Tafakari ya Gertrude Mongella miaka 30 baada ya Mkutano wa Beijing (1995)
Tafakari ya Gertrude Mongella miaka 30 baada ya Mkutano wa Beijing (1995)
Ni miaka thelathini tangu Mkutano wa Beijing ulipofanyika jijini Beijing, China na kupitisha lililofahamika kama Azimio la Beijing lengo kuu likiwa kuleta usawa wa kijinsia kwa kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali baada ya kundi hilo kuwa limekandamizwa kwa miaka mingi kote duniani.
Kwa wiki mbili mfululizo hadi Ijumaa wiki iliyopita, ulimwengu umekutana hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani katika Mkutano wa 69 wa Hali ya Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69 ili kujadili ni kwa kiasi gani Azimio la Beijing limefikiwa.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huu ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano huo wa Beijing, Balozi Gertrude Mongella. Anold Kayanda wa Idhaa hii amepata fursa ya kuzungumza naye.
Ni ujumbe gani Gertrude Mongella anauacha kwa msichana au mwanamke wa miaka 30 ijayo?
Balozi Mongella analijibu swali hili kwa namna tofauti kabisa – anasema, “ujumbe ninaouacha sio kwa mtoto wa kike tu, mimi nawaachia wote, mtoto wa kike na mtoto wa kiume. Kwasababu taabu iliyotupata huko nyuma ni kutokana na kutenganisha binadamu mwanaume, binadamu mwanamke ndio imetupa matatizo wanaume wakaanza kuwanyanyasa wanawake hata mahali ambako hawapasi kunyanyasika.”
Ujumbe
“Kwa hiyo mimi ujumbe nilionao ni kubadilisha mtazamo wa binadamu, wanaume kwa wanawake. Kwa hiyo sasa ndio mwanzo mzuri watoto wa kiume na wa kike wote wajifunze haki za binadamu na wazione kwamba haki ya mwanamke pia ni haki ya binadamu ili tufike mahali suala lisiwe ni mwanamke au mwanaume, tuseme ana uwezo? Ndilo liwe suala.” Anasisitiza Bi. Mongella.
Matumaini
Pamoja na changamoto zilizopo, Balozi Gertrude Mongella ana matumaini na anatia ushuhuda akisema katika maisha yake kabla hawajaenda kwenye Mkutano wa Beijing, “kuzungumzia mwanamke kwenda kuwinda ilikuwa mwiko, kuzungumzia mwanamke kwenda kuvua samaki ilikuwa mwiko, kuzungumzia suala la kuchimba madini hiyo ndio mwiko zaidi mwanamke kwenda shimoni.” Lakini sasa anasema, “tunaanza kubadilika kuna vikundi vya akina mama wavuvi, wakina mama wachimba madini, wakina mama ambao wanafanya kazi na shughuli mbalimbali.”