Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la uwajibikaji litachochewa na kukata ufadhili - Grandi

Wanawake mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini wakibeba chakula kilichowasilishwa na  Umoja wa Mataifa na wadau wake.
WFP
Wanawake mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini wakibeba chakula kilichowasilishwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Janga la uwajibikaji litachochewa na kukata ufadhili - Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amesema kukata ufadhili kwa mashirika yanayotoa huduma za kibinadamu kunasababisha janga la uwajibikaji.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na UNHCR, Bwana Grandi amesema kukata ufadhili kunaweka hatarini maisha ya mamilioni ya watu na madhara yake kwa watu wanaokimbia majanga, yatakuwa makubwa zaidi na yataonekana wazi.

Mathalani amesema wanawake na watoto wa kike wakimbizi walio hatarini zaidi kubakwa au aina nyingine ya ukatili tayari wanakosa huduma ambazo zilikuwa zinawahakikishia usalama.

Watoto wanasalia bila walimu shuleni, na hivyo wanatumbukia kwenye ajira za kutumikishwa, usafirishaji haramu au hata ndoa za mapema. “Kwa jamii za wakimbizi, suala la makazi litasalia kuwa ndoto, bila kusahau maji na chakula,” amesema Grandi.

Ameonya kuwa kupunguza usaidizi au ufadhili kutafanya dunia kuwa pahala pasipo salama zaidi na hivyo “kuchochea watu wengi wanaohaha kusaka maisha bora kuwa wakimbizi au kuendelea kuhama.”

Grandi amesema tayari UNHCR imesaka mbinu bunifu na fanisi za kutekeleza wajibu wake, na kutumia vema mchango unaotolewa ili kusaidia wale wanaokimbia hatari.

Wafanyakazi wa UNHCR wanasaidia wakimbizi wanaorejea na wakimbizi wa ndani katika vijiji vya Aleppo, Syria.
© UNHCR/Hameed Maarouf
Wafanyakazi wa UNHCR wanasaidia wakimbizi wanaorejea na wakimbizi wa ndani katika vijiji vya Aleppo, Syria.

Huu ni wakati wa ufadhili na si kurudi nyuma

“Zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wetu wako maeneo ya mstari wa mbele yenye majanga na mizozo wakisaidia jamii zilizodhurika.  Sisi na wadau wetu mwaka huu pekee tayari tumeshughulikia dharura 43. Sasa fedha zikiendelea kupungua, ina maana watendaji wachache, na uwepo mdogo wa UNHCR kwenye nchi zinazohifadhi wakimbizi, na hapo kanuni ni dhahiri: Watu watakufa.”

Ametanabaisha kuwa hilo sio tu ukata bali ni janga la uwajibikaji. Gharama ya kutochukua hatua itapimwa kwa machungu yatakayopatikana, ukosefu wa utulivu na mustakabali utakaopotea.

Grandi amesema azma yao ya kuendelea kusaidia watu wanaolazimika kukimbia makwao haijatetereka na kwamba iwapo wataendelea kupata msaada wataweza kubaini wale walio hatarini zaidi na kuwasaidia na sambamba na kuweka mbinu za kurejesha makwao kwa hiari na kiutu wale wanaotaka kurejea.

“Tunaomba nchi wanachama zitimize ahadi zao kwa wakimbizi. Sasa ni wakati wa mshikamano na si wakati wa kurudi nyuma.”