Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu UN ana wasiwasi kuhusu hali ya Sudan Kusini

Mfanyakazi wa Afya wa Bomi anayeungwa mkono na UNICEF Awan Agaan anashauriana na wakazi wa eneo hilo, akiwemo Deborah Yar na binti yake, katika kijiji kimoja huko Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftali Wanajamii wakikutana na muhudumu wa afya anayesaidiwa na UN katika maeneo ya vijijini nchini Sudan Kusini, ambako upatikanaji wa huduma za afya bado ni changamoto kubwa.

Katibu Mkuu UN ana wasiwasi kuhusu hali ya Sudan Kusini

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali ya kutisha nchini Sudan Kusini, Msemaji wake amewaambia waandishi wa habari leo Machi 27.

Stéphane Dujarric, akiwaeleza waandishi wa habari leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini, New York, Marekani kuhusu hali ya usalama inavyoendelea kuzorota na pia kuwekwa katika kifungo cha nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini (UNMISS) umetoa wito kwa pande zote kuwa na uvumilivu na kuheshimu Makubaliano ya Amani yaliyoboreshwa.
 
"Tunatahadharisha kuwa hatua hii inasogeza nchi hatua moja zaidi karibu na kuanguka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuvuruga makubaliano ya amani," Dujarric amesema.
 

Wito

 
Aidha msemaji huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Maraifa ameeleza kwamba Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Machar kutatua tofauti zao kwa mazungumzo na kumaliza mapigano ya kijeshi yanayotishia mchakato wa amani.
 
Dujjaric amesema UNMISS inasisitiza wito wake kwa Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais kutatua malalamiko, kumaliza makabiliano ya kijeshi, kuheshimu Makubaliano ya Amani na kupeleka nchi mbele kwa pamoja kuelekea mustakabali wa amani na demokrasia ambao wananchi wao wanastahili.
 
“Kwa kuwa tumekuwa tukionesha kila siku hali ngumu na mateso ya watu wa Sudan Kusini, inapaswa kuwa wazi kwa wote kwamba watu wa Sudan Kusini hawawezi kuvumilia athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe.”  Amesema Dujjaric.
 
Hali ya kibinadamu nchini humo inaendelea kuwa mbaya, huku watu milioni 9.3 wakihitaji msaada wa dharura kutokana na athari za vita, mabadiliko ya tabianchi, na janga la kiuchumi. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa nchi hiyo haiwezi kustahimili vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe, kwani mamilioni ya watu tayari wanahangaika kuendelea kuishi.
 
Taarifa rasmi kutoka kwa ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili inatarajiwa kutolewa baadaye leo.
 
Sudan Kusini, iliyopata uhuru wake mwaka 2011, imekumbwa na misukosuko ya kisiasa na vita kwa muda mrefu. Makualiano ya Amani yaliyoboreshwa mwaka 2018 yalileta utulivu wa muda mfupi kati ya makundi yanayohasimiana, lakini hali ya sasa inaonekana kuhatarisha maendeleo yaliyopatikana.