Watoto 100 wauawa au kujeruhiwa kila uchao huko Gaza katika siku 10 zilizopita
Watoto 100 wauawa au kujeruhiwa kila uchao huko Gaza katika siku 10 zilizopita
- Kuvunjika kwa sitisho la mapigano ni 'mwiba' kwa watoto
- Watoto 100 wanauawa au wanajeruhiwa kila siku Gaza
- Chonde chonde rejesheni sitisho la mapigano
Kuvunjika kwa makubaliano ya sitisho la mapigano huko Gaza kati ya wanamgambo wa Hamas na Israeli, na kuanza tena kwa mapigano makali kumesababisha vifo vya watoto 322 huku wengine 609 wakiwa wamejeruhiwa katika siku kumi zilizopita.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa NewYork, Marekani na Amman, Jordan, Jumatatu usiku, ikisema hali inazidi pia kuwa mbaya kutokana na kuanza tena kwa operesheni za mashambulizi ya ardhini kwenye Ukanda a Gaza.
“Hii inamaanisha kuwa kwa wastani kila siku watoto 100 wanauawa au wanajeruhiwa,” imesema taarifa hiyo ikiongeza kuwa idadi kubwa ya watoto hao walikuwa wameshafurushwa makwao, wanaishi kwenye makazi ya mud ana nyumba zao zimeharibiwa.
Idadi hiyo ya watoto inajumuisha watoto ambao wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa wakati hospitali ya upasuaji ya Al Nasser iliyoko kusini mwa Gaza iliposhambuliwa tarehe 23 mwezi Machi.
Mashambulizi yanafanywa kiholela
Wiki tatu za mashambulizi yaliyoibuka upya, mashambulizi yasiyoyachagua eneo iwapo ni la raia au la, na kuzuiwa kwa kabisa uingizaji na usambazaji wa misaada kumeongeza shinikizo kwenye majawabu ya changamoto za kibinadamu kwa raia wa Gaza, hususan watoto milioni moja.
“Sitisho la mapigano Gaza kulitoa fursa ya kufikisha msaada wa dharura kwa watoto wa Gaza na matumaini ya njia ya kupona,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell kupitia taarifa hiyo.
“Lakini watoto tena wameingizwa katika mzunguko wa vurugu na kukosa mahitaji. Pande zote lazima zifuate majukumu yao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu ili kuwalinda watoto,” amesema Mkuu huyo wa UNICEF.
Baada ya takribani miezi 18 ya vita, zaidi ya watoto 15,000 wameripotiwa kuuawa, zaidi ya 34,000 wameripotiwa kujeruhiwa, na karibu watoto milioni moja mara kwa mara wamelazimika kuhama na kunyimwa haki yao ya huduma za kimsingi.
Misaada haijaingia Gaza tangu tarehe 2 Machi
Kwa kuwa hakuna msaada unaoruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza tangu tarehe 2 mwezi uliopita wa Machi – ikiwa ni kipindi kirefu zaidi cha kuzuiwa msaada tangu kuanza kwa vita Oktoba 7 2023, – chakula, maji salama, makazi, na huduma za matibabu vimekuwa haba.
UNICEF inasema bila huduma hizi muhimu, utapiamlo, magonjwa na hali nyingine zinazoweza kuzuiliwa huenda zikazidi, na kusababisha kuongezeka kwa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika.
Mashirika ya kibinadamu yanafanya kazi bila kuchoka ili kulinda na kusaidia watoto katika hali hizi za kutisha lakini bado wanakutana na mashambulizi ambayo yameua na kujeruhi maelfu ya wafanyakazi wa msaada.
“Mashambulizi haya ni kinyume na sheria ya kimataifa ya kibinadamu na yanahatarisha kuendelea kwa operesheni muhimu za kuokoa maisha kwa wale wanaohitaji msaada wa dharura.” Imesema UNICEF.
Chonde chonde rejesheni sitisho la mapigano
Hata hivyo licha ya hatari zinazoendelea, UNICEF imejizatiti kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu ambao watoto na familia zao wanategemea kwa ajili ya uhai na ulinzi.
UNICEF inaendelea kutoa wito kwa pande zote kuacha mapigano na kurudisha tena mkataba wa kusitisha mapigano.
Tarehe 17 mwezi Januari, 2025, Israeli na Hamas walifikia makubaliano ya sitisho la mapigano kwa siku 42 ili kuwezesha kuachiliwa huru kwa mateka wa Israeli wanaoshikiliwa na Hamas na pia wafungwa wa kipalestina wanaoshikiliwa na Israeli.
“Msaada wa kibinadamu na bidhaa za kibiashara lazima ziruhusiwe kuingia na kusafirishwa kupitia Ukanda wa Gaza. Watoto wagonjwa na majeruhi lazima wahamishwe kwa ajili ya matibabu. Raia, wakiwemo watoto na wafanyakazi wa kibinadamu, na miundombinu muhimu iliyosalia lazima ilindwe, na mateka lazima waachiliwe.”
UNICEF pia inasisitiza kwa mataifa yenye ushawishi kutumia nguvu zao kuzuia mgogoro na kuhakikisha kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kwamba watoto walindwe. “Dunia haipaswi kusimama tu na kuacha mauaji na mateso ya watoto kuendelea,” imetamatisha taarifa hiyo.