Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya kwanza idadi ya wakimbizi wa ndani Sudan yapungua

Wavulana wawili wadogo wamekaa kwenye sakafu ya vigae huko Sudan, mmoja akila chakula.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdeen Watoto wawili waliofurushwa na mapigano katika jimbo la Al Jazirah wamepumzika katika eneo la mapokezi kusini mashariki mwa Sudan.

Kwa mara ya kwanza idadi ya wakimbizi wa ndani Sudan yapungua

Wahamiaji na Wakimbizi

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo Machi 27 na shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM huko Port Sudan nchini Sudan na Geneva, Uswisi, idadi ya wakimbizi wa ndani (IDPs) nchini Sudan imepungua kwa asilimia 2.4 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, ikiwa ni upungufu wa kwanza tangu kuanza kwa janga hilo karibu miaka miwili iliyopita.

Upunguaji huu unatokana hasa na watu kurudi katika maeneo yao ya asili. Hata hivyo, maeneo wanayorejea yana uharibifu mkubwa na wanakosa huduma muhimu, kama vile makazi bora, chakula, miundombinu, na elimu, imeeleza IOM.

Harakati ya kurudi nyumbani

Tangu Desemba 2024, jumla ya watu 396,738 wamerudi nyumbani katika majimbo ya Aj Jazirah, Sennar, na Khartoum. Harakati hii inaonesha mabadiliko ya taratibu lakini yenye matumaini kwani jamii zinazohama zinajaribu kurejesha maisha yao ya kawaida baada ya miezi mingi ya vita vikali. Hata hivyo, hali ya usalama imezorota katika majimbo ya North Darfur na White Nile, ambapo idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka, na hitaji la msaada wa kibinadamu linabaki kuwa kubwa sana kote Sudan.

Mohamed Refaat, Mkuu wa IOM Sudan, amesema,“wakati watu wengi wanatamani kurejea nyumbani, bado masharti ya kurejea kwa usalama na kuunganishwa kwa kudumu hayajafikiwa. Huduma za msingi ikiwa ni pamoja na afya, ulinzi, elimu, na chakula ni adimu, na ukosefu wa miundombinu inayofanya kazi na uwezo wa kifedha utafanya iwe vigumu kwa familia kujenga upya maisha yao.”

Taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uhamaji wa IOM (DTM) inaonesha kwamba Sudan inahifadhi takriban wakimbizi wa ndani 11,301,340, ikiwa ni pamoja na wale waliokimbia kabla na baada ya kuanza kwa mgogoro. Wakimbizi wengi wa ndani walikimbia Khartoum, Darfur Kusini na Kaskazini. Karibu milioni nne za watu wamevuka mpaka kwenda nchi jirani, ambapo wengi wamekimbilia Misri, Sudan Kusini, na Chad.

Zaidi ya nusu ya waliofurushwa ni watoto

Ripoti inaonesha kuwa wengi wa wakimbizi wa ndani wanakaa katika hali ngumu za kibinadamu, wakiwa na upatikanaji mdogo wa huduma za kimsingi. Zaidi ya nusu ya waliofurushwa ni watoto, na asilimia 27 ni chini ya umri wa miaka mitano. Wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 ni takriban asilimia 28 ya idadi ya wakimbizi wa ndani.

Refaat amesisitiza madhara makubwa yaliyosababishwa na mgogoro, akisema, “miaka miwili ya vita isiyokoma nchini Sudan imesababisha mateso makubwa, na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, ambapo watu zaidi ya milioni 30.4, zaidi ya nusu ya idadi ya watu wanahitaji msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 16. Kupunguzwa kwa bajeti za msaada wa kibinadamu wa kimataifa kumezidisha mgogoro na kuongeza mateso.”

Upungufu wa ufadhili unahatarisha urejesho salama na ustawi wa waathiriwa

Mpango wa Misaada wa IOM Sudan unalenga kukusanya dola milioni 250 kusaidia watu milioni 1.7 wanaohitaji msaada. Hata hivyo, hadi Februari 2025, mpango huo haujafikiwa vya kutosha, ambapo ni asilimia 6 tu ya fedha zinazohitajika zimepatikana.

Tangu kuanza kwa mgogoro, IOM imekuwa ikitekeleza shughuli za dharura, ikitoa msaada wa maisha kwa watu wa Sudan na nchi jirani.Msaada wa kibinadamu ni muhimu kuhakikisha urejesho salama na kutoa misaada ya haraka, kama chakula, makazi, huduma za afya, na ulinzi. Upatikanaji wa huduma hizi za kimsingi utaweza kusaidia watu waliothiriwa kupona na kujenga maisha yao upya.