CSW69: Maendeleo ya kidijitali yamfikie pia mkulima mwanamke
- Maendeleo ya kidijitali yatamkomboa mwanamke mkulima
- Mapambano ya usawa wa kijinsia yaendelee kwani si rahisi
- Maazimio ya kisiasa yageuzwe kuwa mikataba ya kimataifa
Wanawake wakulima wanahitaji kupatiwa mbinu za kidijitali ili waweze kujikwamua kiuchumi wakati huu ambapo maendeleo ya kidijitali yanasonga kwa kasi, amesema Julie Cissé, mwanamke mwanaharakati wa haki ardhi kwa wanawake nchini Senegal.
Alikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani, CSw69 uliomalizika jijini New York, Marekani tarehe 21 Machi 2025.
Yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Kiraia la Maendeleo ya Kijamii GIPS nchini Sénégal, na pia ni mwanachama wa Shirika liitwalo Women To Kilimanjaro linalosaka haki ya ardhi kwa wanawake barani Afrika.
Akiwa amevalia kofia ya kitamaduni, inayotumiwa na wakulima wanawake Senegal, Bi, Cissé anasema walifika New York kuendeleza mafanikio ya Azimio la Beijing lililopitishwa miaka 30 iliyopita wakati wa mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake nchini China, ambalo linachagiza usawa wa kijinsia.
Nafasi ya mwanamke mkulima katika kulinda tabianchi
Anakiri licha ya mafanikio kuna changamoto mpya hasa mbili zinazohusiana na kilimo. Mosi ni dunia ya kidijitali, kutambua na kuendeleza, na vile vile kutambua mchango wa wanawake katika uhakika wa kupatikana kwa chakula. Na zaidi ya yote changamoto nyingine ni tabianchi. Umuhimu wa kutambua uongozi wa wanawake katika kubaliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo tuna mambo mengi sana ya kufanya hapa New York.”
Kuhusu haki za wanawake Bi. Cissé amesema katika CSW69 “tumepaza zaidi sauti ili kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa sababu kuna vitendo kama hivyo wanafanyiwa wanawake na wasichana. Lakini eneo lingine la uchechemuzi ni hatimaye uwezeshaji halisi wa kiuchumi kwa wanawake wote hasa wanawake wakulima.”
Pamoja na kukiri kuwa CSW69 imempatia fursa ya kupaza zaidi sauti za wanawake kwa kuwa ni jukwaa la kimataifa ametoa shukrani kwa vyombo vya habari akisema, “jambo la pili ni kukutana na watu kama nyie. Tunashukuru vyombo vya habari kwa kueneza ujumbe wetu.”
Bila wakulima wanawake hakuna uhakika wa chakula
Amesema jambo lingine ambalo wataendelea kupazia sauti ni jamii ya kimataifa kutambua nafasi ya wanawake wakulima katika upatikanaji wa chakula akisema, “bila wakulima wanawake hakuna chakula. Kwa hiyo kwa kuzingatia hayo, tuna imani.”
Kwa Bi. Cissé hatma ni kuona “Umoja wa Mataifa unatambua kuwa wakulima wanawake wanataka kusikilizwa zaidi, haki zao zipatikane na washiriki zaidi kwenye usimamizi wa rasilimali. Ukiwa na ardhi, kuna rasilimali za kilimo, na rasilimali fedha zinazohusiana na kilimo.”
Maazimio ya kisiasa yageuzwe kuwa mikataba - Wajiri
Mshiriki mwingine ni Melvin Wajiri kutoka nchini Burkina Faso. Huyu ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali au NGO liitwalo “People Helping People” ikimaanisha watu wanaosaidia watu na linafanya kazi katika nchi 42 barani Afrika ikiwawezesha vijana kufanya maamuzi bora kwa ajili ya mustakbali wao.
Ametanabaisha kuwa “jinsia ni muundo wa jamii unaojumuisha wanawake, wanaume, watoto watu wazima au muundo na mgawanyo wa aina yoyote ile uliowekwa na jamii lakini unamaanisha kuishi kwa pamoja kwa amani, ni kuhusu jamii , ina mawanda mapana lakini wakati mwingine inajikita katika kundi fulani la watu kama wanawake na ndio maana tumekuwa na CSW ambapo tunakuja kujadili masuala yanayowahusu wanawake baada ya azimio la Beijing miaka 30 iliyopita.”
Mapambano yaendelee kwani si kazi rahisi
Amesema ujumbe wake ni kwamba wanawake waendelee na mapambano kwani si kazi rahisi kupigania usawa wa kijinsia ingawa kwa miaka 30 hatua zimepigwa. Tunapaswa kuangalia ujumbe ni nini?”
Halikadhalika kuhakikisha ujumbe huo unageuzwa kuwa hatua, na hilo litawezekana tu endapo maazimio ya kisiasa yanabadilishwa na kuwa mikataba. Na pia kuna wanaume na watoto wavulana ambao kesho watakuwa wanaume, tunahitaji kutafuta fursa kwa wao kushiriki.
Sasa ni wakati wa kujitambua – Bi. Juma
Kutoka Tanzania Zanzibar ni Jamila M. Juma, Mkurugenzi kwenye jumuia ya wanasheria ya wanawake Zanzibar. Yeye anasema, “kwa muda mrefu, wanawake wamekuwa wakichukuliwa kama raia wa daraja la pili. Huu sasa ni wakati wa kujitambua, kusimama imara, na kudai haki zetu kwa pamoja. Kama wanawake, hatupaswi tu kudai haki zetu, bali pia kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu ipasavyo.”
Amesisitiza kuwa wale wanaoshikilia haki za wanawake wanapaswa kuziachia nafasi hizi ili wanawake waweze kusukuma gurudumu la maendeleo mbele kwa ujasiri na ari mpya.
Sheria nyingi hazizingatii usawa wa kijinsia
Na kuhusu changamoto wanasheria wanazipitia katika utekelezaji wa sheria za haki za wanawake, amesema “changamoto bado ni nyingi kwani sheria zetu nyingi hazizingatii usawa wa kijinsia. Bado kuna mtazamo unaowapa wenye madaraka nafasi ya kuendelea kushikilia mamlaka, ambapo kwa muda mrefu nafasi hizo zimekuwa zikishikiliwa na wanaume.”
Amesema alichojifunza ni kwamba kuna mikakati mbalimbali inayotekelezwa na mataifa mengine ili kumkomboa mwanamke na mtoto wa kike, kuhakikisha wanapata haki zao na kushiriki kikamilifu katika masuala ya uongozi na maendeleo. “Tunapoondoka hapa, tutahakikisha kuwa yale mazuri tuliyojifunza tunayatekeleza kisheria na kuyasimamia katika jamii zetu nyumbani.”