Wanaohusika na ghasia za pwani Syria lazima wawajibishwe: UN
Wanaohusika na ghasia za pwani Syria lazima wawajibishwe: UN
Takriban miezi minne baada ya kuanguka kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad, Wasyria wengi walifurahia kukusanyika katika maeneo ya umma kusherehekea kuanza kwa majira ya chipukizi au Nowruz, lakini maeneo ya pwani yamekumbwa na ghasia za kutisha ambazo zimeleta hofu na wasiwasi kuhusu mustakabali wa nchi hiyo, amesema Geir Pedersen, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, akitoa taarifa leo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa.
Amesema mapigano makali kati ya vikosi vinavyohusiana na utawala wa zamani na vikosi vinavyounga mkono mamlaka mpya yamesababisha idadi kubwa ya vifo miongoni mwa makundi yenye silaha.
"Lakini lililo la kushtua zaidi ni idadi kubwa ya vifo vya raia, huku mauaji makubwa ya raia na watu wasio na silaha yakiripotiwa, na familia nzima zikiripotiwa kupigwa risasi kwa karibu," amesema Pedersen, akiongeza kuwa baadhi ya video zilionyesha ukiukwaji wa haki za binadamu wenye mlengo wa kidini na adhabu dhidi ya jamii ya Alawite.
Wanaohusika wanapaswa kuadhibiwa
Bwana Pedersen amesema Hali sasa imetulia, lakini kuna ripoti za unyanyasaji na vitisho, ikiwa ni pamoja na kwa misingi ya kidini.
Ameliambia Baraza la Usalama kwamba vikosi vya usalama vimeongeza uwepo wao katika maeneo ya pwani, huku baadhi ya wafuasi wa utawala ulioangushwa wakisema wataendelea kupigana.
Pedersen amesisitiza kuwa uchunguzi zaidi unahitajika ili kubaini na kuwafikisha mbele ya sheria wale waliohusika na ghasia dhidi ya raia.
"Kwa upande wao, mamlaka za mpito zilisema kuwa raia waliuawa na vikosi kutoka pande zote mbili, ikiwa ni pamoja na kukiri baadhi ya wajitolea na makundi mengine yanayohusiana nao”.
Wametangaza kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi itakayochunguza ukiukwaji wa haki uliofanywa na pande zote na kuwasilisha matokeo yake ndani ya siku 30, amesema Mjumbe Maalum.
Kamati hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana na mashirika husika ya Umoja wa Mataifa, ambayo yako tayari kutoa msaada unaohitajika.
Mjumbe huyo maalum amesema mamlaka za mpito pia zimetangaza kuundwa kwa Tume Kuu ya Amani ya Kiraia katika jimbo la Pwani.
Pedersen amesisitiza kuwa mashirika ya kiraia ya Syria yanapaswa kushiriki katika juhudi za kuondoa migawanyiko ya kimadhehebu na hali ya kutoaminiana.
Mgogoro eneo la Kaskazini-Mashariki
Mjumbe huyo Maalum pia amekumbusha kuwa mgogoro katika eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi bado unaendelea, ambapo mapigano kati ya Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF) na Jeshi la Kitaifa la Syria yanaendelea.
Wiki iliyopita, kulikuwa na ripoti za mashambulizi ya anga ya Uturuki katika maeneo yanayodhibitiwa na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria.
Uwepo wa Israel katika ukanda wa mgawanyiko
Mwezi Februari na Machi, Israel ilizindua mashambulizi dhidi ya eneo la kusini-magharibi mwa Syria, ikiwa ni pamoja na Damascus, Homs, na pwani.
Israel imethibitisha kuwa imejenga vituo katika ukanda wa mgawanyikoo, jambo linalokiuka Mkataba wa 1974 wa Kutenganisha Vikosi.
Kwa mantiki hiyo Bwana Pedersen amesema Baraza la Usalama linapaswa kudai Israel itimize ahadi zake, ijitoe kutoka Syria, na iheshimu uhuru na ukamilifu wa ardhi ya nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa unaendelea na mazungumzo na pande zote mbili ili kutafuta suluhisho.
Mkutano wa mazungumzo ya kitaifa
Mwezi Februari, mkutano wa mazungumzo ya kitaifa ulifanyika Damascus na kutoa tamko la mwisho lenye mapendekezo.
Ingawa kulikuwa na ushiriki wa makundi tofauti na mijadala ya wazi, mkutano huo ulikosolewa kwa ukosefu wa ujumuishi.
Mwezi Machi, serikali ya mpito iliwasilisha tamko la kikatiba lenye lengo la kurejesha utawala wa sheria na kuwezesha mchakato wa mpito wa kisiasa.
Ingawa hati hiyo ilipata uungwaji mkono fulani, mchakato wa kuandaa ulikumbwa na utata kutokana na ukosefu wa uwazi na mgawanyiko usio wazi wa madaraka kati ya matawi ya serikali.
Hatua zinazofuata
Kwa kumalizia, Pedersen ameeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele yanayostahili kupewa msukumo na jumuiya ya kimataifa.
Kwanza kabisa, alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa serikali ya mpito na baraza la sheria, ambalo linapaswa kuwa jumuishi na kuakisi matarajio ya wapiga kura wa Syria kutoka makundi mbalimbali.
Mjumbe huyo Maalum pia alisisitiza haja ya mabadiliko ya katiba na kuundwa kwa katiba ya kudumu.
Kwa mujibu wake, hili ni jambo muhimu sana katika maandalizi ya “uchaguzi huru na wa haki.”
Umoja wa Mataifa unachukua jukumu muhimu katika kusaidia mchakato huu amesema akisisitiza umuhimu wa suluhu za Kisyria zenye msaada wa kimataifa, akibainisha kuwa hatua hizi ni msingi wa mpito endelevu na jumuishi.
Hali ya kibinadamu bado ni ngumu- Fletcher
Hali ya kibinadamu nchini Syria bado ni mbaya, lakini kuna ishara za maendeleo, amesema Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher. Akizungumza mbele ya Baraza hilo amesema kuwa usambazaji wa misaada mipakani kutoka Uturuki umeongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka, na kuruhusu maghala kote nchini, yakiwemo Damascus na Homs, kupata vifaa vya msaada.
Amesema “Tunapiga hatua shukrani kwa timu zetu zilizo mashinani na wale wanaotuunga mkono katika operesheni zetu kubwa za kibinadamu,”
Moja ya mafanikio makubwa ni urejeshaji wa kituo cha kusambaza maji katika eneo la Atarib, mkoa wa Aleppo, tarehe 14 Machi. Kituo hiki kinatumia nishati ya jua na kinatoa maji safi kwa watu 40,000.
Zaidi ya hayo, amesema silaha zisizolipuka zipatazo 1,700 zimeteketezwa nchini Syria, na hivyo kuunda mazingira salama kwa watu kurejea nyumbani.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), wakimbizi 355,000 wameweza kurejea makwao tangu Desemba mwaka jana.
Hata hivyo, mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.
Dola bilioni 2 zinahitajika katika miezi ijayo kusaidia Wasyria milioni 8 walio hatarini zaidi. Hadi sasa, ni asilimia 13 tu ya kiasi hicho takriban dola milioni 155 ndizo zimepatikana.
Fletcher amesema“Kupungua kwa ufadhili hakumaanishi kuwa mahitaji ya kibinadamu yatapungua. Zaidi ya watu milioni 16 karibu robo tatu ya idadi ya watu wote bado hawana chakula, maji, makazi yanayofaa na huduma za msingi.”
Ameongeza kuwa licha ya maboresho ya kiasi fulani ya kiusalama tangu Desemba, mapigano yanaendelea katika maeneo kadhaa, yakisababisha vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu. Tangu mwanzo wa mwaka, zaidi ya watu 600, wakiwemo watoto, wameathirika na mabomu na silaha nyingine za kivita.
Fletcher amehitimisha kwa kusema kuwa Jumuiya ya kimataifa inapaswa kusaidia ujenzi mpya wa Syria na kutenga rasilimali muhimu kwa ajili ya mchakato huu.