Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda yaunga mkono hatua ya M23 kujiondoa Walikale, DRC na kusitishwa kwa mapigano

Kama watu wengi waliokimbia makazi yao huko Bulengo, Francine alihofia usalama wa familia yake.
© WFP/Michael Castofas
Kama watu wengi waliokimbia makazi yao huko Bulengo, Francine alihofia usalama wa familia yake.

Rwanda yaunga mkono hatua ya M23 kujiondoa Walikale, DRC na kusitishwa kwa mapigano

Amani na Usalama

Taarifa iliyotolewa leo mjini Kigali nchini Rwanda imesema kuwa, mamlaka ya Rwanda jana Jumapili iliunga mkono uamuzi wa kundi la waasi la M23 kujiondoa katika mji muhimu wa madini wa Walikale na hatua ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kusitisha mapigano katika mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC.

Taarifa kutoka ofisi ya msemaji wa serikali ya Rwanda imeeleza kuwa Rwanda inaunga mkono juhudi zinazoendelezwa ili kufanikisha suluhisho la kisiasa na usalama wa kudumu katika eneo hilo.

"Rwanda inaunga mkono tangazo la M23 la kuhamasisha vikosi vyake kutoka Walikale kuunga mkono juhudi za amani zinazoendelea, pamoja na tangazo la DRC kwamba operesheni zote za Jeshi la serikali ya  Congo Congo FARDC na Wazalendo ambao ni wanamgambo wanaoiunga mkono serikali zitasitishwa. Rwanda imejitolea kushirikiana na pande zote kuhakikisha utekelezaji wa ahadi, hasa katika muktadha wa mchakato wa pamoja wa mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, EAC-SADC na juhudi zingine zinazolenga kutatua mzozo kwa njia ya kisiasa na kiusalama kwa muda mrefu katika eneo hilo " imesema taarifa hiyo.

M23 yatangaza kujiondoa Walikale

Muungano wa waasi wa Alliance Fleuve Congo, unaojumuisha kundi la M23, ulitangaza Jumamosi nia yake ya kuhamasisha vikosi vyake kutoka mji wa Walikale na maeneo jirani ili kuunga mkono juhudi za amani zinazolenga kuweka mazingira ya mazungumzo ya kisiasa yatakayoshughulikia mizizi ya mgogoro mashariki mwa DRC.

Baada ya tangazo hilo la waasi, jeshi la Congo pia limesema limevitaka vikosi vya kujilinda vya Congo kupunguza mvutano ili kutoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani na kuendeleza mchakato wa mazungumzo ya Luanda na Nairobi.

Mgogoro unaendelea Mashariki mwa DRC

Tangu kuzidisha mashambulizi mwaka jana, waasi wa M23 wameteka maeneo mengi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

DRC na nchi nyingine zimeishutumu Rwanda kwa kusaidia kundi la M23, madai ambayo Rwanda inaendelea kuyakanusha.

Wiki iliyopita, Rais wa DRC Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo muhimu yaliyosimamiwa na Emir wa Qatar mjini Doha, ikiwa ni mkutano wa hivi karibuni tangu M23 walipoteka miji mikuu ya Goma na Bukavu mwaka huu.

Katika kipindi cha chini ya miezi mitatu, idadi ya raia wa Congo waliokimbia mzozo kwenda nchi jirani imeongezeka hadi zaidi ya watu 100,000, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.