Tukizingatia usawa wa kijinsia, tutafanikisha SDGs zote – Prof. Smile
Tukizingatia usawa wa kijinsia, tutafanikisha SDGs zote – Prof. Smile
Hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake Duniani CSW69 umebakiza siku moja tu kukunja jamvi kesho Machi 21. Wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wameendelea kutoa maoni yao ni kwa vipi Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs yanaweza kufanikishwa kwa kusongesha usawa wa kijinsia.
Miongoni mwa mashirika yaliyohudhuria mkutano huu ni I believe Global, shirika lisilo la kiserikali linalojikita na lengo namba 5 (SDG5) la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGS wakitetea Usawa wa kijinsia na haki za binadamu kwa wanawake na wasichana katika nyanja zote kote duniani.
Usawa wa kijinsia ni mtambuka
Profesa Smile Dzisi, Mkurugenzi wa shirika hilo kutoka Ghana amezungumza na Selina Jerobon wa Idhaa hii na kusema kwamba “letu ni kufikia usawa wa kijinsia ambao ni lengo namba 5 la malengo ya Maendeleo endelevu. Tumefanya utafiti na kuona kwamba tunapozingatia usawa wa kijinsia, matokeo ya mapambano yetu ya kimataifa na mashinani ni kufikiwa kwa malengo yote 17.”
Hivyo basi lengo letu ni kuhakikisha kwamba katika nchi zinazoendelea kiuchumi, kama nchi nyingi za Afrika, tumefikia usawa wa kijinsia katika nyanja zote kwa mfano elimu, mabadiliko ya tabianchi, siasa na uchumi. Mafanikio haya yote inamaanisha uchumi wetu katika nchi zinazoendelea unafikiwa.
Ni miaka 30 sasa tangu Azimio la Beijing na Jukwaa la Hatua za Utekelezaji wa azimio hilo la haki za wanawake na masuala yanayoathiri usawa wa kijinsia, matarajio yake mengi hayajatimia.
Akaulizwa je, wanafanya nini mashinani, mathalani nchini Ghana au wanapotembelea nchi zingine barani Afrika kuhakikisha kuwa lengo hili linatekelezwa wakati huu ambapo bado kuna changamoto kufikia usawa wa kijinsia?
Tushikamane tusifanye kazi kwa utengano
Profesa Smile Dzisi akafunguka kwa kusema, “ninakubaliana na wewe kwamba mengi hayajafikiwa, kwa sababu tumekuwa tukishughulikia masuala kwa kujitenga sisi wenyewe. Tunapaswa kukabiliana nayo kikamilifu na kuwashirikisha wadau wote. Haimaanishi kwamba ni wanawake au mashirika ya wanawake au wanaharakati wanawake pekee waongoze harakati kuhusu kufikiwa kwa usawa wa kijinsia, kutokomeza ukatili wa kijinsia na masuala yote.”
Tunahitaji kuja pamoja, mashirika yote, wanaharakati wote wa jinsia zote. Katika I believe Global tunatambua kuwa kuhusisha wanaume ni muhimu sana. Kwa hiyo tunao wanaume wengi mashinani, kimataifa na tunawatumia kwenye vuguvugu na kampeni, kwenye programu za uhamasishaji ili wafikie taasisi zote, mila, jamii zote na dini zote, wajue kwamba kufikia usawa wa kijinsia maana yake ni maendeleo ya nchi yetu, sio tu wanawake bali nchi nzima itasonga mbele.
Ushirikiano na taasisi za elimu ya juu
Profesa Smile Dzisi akaenda mbali zaidi kufafanua hatua wanazozichukua kujengea uwezo wanawake na wasichana kote barani Afrika akisema, “tunashughulikia taasisi ya elimu. Ukiangalia nyadhifa zetu za uongozi, kwenye mabaraza na nyadhifa za juu, unaona wanaume wengi sana. Kwa hiyo ni nini kimezuia wanawake, kwani hawawezi jukumu hilo?” amehoji.
Ametamatisha kwa kusema kuwa chochote mwanaume anachoweza kukifanya pia wanawake wanaweza. Kwa hivyo “tunalenga wanawake, tunawasaidia katika machapisho, katika utafiti na masuala mengine ili waweze kupata nyadhifa zao.”
Hivyo amesisitiza kuwa dunia ishikamane kuwaunga mkono wasichana na wanawake katika kila nyanja kote duniani hususani barani Afrika na nchi zenye mapato ya chini, kwani wanawake na wasichana wanaweza, na uwekezaji kwa mwanamke ni uwekezaji kwa jamii na maendeleo ya nchi.