumi wa mzunguko, kuhimiza maendeleo endelevu na ustahimilivu katika LDCs.

Kwa maelezo zaidi kuhusu jukwaa, tafadhali tembelea tovuti rasmi: (https://www.un.org/ohrlls/ldc-future-forum-2025).