Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu DRC kufuatia ukata wa fedha

Maelfu ya watu wamekimbia kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuingia Burundi. (Maktaba)
© UNHCR/Bernard Ntwari
Maelfu ya watu wamekimbia kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuingia Burundi. (Maktaba)

UNHCR yatahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu DRC kufuatia ukata wa fedha

Amani na Usalama

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, (UNHCR) limeonya kuwa ukata mkubwa wa fedha unakwamisha juhudi za kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi jirani, na kusababisha hali mbaya zaidi ya kibinadamu.

Katika miezi mitatu iliyopita, zaidi ya Wacongo 100,000 wamekimbilia nchi jirani kutokana na kuongezeka kwa ghasia, hasa katika maeneo ya Masisi na Walikale katika jimbo la Kivu Kaskazini, na Bukavu katika Kivu Kusini. Jijini Goma, maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yakihifadhi wakimbizi wa ndani 400,000 yameharibiwa, na familia zimeachwa bila makazi au ulinzi. Wadau wa kibinadamu, wakikabiliwa na ukosefu wa fedha, wanashindwa kujenga upya makazi au kusambaza misaada muhimu.

Safari za hatari na mazingira magumu

Tangu Januari 2025, zaidi ya wakimbizi wa ndani 40,000 kutoka Kivu Kaskazini na Kusini wamefika Kalemie, jimbo la Tanganyika, baada ya safari hatari za kilomita 700 kupitia maeneo ya vita na kuvuka viziwa. Wengi wao ni vijana wanaotoroka kujiunga na makundi ya wapiganaji kwa lazima, na wanawake na watoto waliotenganishwa na familia zao. Safari hizo hatari zimesababisha majanga kadhaa ya kuzama kwa boti kutokana na msongamano na vyombo dhaifu.

Janga la wakimbizi Uganda na Burundi

Nchini Uganda, zaidi ya Wacongo 28,000 wamevuka mpaka tangu Januari, ongezeko la asilimia 500 ikilinganishwa na mwaka jana. Vituo vya mapokezi vimefurika, vikihifadhi mara saba zaidi ya uwezo wake, huku ukosefu wa maji, usafi wa mazingira, na makazi ukiathiri hali ya wakimbizi. Vituo vya afya vimelemewa, huku utapiamlo kwa watoto ukiongezeka baada ya kufungwa kwa vituo vya lishe.

Katika eneo la Rugombo nchini Burundi, ambapo wakimbizi 68,000 wamewasili tangu Februari, msongamano na uhaba wa huduma za usafi umechochea visa vya kolera. Bila ufadhili wa haraka, kuna hatari kubwa ya kuenea kwa magonjwa, huku kambi mpya za wakimbizi zikijaa kupita uwezo wake. Uhaba wa chakula unazidi kuwa mbaya, na huduma kwa makundi yaliyo hatarini, ikiwa ni pamoja na watoto wasio na walezi na waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia, ziko kwenye shinikizo kubwa.

Ombi la dharura la ufadhili

UNHCR imetoa shukrani kwa wafadhili waliotoa msaada lakini imesisitiza kuwa mahitaji yanayoongezeka yanazidi rasilimali zilizopo. Bila ufadhili wa haraka, hali ya kibinadamu DRC na nchi jirani itazidi kuzorota, na kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu.