DRC: Kinachotakiwa ni sitisho la mapigano bila masharti yoyote
DRC: Kinachotakiwa ni sitisho la mapigano bila masharti yoyote
- Sitisho la mapigano ni muarobaini
- Balozi Ngay asema hakuna askari wa Rwanda aliyeondoka DRC
- Waziri Nduhungirehe asema mikakati ya Rwanda kujilinda kwa sasa itasalia pale pale
Mapigano yakizidi kushamiri huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC tangu mwezi Januari mwaka huu, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Bintou Keita ameliambia Baraza la Usalama kuwa juhudi zote zielekezwe kwenye sitisho la mapigano lisilo na masharti yoyote.
Bintou Keita akihutubia ikiwa ni moja ya vikao vinavyofanyika kila baada ya miezi mitatu kueleza Baraza juu ya hali ya amani na usalama DRC, amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulindaa amani nchini humo ambao yeye pia anauongoza, “umejizatiti kusaidia harakati za kikanda za kuleta amani kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu.
"MONUSCO iko tayari kutumia uwezo wake wote kutekeleza sitisho la mapigano linaloweza kupatikana,” amesema hayo kwenye mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe.
Msuluhishi wa AU ateuliwe mapema kuratibu michakato ya amani ya kikanda
Ameweka bayana hata hivyo kwamba “licha ya juhudi muhimu za kikanda na kimataifa, sitisho la mapigano lisilo na masharti yoyote lililoitishwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, Muungano wa Afrika, AU na Baraza la Usalama kupitia azimio namba 2773, na vile vile hivi karibuni huko Qatar, hadi sasa hakuna kilichopatikana.
"Ni vema pande zote kuheshimu ahadi zao za kunyamazisha silaha na kusaka Suluhu kwa njia ya amani,” amesema hayo huku akishukuru harakati za Rais wa Angola ambaye ni Mwenyekiti wa AU, João Lourenço, "kwa kusaka bila kuchoka harakati za kurejesha mazungumzo kati ya DRC na Rwanda.”
Amesihi kuteuliwa haraka kwa Msuluhishi wa AU atakayeteuliwa na viongozi wa EAC na SADC, kwa lengo la kuunganisha michakato ya amani kwa kutumia msingi wa michakato ya Luanda na Nairobi.
Guterres kuandikia barua Baraza la Usalama kuhusu uondokaji wa MONUSCO
MONUSCO inatekeleza wajibu wake kule ambako M23 inashikilia
Madhara ya Marekani kuondoa ufadhili
Hakuna askari wa Rwanda aliyeondoka DRC – Balozi Ngay
Zénon Mukongo Ngay, Mwakilishi wa Kudumu wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa, alipatiwa fursa ya kuhutubia wajumbe wa Baraza ambapo amesema “utekelezaji wa azimio namba 2773 la mwaka 2025 unasalia kuwa kipaumbele.”
Amesema “hadi leo hii, hakuna askari wa Rwanda ameondoka kutoka ardhi ya DRC, hakuna wapiganaji wa M23/AFC walioondoka kutoka Goma au Bukavu, au eneo lolote linalodhibitiwa na waasi hao na hakuna utawala wowote sambamba na ule wa serikali ambao umevunjwa,” akizungumzia waasi wa M23 ambao wameunda utawala wao kwenye mji wa Goma na kuteua Gavana wao, hali iliyosababisha DRC kuhamishia makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini kwenda mji wa Beni.
Mikakati yetu ya kujilinda itasalia palepale kwa sasa – Waziri Nduhungirehe
Kwa upande wake, Bwana Nduhungirehe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda ameeleza Baraza kuwa, “kilicho dhahiri kwetu Rwanda ni kwamba mikakati ya kujilinda ambayo tumeiweka itaendelea kusalia, hadi pale kuna mfumo wa uhakika wa muda mrefu wenye hakikisho la usalama, kwenye mpaka wetu na DRC.”
Kisha Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Rwanda alizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Baraza na kusema kuwa “ni juu ya ukanda wetu na Afrika kutuongoza kwenye mchakato wa kutusongesha mbele.”