Vurugu na ukosefu wa usalama viamethiri huduma zetu DRC - Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu UN
Vurugu na ukosefu wa usalama viamethiri huduma zetu DRC - Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu UN
Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nada Al-Nashif, amewasilisha ripoti leo hii akiwa katika Ofisi za Umoja wa Mataifa za Geneva, Uswisi akiangazia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuongezeka kwa vurugu na janga la kibinadamu mashariki mwa DRC kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda.
Kuongezeka kwa vurugu na janga la kibinadamu
Al-Nashif amesisitiza kuwa mashambulizi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yameongeza hali mbaya zaidi. "Kiwango cha vurugu na ukosefu wa usalama kimeathiri uwezo wa Ofisi yetu kutekeleza majukumu yake ipasavyo," amesema. Pamoja na changamoto hizi, juhudi zinaendelea kusaidia utawala wa sheria, haki ya mpito, na kupambana na hali ya kutoadhibiwa kwa wahalifu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takribani waathiriwa 602 wamethibitishwa kuuawa kwa njia zisizo za kisheria na mauaji yaliyofanywa na pande zote za mzozo katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini tangu mwanzoni mwa mwaka. Katika jimbo la Ituri, makundi kadhaa ya waasi yanaendelea kuua,kulemaza na kuwateka nyara raia.
Ukatili wa kijinsia na uhaba wa chakula
Naibu Kamishna Mkuu ameeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia unaohusiana na vita, ambapo visa vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 270 kati ya Januari na Februari. Aidha, karibu watu milioni 26, karibu robo ya idadi ya watu nchini, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Takriban watu milioni 7.8 wamekosa makazi, wakiwemo milioni 3.8 katika majimbo ya Kivu pekee. Maelfu ya shule zimefungwa, kuharibiwa, au kutawaliwa na makundi yenye silaha, na zaidi ya watoto milioni 1.6 mashariki mwa DRC wameachwa bila elimu.
Wito wa amani endelevu na uwajibikaji
Al-Nashif amesisitiza umuhimu wa kushughulikia chanzo cha mgogoro, hasa unyonyaji haramu wa rasilimali asili. Ametoa wito kwa mamlaka za DRC kuchukua hatua thabiti dhidi ya ufisadi, hali ya kutoadhibiwa kwa wahalifu, na kauli za chuki. Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia juhudi za haki ya mpito, ikiwa ni pamoja na mashauriano ya kitaifa na marekebisho ya Sheria ya Jinai ili kufanya kauli za chuki kuwa kosa la jinai.
Amesisitiza kuwa "baada ya karibu miongo mitatu ya vita na vifo vya zaidi ya watu milioni sita, inapaswa kuwa wazi kabisa kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwa mzozo huu." Badala yake, amehimiza viongozi wa kitaifa na kikanda kuweka mbele mazungumzo badala ya vurugu na maslahi binafsi.
Wito wa amani kwa jumuiya ya kimataifa
Al-Nashif ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha amani ya kudumu nchini DRC. Amewataka mataifa na kampuni binafsi zinazofaidika na rasilimali zinazonyonywa kinyume cha sheria kuacha kujificha nyuma ya minyororo tata ya usambazaji.
"Bila hatua madhubuti, vurugu za sasa zinaweza kusambaa katika eneo zima. Hatari za janga kama hilo zinaongezeka kila siku," ameonya, akisisitiza kuwa uwajibikaji kwa mateso ya raia ni jambo la lazima. Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa ujumbe thabiti kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kimataifa lazima vikome na kushughulikiwa ipasavyo.