MONUSCO: Mashambulizi yakiendelea Ituri, waasi wa Zaire wajisalimisha
MONUSCO: Mashambulizi yakiendelea Ituri, waasi wa Zaire wajisalimisha
Stéphane Dujarric, ambaye ni Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema licha ya kumekuweko kwa ongezeko la mashambulizi kutoka kwa makundi yaliyojihami dhidi ya raia huko jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, wameweza kufanikisha mazungumzo yaliyowezesha baadhi ya makundi kujisalimisha.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani, Bwana Dujarric amesema ongezeko hilo la mashambulizi ni kwenye maeneo karibu na makazi ya wakimbizi pamoja na maeneo yenye madini huko Djugu na Mahagi.
Ingawa hivyo mazungumzo kati ya serikali na makundi ya waasi kama vile CODECO na Zaire, mazungumzo yaliyoratibiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa na kuongozwa na serikali yamefanikisha kujisalimisha kwa wafuasi 171 wa kundi la Zaire na hivyo kuwa hatua muhimu kuelekea upunguzaji wa ghasia kwenye jimbo hilo la Ituri.
“Walinda amani wanaendelea kuimarisha uwepo wao kwenye maeneo hatari kwa kufanya doria za mara kwa mara kwenye maeneo yenye jukumu la kusambaza huduma na pia kuwapatia ulinzi wa moja kwa moja raia 100,000 ambao ni wakimbizi,” amesema Dujarric.
Doria za pamoja za MONUSCO na FARDC
Mathalan tarehe 24 mwezi huu wa Machi, walinda amani waliweza kusambaratisha shambulio lililofanywa na waasi wa CODECO kwenye makazi ya wakimbizi ya Lodha, nah atua hiyo ilifanikishwa kutokana na ushirikiano na jeshi la serikali, FARDC.
Halikadhalika, miezi miwili ya mwanzoni mwa mwaka huu, vikosi vya polisi huko Bunia, amba oni mji mkuu wa jimbo la Ituri, vilifanya doria 310 kusaidia ulinzi wa raia kambini.
“Kwa sasa Umoja wa Mataifa unasalia umejizatiti kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia wakati huu ambapo mapigano yanaendelea, sambamba na watu kufurushwa makwao,” amesema Dujarric.
Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, waasi wa M23 walitwaa mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini na sasa wameshateka miji mingine katika jimbo la Kivu Kusini ikiwemo Kamanyola.