Unyafuzi tishio kwa watoto na jamii nzima Yemen - UNICEF
Unyafuzi tishio kwa watoto na jamii nzima Yemen - UNICEF
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen vikitimiza muongo mmoja, zaidi ya nusu ya watoto nchini humo wanakabiliwa na unyafuzi yaani utapiamlo mkali, limesema hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini humo.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen, Peter Hawkins, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya video kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana’a, amesema “muongo mmoja wa mzozo umekuwa mbaya sana kwa watoto wa nchi hiyo wanaoishi chini ya tishio la mashambulizi ya anga na viwango vya juu sana vya utapiamlo.”
Wayemen wamekata tamaa, sisi tusikate tamaa
Amesema ni wakati wa kuchukua hatua haraka, huku akielezea kile alichoshuhudia alipotembelea eneo la Hudaydah siku tatu zilizopita.
“Nilipitia maeneo ya nyanda za chini upande wa magharibi, ambapo kuna watu mitaani, kando ya barabara, wakiomba msaada. Wao wamekata tamaa. Lakini sisi hatuwezi kukata tamaa,” amesema Hawkins.
Bwana Hawkins amesema janga la vita Yemen limeharibu uchumi wa Yemen, mfumo wa afya na miundombinu. “Hata wakati wa vipindi vya kupungua kwa vurugu, matokeo ya madhara ya mzozo huu, hasa kwa wasichana na wavulana, yamebaki kuwa makubwa,” amesema, akisisitiza kwamba zaidi ya nusu ya takribani watu wote milioni 40 nchini Yemen wanategemea msaada wa kibinadamu.
UNICEF imesaidia vituo vya afya vinavyotoa huduma za kuokoa maisha na matibabu ya utapiamlo kote nchini, lakini shughuli zake zimefadhiliwa kwa asilimia 25 tu mwaka huu.
Bwana Hawkins ameonay kuwa shirika hilo halitaweza kudumisha hata huduma za kimsingi bila ufadhili wa haraka.
Msingi wa mapigano Yemen
Nchini Yemen wapiganaji wa kihouthi, wanaojulikana rasmi kama Ansar Allah – wamekuwa wakipigana na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kwa zaidi ya muongo mmoja na walimwondoa Rais wa nchi hiyo Abd Rabbu Mansour Hadi mwezi Machi mwaka 2015.
Ingawa kuanza tena kwa operesheni kubwa za kijeshi za ardhini nchini Yemen hakujatokea tangu usitishaji wa mapigano uliofanywa na Umoja wa Mataifa, mwezi Aprili 2022, shughuli za kijeshi zinaendelea.
Sitisho la mapigano mashakani
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg alionya tarehe 6 mwezi huu katika mkutano wa Baraza la Usalama kwamba kusitishwa kwa mapigano kunazidi kuwa mashakani.
Mapema mwezi huu Marekani ilizindua mashambulizi kadhaa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na wahouthi nchini Yemen, ikiripotiwa kuwa ni kulipiza kisasi kwa kulenga meli za kibiashara na za biashara katika Bahari ya Sham.
Bw. Hawkins amezungumza kuhusu uharibifu aliouona mwenyewe katika mji wa bandari wa Hudaydah na kusisitiza kwamba watoto 8 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya hivi karibuni kaskazini mwa Yemen.
“Bandari na barabara muhimu, ni njia muhimu za kupitisha vyakula na dawa za kuokoa uhai, nazo zimeharibiwa au kuwekewa vizuizi,” amesema Bwana Hawkins.
Takwimu muhimu Yemen:
- Bei za chakula zimepanda zaidi ya asilimia 300 katika muongo uliopita, na kusababisha njaa na utapiamlo.
- Mtoto 1 kati ya 2 wenye chini ya umri wa miaka mitano ana utapiamlo
- Zaidi ya wasichana na wavulana 540,000 wana unyafuzi
- Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha milioni 1.4 wana utapiamlo