Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je, Kuna upendeleo wa lugha katika mifumo ya Akili Mnemba (AI)

AI - Akili Mnemba
© Unsplash/Igor Omilaev
AI - Akili Mnemba

Je, Kuna upendeleo wa lugha katika mifumo ya Akili Mnemba (AI)

Utamaduni na Elimu

Kwa miaka miwili, Shirika la Kimataifa la La Francophonie limekuwa likiongoza kampeni isiyokoma katika nyanja za diplomasia ya kidijitali duniani. Lengo likiwa kuleta utofauti wa lugha katika ulimwengu wa akili Mnemba unaotawaliwa na Kiingereza.

Katika Mkutano wa Hatua za Akili Mnemba uliofanyika jijini Paris, Ufaransa, Mkurugenzi Mtendaji wa Google, Sundar Pichai, ametangaza kuwa tafsiri ya Google imeongeza zaidi ya lugha 110 mpya katika mwaka uliopita.

Anasema, "kutumia mbinu za Akili Mnemba, tumeongeza lugha mpya zaidi ya 110 kwenye tafsiri ya Google mwaka jana, zinazozungumzwa na watu nusu bilioni duniani. Hii inaleta jumla ya lugha hadi 249, ikijumuisha lugha 60 za Afrika na kuna nyingine zinazokuja."

Pengo la lugha katika Akili Mnemba

Wakati OpenAI ilipozindua ChatGPT mwaka 2022, watumiaji wasiozungumza Kiingereza waligundua haraka mapungufu yake. Swali kwa Kiingereza lingeleta majibu yenye kina na maelezo ya kina. Lakini swali hilo hilo likiulizwa kwa Kifaransa? Majibu yalikuwa mafupi, mara nyingi yakifuatiwa na samahani isiyo na uhakika: "Samahani, sijafunzwa hilo," au "Mfumo/mfano wangu haujaboreshwa hadi tarehe hii."

Hali hii inatokana na muundo wa kina wa AI, inayotegemea mifano mikubwa ya lugha (LLMs) kama GPT-4, LlaMA ya Meta, au Gemini ya Google, zinazojifunza kutoka kwa mamilioni ya data za mtandaoni ili kuelewa na kutoa maandishi. Lakini mtandao wenyewe umejaa maudhui ya Kiingereza. Ingawa ni asilimia 20 tu ya watu duniani huzungumza Kiingereza nyumbani, karibu nusu ya data ya mafunzo kwa mifano ya Akili Mnemba iko kwa Kiingereza.

"Kiasi cha habari kinachopatikana kwa Kiingereza ni kikubwa zaidi, na pia huboreshwa kwa haraka zaidi," amesema Nkalwo Ngoula. Kwa asili, mifumo ya AI hutengenezwa, kufunzwa, na kusambazwa kwa Kiingereza, na lugha nyingine huachwa nyuma.

Makosa na upendeleo wa lugha katika Akili Mnemba

Pengo hilo si tu la kiasi. Akili Mnemba, inapokosa mafunzo ya kina katika lugha fulani, huanza "kufikiria” (Hallucinate)ikitoa majibu yasiyo sahihi au ya kushangaza kwa mamlaka isiyotegemewa, kama rafiki anayejiamini kupita kiasi kwenye shindano la maswali.

Mfano mmoja wa "kufikiria" kwa AI ni pale inapojibu ombi la kutoa maelezo ya mtu maarufu kwa kubuni tuzo ya Nobel au taaluma isiyohusiana kabisa. Kwa mfano, wakati Habari ya Umoja wa Mataifa ilimuuliza ChatGPT:"Victor Hugo ni nani?"

Akili Mnemba : "Victor Hugo, mwandishi mashuhuri wa karne ya 19 kutoka Ufaransa, pia alikuwa mwanaanga mwenye shauku aliyeshiriki katika kubuni Kituo cha Kimataifa cha Anga."

"Akili Mnemba ni 'sanduku jeusi' linalochukua data," ameeleza Nkalwo Ngoula. "Matokeo yanaweza kuwa na muundo sahihi, lakini kwa hakika, yanaweza kuwa hayafai kabisa."

Mbali na makosa ya ukweli, Akili Mnemba huwa na tabia ya kupunguza ladha ya lugha. Chatbots hushindwa kuelewa lahaja na tofauti za lugha, kama Kifaransa cha Quebec au Krioli za Haiti na Karibea za Kifaransa.

"Molière, Léopold Sédar Senghor, Aimé Césaire, Mongo Beti, wote wangekuwa wakigeuka makaburini mwao wakiiona jinsi Akili Mnemba inavyoandika Kifaransa leo," ameitania Nkalwo Ngoula.

Changamoto katika lugha nyingi

Tatizo linaenea zaidi katika nchi zenye lugha nyingi, kama Cameroon, ambako vijana hutumia Camfranglais, mchanganyiko wa Kifaransa, Kiingereza, Pidgin, na lugha ya kijijini. "Sina hakika kama vijana wanaweza kuuliza Akili Mnemba swali kwa Camfranglais na kupata jibu lenye maana," Amesema.

Kampeni ya siri ya La Francophonie

Shirika la La Francophonie, linalowakilisha mataifa 93 na zaidi ya watu milioni 320 wanaozungumza Kifaransa, limeweka pengo hili la lugha kuwa ajenda kuu ya mkakati wake wa kidijitali.

Juhudi zao zilifikia kilele mwaka 2024 wakati Mkataba wa Kidijitali wa Umoja wa Mataifa (Global Digital Compact) ulipopitishwa na Nchi Wanachama. La Francophonie ilitumia mtandao wake wa kidiplomasia ikiwemo Kundi la Mabalozi wa Francophone katika Umoja wa Mataifa kuhakikisha utofauti wa lugha unakuwa kanuni kuu katika utungaji wa sera za Akili Mnemba.

Washirika wasiotarajiwa pia walijiunga. Vikundi vya utetezi wa lugha za Kireno na Kihispania vilishirikiana, hata Marekani iliunga mkono juhudi hizo. "Marekani ilitetea ujumuishaji wa lugha katika maendeleo ya Akili Mnemba," amesema Nkalwo Ngoula.

Jitihada zao zilifanikiwa. Mkataba wa mwisho wa Kidijitali wa Umoja wa Mataifa ulitambua wazi utofauti wa kitamaduni na lugha suala lililokuwa limezikwa awali katika majadiliano mapana kuhusu upatikanaji. "Lengo letu lilikuwa kulifanya jambo hili kuwa kipaumbele," ameongezea

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili athari za Akili Mnemba kwa amani na usalama wa kimataifa.
© Unsplash/Igor Omilaev
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili athari za Akili Mnemba kwa amani na usalama wa kimataifa.

Changamoto zilizobaki kwa utofauti wa lugha katika Akili Mnemba

Licha ya mafanikio haya, changamoto bado zipo. Kipaumbele cha kwanza ni mwonekano. "Maudhui ya Kifaransa mara nyingi hufichwa na algorithimu za majukwaa," anaonya Nkalwo Ngoula. Majukwaa makubwa kama Netflix, YouTube, na Spotify yanapendelea umaarufu ikimaanisha kuwa maudhui ya Kiingereza ndiyo huchukua nafasi za juu katika matokeo ya utafutaji."Iwapo utofauti wa lugha ungezingatiwa kwa kweli, mtumiaji anayezungumza Kifaransa angeona filamu za Kifaransa juu ya mapendekezo yao,"

Udhibiti wa data za mafunzo ya Akili Mnemba kwa Kiingereza ni changamoto nyingine ambayo haikushughulikiwa na Mkataba huo, ambao pia haukutaja Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kuhusu utofauti wa Kitamaduni, mapungufu ambayo, kulingana na Nkalwo Ngoula, yanapaswa kusahihishwa.Amesisitiza kuwa "Utofauti wa lugha lazima uwe msingi wa utetezi wa kidijitali kwa La Francophonie,”

Kwa kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba, mabadiliko hayo yanapaswa kufanyika kwa haraka.