UDADAVUZI: Fahamu njia 5 za kupunguza taka katika sekta ya mitindo ya mavazi
UDADAVUZI: Fahamu njia 5 za kupunguza taka katika sekta ya mitindo ya mavazi
- Kuunda sekta ya mitindo ya mavazi yenye mzunguko endelevu
- Kuboresha urejeleaji wa vitambaa na nguo
- Kuondoa kemikali hatari kwenye nguo
- Kubadili mtazamo wa kuamini nguo mpya ni bora
- Kununua nguo chache lakini zenye ubora
Tarehe 30 Machi, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutozalisha Taka ambayo mwaka huu inaangazia mitindo ya mavazi na nguo. Kuelekea siku hiyo, shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP, ambalo ndilo linaongoza kwenye maadhimisho haya, limechapisha kwenye wavuti wake njia tano za kufanya sekta ya mitindo na mavazi iwe endelevu kimazingira.
Mambo hayo matano yamekekwa bayana na Elisa Tonda ambaye ni Mkuu wa Idara ya Rasilimali na Masoko UNEP
1. Kuunda sekta ya mitindo ya mavazi yenye mzunguko endelevu
“Mfumo wa biashara mfululizo (LINEAR) wa sekta ya mitindo ya mavazi ndio chanzo kikuu cha taka zinazozalishwa,” anasema Tonda. Idadi kubwa ya nguo zinatengenezwa kwa haraka na kwa gharama ya chini, bila kuzingatia athari zake kwa mazingira. Nguo hizi zinavaliwa kwa muda mfupi kisha kutupwa kwenye dampo au kuchomwa. Hii inachangia mabadiliko ya tabianchi, inapunguza rasilimali asili na kuchafua ardhi, bahari na hewa kwa kemikali hatari.
Jawabu:
Tonda anasema sekta hiyo inahitaji kupunguza uzalishaji wa bidhaa mpya na kuwa endelevu zaidi kwa kuhakikisha nguo na malighafi zinatumika kwa muda mrefu zaidi. Ili kufanikisha hili, watengenezaji wa nguo wanaweza kubuni mavazi yanayodumu, kutumia vitambaa endelevu zaidi na kurahisisha mchakato wa urejeleaji wa nguo.
“Kadri sekta ya mitindo na watumiaji wanavyokumbatia mifumo ya biashara inayozingatia mzunguko endelevu na kuachana na mitindo ya haraka, itakuwa muhimu kusaidia nchi zinazozalisha nguo ili zisiachwe nyuma katika mpito huo,” anaongeza Tonda.
2. Kuboresha urejeleaji wa vitambaa na nguo
Ni asilimia 1 pekee ya nyuzi zinazotumika kwa mavazi mapya, nguo na vitambaa vya samani, na viatu zinatokana na nguo zilizochakatwa, kulingana na Shirika la Lisilo la Serikali la Mabadilishano ya Mavazi au Textile Exchange
Ili kuongeza Urejeleaji, Tonda anasema manispaa zinanaweza kuwekeza katika miundombinu ya kukusanya taka za nguo, kama vile benki za nguo zinazoruhusu watu kuweka mavazi yao ya zamani.
Pia, wanaweza kupanua programu za urejeleaji wa nguo. Wakati huo huo, serikali za kitaifa zinaweza kutekeleza mipango ya uwajibikaji wa wazalishaji ambayo inawafanya wazalishaji wawajibike kwa nguo zinapomaliza muda wake, badala ya kuziachia manispaa na watumiaji. Nchi nyingi tayari zimeanza kufanya hivyo.
Aidha, kampuni za mavazi zinaweza kubuni mavazi rahisi kwa ajili ya urejeleaji, ikiwa ni pamoja na kuchagua vitambaa vinavyoweza kutumika tena kwa urahisi na kuondoa kemikali hatari.
3. Kuondoa kemikali hatari kwenye nguo
Zaidi ya kemikali 15,000 zinatumika katika utengenezaji wa nguo, kulingana na makala ya jarida la Springer Nature. Baadhi ya kemikali kama zile zinazoongezwa ili kufanya nguo zisishike moto au zisichafuke, ni hatari na zinaweza kubaki kwenye mazingira kwa miongo kadhaa, zikiathiri binadamu, wanyama na mazingira. Kemikali hizi pia huingiliana kwa njia tata na kufanya iwe vigumu kuchakata nguo kwa usalama.
Ndiyo maana Tonda anasema “ni muhimu kwa serikali kudhibiti na kusimamia matumizi salama ya kemikali hatari zinazotumika katika uzalishaji wa nguo. Wakati huo huo, makampuni ya mavazi yanaweza kuhakikisha bidhaa zao zimetengenezwa kwa kemikali rafiki kwa mazingira, wakikumbatia kile wataalamu wanakiita “kemia endelevu na salama.”
Nguo za nailoni zinapofuliwa au kuvaliwa, hutoa nyuzi ndogo za plastiki (microfibres), baadhi zikiwa na kemikali hatari, kulingana na utafiti wa jarida la (Microplastics). Hii ni sababu nyingine kwa nini Tonda anasema ni muhimu makampuni kuondoa kemikali hatari kwenye bidhaa zao. Watengenezaji wa nguo, wazalishaji wa mashine za kufua nguo, na mitambo ya kusafisha maji machafu ya manispaa wanahitaji kukusanya takwimu zaidi kuhusu utoaji wa nyuzi ndogo na vichungi vya kuondoa nyuzi hizo, huku makampuni yakitoa taarifa kwa watumiaji kuhusu jinsi ya kuhifadhi na kutunza mavazi yao ipasavyo.
4. Kubadili mtazamo wa kuamini nguo mpya ni bora
Wakosoaji wanasema sekta ya mitindo, ikichochewa na injini yenye nguvu ya masoko, kwa muda mrefu imewahimiza watumiaji kununua mavazi zaidi ya wanavyohitaji.
Uzalishaji wa mavazi uliongezeka maradufu kutoka mwaka 2000 hadi 2015, huku idadi ya mara nguo zilipovaliwa ikipungua kwa asilimia 36, kulingana na Ellen MacArthur Foundation.
Ripoti ya hivi karibuni ya UNEP na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Hali ya Hewa imewataka wahusika wa sekta ya mitindo ya nguo wakiwemo wauzaji wa bidhaa, wahariri wa majarida na wanahabari wa mitandao ya kijamii kukabiliana na mtazamo huu wa “mpya ni bora.” Ripoti hiyo imesema wanaweza kufanya hivyo kwa kukuza mitindo endelevu ya maisha, kuwahimiza wazalishaji wa mavazi kupunguza uzalishaji, na kuondoa ujumbe unaohimiza ununuzi kupita kiasi.
“Kampuni zinaweza kuunda ujumbe kwa masoko na bidhaa zenye maisha marefu ya kihisia ambapo wateja wanahamasishwa kuvaa na kutunza mavazi kwa muda mrefu. Kila mtu anaweza kuwahimiza watu waliomzunguka kuthamini na kuwa wabunifu na mavazi waliyonayo badala ya kununua zaidi.” anasema Tonda.
Ili kusaidia hili, serikali zinaweza kufanya kampuni kufichua athari za mazingira za mavazi wanayotengeneza, hatua ambayo ingesaidia watumiaji kufanya maamuzi yaliyo bora na endelevu zaidi.
5. Kununua nguo chache lakini zenye ubora
Ingawa mzigo mkubwa wa kufanya sekta ya mitindo iwe endelevu zaidi unatakiwa kuwa kwa serikali na wafanyabiashara, Tonda anasema watumiaji wana jukumu muhimu. Anawahimiza “kununua ndani ya makabati yao wenyewe” na kuunga mkono mifumo ya biashara endelevu. Hii inamaanisha, kwa mfano, kurekebisha au kuremba nguo zilizopo, kukodi mavazi kwa hafla maalum, kununua mavazi ya zamani kwenye maduka ya mtandaoni, na kubadilishana nguo na marafiki.
Iwapo kununua kipya ni chaguo pekee, Tonda anapendekeza kuchagua chapa endelevu na vitambaa vya kutengeneza nguo vya ubora wa juu vinavyoweza kudumu kwa muda mrefu.
“Watumiaji wana nguvu kubwa, na kwa kuchukua chaguzi endelevu zaidi, wanaweza kutuma ujumbe kwa wale walio na ushawishi na uwezo wa kufanya sekta ya mitindo kuwa endelevu zaidi,” anasema Tonda.