Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani ni janga kubwa kwa vita dhidi ya ukimwi na chachu ya vifo: UNAIDS

Mtetezi wa matibabu, Elizabeth Sangu, anapokea dawa zake zilizojazwa tena kutoka kwa muuguzi katika Kituo cha Tambukareli CTC huko Temeke, Dar es Salaam, Tanzania.
© UNAIDS/Daniel Msirikale Mgonjwa nchini Tanzania akipokea dawa za kupunguza makali ya VVU kutibu VVU.

Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani ni janga kubwa kwa vita dhidi ya ukimwi na chachu ya vifo: UNAIDS

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS leo limeonya kwamba kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani sio tu janga kwa vita dhidi ya gonjwa hilo bali ni chachu ya vifo na ongezeko la maambukizi mapya. Flora Nducha amefuatilia onyo hilo lililotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Mkurugenzi mtendaji wa UNAUDS Winnie Byanyima alipozungumza na waandishi wa habari.

Bi. Byanyima amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya Marekani imekuwa mfadhili mkubwa wa mipango ya kukabiliana na UKIMWI, hasa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).

Hata hivyo, kukatwa kwa msaada wa kifedha sasa kunahatarisha programu muhimu zinazotoa matibabu ya kuokoa maisha, huduma za kuzuia maambukizi, na utafiti wa kisayansi hasa kwa nchi ambazo msaada huo ni tegemeo kubwa mathalani amesema “Lakini sasa hebu fikiria nchi kama Tanzania ambayo inategemea asilimia 94 ya mapambano yake msaada kutoka nje na hasa Marekani hivyo athari zitakazojitokeza unaweza kuona .”

UNAIDS inatahadharisha kuwa bila msaada wa kifedha wa kutosha, mamilioni ya watu, hasa katika nchi zenye kipato cha chini, wanaweza kukosa huduma muhimu za UKIMWI na hasa wale wanaotegemea dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ili kuendelea kuishi akisema “Hata kufurugwa kwa muda mfupi kwa matibabu kuna athari kubwa kwa watu wanaoishi na HIV. Endapo mtu ataruka kunywa dozi kutamsababishia usugu wa dawa , hii itaongeza idadi ya virusi, na hii itaongeza maambukizi.”

Mwanamke mwenye tabasamu na mtoto mdogo ameketi kwenye kaunta ya hospitali nchini Zimbabwe. Mfanyakazi wa afya anampatia mwanamke huyo chupa ya dawa.
© UNAIDS/Cynthia R Matonhodze Mama anayeishi na virusi vya Ukimwi akipokea dawa za kupunguza makali ya VVU kwenye hospitali moja nchini Zimbabwe. (Maktaba)

Bi Winnie amesema waathirika wakubwa katika zahma hii ya ukataji ufadhili ni jamii zilizo hatarini, zikiwemo wanawake, watoto, na makundi yaliyotengwa ambayo tayari yanakumbwa na changamoto za kupata huduma za afya hususan  Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kiwango cha maambukizi ya UKIMWI bado ni cha juu, na hivyo kupungua kwa msaada wa kifedha kunaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi na kuboresha upatikanaji wa matibabu.

Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kurudi nyuma kwa maendeleo katika juhudi za kimataifa za kumaliza janga la UKIMWI ifikapo 2030.

UNAIDS na mashirika mengine ya afya duniani yameitaka serikali ya Marekani kufikiria upya uamuzi wake wa kupunguza ufadhili, yakisisitiza kuwa uwekezaji endelevu ni muhimu ili kuendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Tathimini ya bara la Afrika

Akizungumzia Afrika ambako Mashariki na Kusini mwa bara hilo kunabeba asilimia 53 ya mzigo wa VVU duniani  Bi. Byanyima ameonya kwamba kufunga ghafla vituo vya msaada kwa wasichana na wanawake vijana kutakuwa na madhara makubwa, kwa sababu zaidi ya asilimia 60 ya maambukizi mapya ya VVU barani humo yanawaathiri wasichana na wanawake vijana.

Akizungumza na UN News mapema mwezi huu, mkuu wa ofisi ya UNAIDS nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Susan Kasedde, alisema bado kuna maswali makubwa kuhusu kiwango na upeo wa kupunguzwa kwa ufadhili wa mpango wa PEPFAR wa Marekani.

Mpango huu, ulioanzishwa mwaka 2003, unalenga kuzuia na kudhibiti maambukizi ya VVU ukiwa ni mpango wa dharura wa urais wa Marekani ambao unakadiriwa kuwa umeokoa maisha ya takriban watu milioni 26.

Kwa sasa, kuna takriban watu 520,000 wanaoishi na VVU nchini DRC, wakiwemo wanawake 300,000 na watoto 50,000. Janga hili linaendelea kukua, kwani idadi ya maambukizi mapya karibu inazidi mara mbili idadi ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa UNAIDS Mchango wa PEPFAR uliotarajiwa kwa mwaka wa kifedha wa 2025 ulikuwa ni dola milioni 105, na unalenga kutoa matibabu kwa nusu ya watu wanaoishi na VVU nchini DRCambao ni takriban watu 209,000.

"Hii inamaanisha kuwa kwa sasa tuna watu 440,000 wanaoishi na VVU ambao wanapata matibabu. Kupitia matibabu haya, wanaendelea kuishi," alisema Bi. Kasedde.

Aliongeza kuwa "Na matibabu haya hayawezi kufanikiwa bila uwezo wa kiutendaji. Matibabu hayawezi kutolewa ikiwa hakuna mnyororo wa ugavi unaofanya kazi ipasavyo," alisisitiza, akionyesha kuwa hatua dhidi ya VVU nchini DRC zinategemea kwa kiasi kikubwa programu zinazoingiliana na kusaidiana.

Mwelimishaji rika Florentine Arapri anaonyesha matokeo hasi ya kipimo cha VVU kwa mteja, Blondine Terminé, huko Moutarwa, Kamerun.
© UNICEF/Frank Dejongh Mwanamke huko Moutarwa, Cameroon, anashikilia kipimo cha VVU ambacho kinaonyesha matokeo hasi, au thibitisho kuwa hana virusi vya UKIMWI.

Athari za kimataifa za kupunguzwa kwa ufadhili

Mashirika mengine kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanayotegemea kwa kiasi kikubwa ufadhili wa Marekani pia yameonya kwamba kupunguzwa kwa msaada  pamoja na uwekezaji duni wa muda mrefu katika kazi za kibinadamu duniani tayari kuna athari kubwa kwa jamii wanazohudumia.

Ijumaa iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilisema kwamba maelfu ya watu wameachwa bila msaada muhimu wa kuokoa maisha katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, linalokumbwa na vita.

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, pia lilitangaza kwamba kupunguzwa kwa ufadhili kuna madhara makubwa kwa jamii za wahamiaji walio hatarini, hali inayozidisha migogoro ya kibinadamu na kudhoofisha mifumo muhimu ya msaada kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao.

Pamoja na IOM, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF lilionya Ijumaa kwamba mgogoro wa kifedha umeathiri vibaya kazi za kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na maendeleo katika kupunguza vifo vya watoto, ambavyo vimepungua kwa asilimia 60 tangu 1990.

"Ni jambo la kueleweka kwamba Marekani inataka kupunguza ufadhili wake kwa muda. Lakini uondoaji wa ghafla wa msaada wa kuokoa maisha unaleta athari mbaya katika mataifa mbalimbali, hususan Afrika, lakini pia Asia na Amerika ya Kusini," ameema Bi. Byanyima wa UNAIDS akuongeza kuwa "Tunaomba hatua hii itathminiwe upya na huduma za kuokoa maisha zirejeshwe haraka."

Rai kwa Rais wa Marekani

Katika ombi la moja kwa moja kwa Rais Donald Trump, mkuu wa UNAIDS amebainisha kuwa, kama vile Rais George W. Bush alivyotambulisha mpango wa mageuzi wa PEPFAR, kiongozi mpya wa Ikulu ya Marekani pia anaweza kuwa sehemu ya "mapinduzi ya kinga dhidi ya VVU”.

Hii inajumuisha matumizi ya sindano za VVU zinazodungwa mara mbili tu kwa mwaka ili kutoa ulinzi kamili unaohitajika.

"Mkataba huu unahusu kampuni ya Marekani kupewa uwezo wa kuzalisha na kutoa leseni kwa dawa za gharama nafuu katika kanda mbalimbali ili kuzalisha mamilioni ya dozi na kueneza matumizi ya sindano hii kwa wale wanaoihitaji zaidi," amesisitiza.

Kulingana na takwimu za UNAIDS za mwaka 2023, takriban watu milioni 40 duniani wanaishi na VVU.

Kati ya idadi hiyo, takriban milioni 1.3 walipata maambukizi mapya ya VVU katika mwaka huo, huku watu 630,000 wakifariki duni kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.