Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: ‘Rudisheni mateka wote nyumbani sasa,’ mateka aliyeachiwa aliambia Baraza la Usalama

Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama UN mjini New York kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.
UN Photo/Eskinder Debebe Mtazamo mpana wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Wapalestina.

Gaza: ‘Rudisheni mateka wote nyumbani sasa,’ mateka aliyeachiwa aliambia Baraza la Usalama

Amani na Usalama

Afisa mwandamizi wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa leo ametoa wito kwa Israel na Hamas kurejesha usitishaji mapigano ulioharibika Gaza na kuwaachilia mateka wote waliobaki, huku mmoja wa waliokuwa mateka akieleza Baraza la Usalama kuhusu siku 500 za mateso akiwa ametekwa.

Akiwapa mabalozi muhtasari, Khaled Khiari, Naibu Katibu Mkuu katika Idara ya Masuala ya Kisiasa (DPPA), amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unalaani vikali mashambulizi mabaya yaliyofanywa na Hamas na makundi mengine ya wanamgambo wa Kipalestina dhidi ya jamii za Israeli mnamo 7 Oktoba 2023.

Zaidi ya Waisraeli 1,200 waliuawa kikatili, na zaidi ya 250 walitekwa nyara. Takribani watu 59 wakiwa hai na waliokufa bado wanashikiliwa na Hamas na makundi mengine yenye silaha ndani ya Ukanda wa Gaza.

“Hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha mauaji ya makusudi, mateso, unyanyasaji wa kingono na uharibifu – familia nzima ziliuawa, kuchomwa moto majumbani mwao, na kutekwa nyara,” amesema Khiari.

“Matukio ya siku hiyo ya kutisha hayatasahaulika.”

Khaled Khiari, Katibu Mkuu Msaidizi wa Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki, anawasilisha taarifa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.
UN Photo/Eskinder Debebe Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki, Khaled Khiari akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.

Kuongezeka kwa mgogoro

Bwana Khiari pia ameripoti kuhusu kuzorota kwa hali ya Gaza baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji mapigano wa miezi miwili na mpango wa kuachiliwa kwa mateka – na kurejea kwa mapigano kamili.

Mashambulizi ya anga ya Israeli yamesababisha vifo vya mamia ya Wapalestina, wakiwemo wanawake na watoto, amesema, akiongeza kuwa wafanyakazi sita wa Umoja wa Mataifa pia wameuawa katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Akitoa wito wa kurejeshwa haraka kwa usitishaji mapigano, Khiari ameonya kuwa “kadri siku zinavyopita, tunazidi kujiepusha na lengo la kuwarudisha mateka waliobaki salama nyumbani kwao.”

Amelikumbusha Baraza la Usalama kuhusu maelezo ya mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, mapema wiki hii: “usitishaji mapigano upya ndiyo njia bora zaidi ya kulinda raia huko Gaza, katika maeneo yanayokaliwa ya Palestina, na Israeli kuachilia mateka na wafungwa na kuruhusu misaada na bidhaa za kibiashara kuingia.”

Mvulana mdogo wa Kipalestina akipita kwenye hema la wakimbizi lililoharibiwa huko Mawasi, Khan Younis, katikati ya vifusi na uchafu kutoka kwa shambulio la anga.
© UNICEF Mvulana akipekua mabaki ya mali ya familia yake kufuatia mashambulizi mapya ya anga huko Gaza.

Ushuhuda wa manusura: Nimerejea kutoka kuzimu

Baraza la Usalama pia limekisikiliza ushuhuda wa Eli Sharabi, Muisraeli aliyenusurika baada ya kukaa mateka kwa siku 491 chini ya Hamas. Alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Kibbutz Be’eri mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, Sharabi alishikiliwa chini ya ardhi, akifungwa kwa minyororo, akinyimwa chakula, na kufanyiwa mateso ya kisaikolojia na kimwili.

“Nimetoka kuzimu,” amewaambia mabalozi.

“Kwa siku 491, nilishikiliwa katika mahandaki ya kigaidi ya Hamas… nikiwa kifungoni gizani, nikiwa peke yangu, mbali na dunia kwa mikono ya magaidi wa Hamas,” ameendelea.

“Kwa siku 491, nilishikilia matumaini, niliwaza kuhusu maisha ambayo tungeweza kujenga upya, niliota kuiona familia yangu tena,” amesema. 

Hata hivyo, aliporejea nyumbani mwezi uliopita, aligundua ukweli mchungu kwamba mkewe na binti zake wawili waliuawa na Hamas mnamo 7 Oktoba.