UNHCR na WFP waweka bayana kupungua kwa ufadhili kunavyokwamisha operesheni za usaidizi
UNHCR na WFP waweka bayana kupungua kwa ufadhili kunavyokwamisha operesheni za usaidizi
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la Mpango wa Chakula duniani, WFP yamesema ukata utasababisha madhara makubwa kwenye huduma za usaidizi wa kibinadamu katika maeneo mbalimbali duniani, wakati huu ambapo wahisani wanapunguza ufadhili.
Mathalani Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Umma, UNHCR, Dkt. Allen Maina amewaambia waandishi wa habari hii leo jijini Geneva, Uswisi kuwa “bila rasilimali za kutosha, takribani wakimbizi milioni 12.8, wakiwemo watoto milioni 6.3 wanaweza kukosa huduma za afya za kuokoa maisha yao mwaka huu wa 2025.”
Kwa WFP nako hali si hali kwani kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Roma, Italia shirika hilo linaonya kwamba watu milioni 58 katika maeneo 28 yenye majanga duniani wako hatarini kukosa misaada ya kuokoa maisha iwapo fedha hazitapatikana.
Dkt. Maina wa UNHCR amesema janga la ufadhili kwenye huduma za kiutu linalochochewa na kupunguzwa kwa nchi wenyeji kuwekeza kwenye sekta ya afya kunaathiri mawanda ya ubora wa afya ya umma, mipango ya lishe kwa wakimbizi na wenyeji.
Nchi wenyeji zikipunguza huduma, wakimbizi nao wanadhurika
“Usaidizi kwenye afya kwa wakimbizi unapopunguzwa, wakimbizi watalazimika kujilipia kwa fedha ambazo hawana ,na watashindwa kupata huduma zinazotolewa na serikali za nchi zinazowahifadhi ambako vituo vya afya navyo vimezidiwa uwezo,” amesema Dkt. Maina.
Ametoa mfano wa madhara ya kukatwa kwa ufadhili wa fedha kwenye maeneo tofauti duniani.
Nchini Bangladesh, takribani wakimbizi milioni 1 wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar wanakabiliwa na anga la fya kutokana na kusitishwa kwa ufadhili. Wajawazito zaidi ya 40,000 wanaweza kukosa huduma za msingi za kabla ya kujifungua.
Huko Burundi, kusitishwa kwa programku za lishe kwenye kambi kadhaa za wakimbizi kunamaanisha maelfu ya wakimbizi wakiwemo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano watakosa huduma za tiba dhidi ya utapiamlo.
Na kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mfumo wa afya uko hatarini kusambaratika. Bajeti ya afya ya mwaka 2025 imekatwa kwa asilimia 87 ikilinganishwa na mwaka 2024.Madhara yake yanaweka hatarini maisha ya wakimbizi wa ndani zaidi ya 520,000 ambao wanaweza kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza.
“Kila uchao ambapo ukosefu huu wa uhakika wa fedha unazidi kuripotiwa, kunaongeza madhara kwenye maisha ya mamilioni ya wanaume, wanawake na watoto duniani kote ambao wamekimbia makwao kusaka usalama,” amesema Afisa huyo wa UNHCR.
Ukata kulazimu WFP kupunguza mgao katika programu 28
WFP inasema licha ya ukarimu wa baadhi ya serikali na wahisani binafsi, bado kuna pengo kubwa litokanalo na kupungua kwa ufadhili. “Kupungua kwa ufadhili pamoja na ongezeko kubwa la watu wenye uhitaji vimesababisha ongezeko kubwa la makumi ya mamilioni ya watu duniani wanaohitaij misaada.”
Ufadhili umepungua kwa asilimia 40 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana. Hii ina madhara makubwa kwenye mgao wa chakula cha msaada duniani kote hasa kwenye maeneo ya watu walio hatarini zaidi.
Maeneo ambayo program za WFP zinakabiliwa na madhara ya ukata
Katika maeneo haya usaidizi au mgao wa chakula utakumbwa na changamoto hadi mwezi Agosti. Lebanon, Sudan, Syria, Sudan Kusini, Chad, Afghanistan, Myanmar, Uganda, Niger, Burkina Faso, DRC, Yemen, Mali, Bangladesh, Venezuela, Haiti, Msumbiji, Nigeria, Somalia, Kenya, Ukraine, Malawi, Burundi, Ethiopia, Palestina, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jordan na Misri.
“Kwa sasa WFP inapatia kipaumbele nchi zenye mahitaji makubwa na zinazokabiliwa na mizozo. Pamoja na kujitahidi kupunguza gharama za uendeshaji, tambua kuwa tunakabiliwa na ukata mkubwa unaotishia uhai wa watu,” amesema Rania Dagash-Kamara, Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa WFP akihusika na Ubia na Ubunifu.