Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo langu ni kuona wasichana wadogo wanashiriki kwa wingi CSW - Zahra Salehe ICCAO

Zahra Salehe, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ICCAO la nchini Tanzania akihojiwa na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Flora Nducha jijini New York, Marekani (Machi 2025).
UN News
Zahra Salehe, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ICCAO la nchini Tanzania akihojiwa na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Flora Nducha jijini New York, Marekani (Machi 2025).

Lengo langu ni kuona wasichana wadogo wanashiriki kwa wingi CSW - Zahra Salehe ICCAO

Wanawake

Mwaka huu wa 2025, jumuiya ya kimataifa inaadhimisha miaka thelathini tangu Mkutano wa Nne wa Dunia kuhusu Wanawake na kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji (1995). 

Mkutano wa sitini na tisa cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake ulioanza tarehe 10 Machi 2025 unaendelea katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hadi 21 Machi 2025.

Wawakilishi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yaliyoidhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC kutoka kanda zote za dunia wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.

Miongoni mwa mashirika yaliyohudhuria mkutano huu muhimu ni ICCAO la nchini Tanzania likiwakilisha na Mkurugenzi Mtendaji wake, Zahra Salehe.

Zahra Salehe alipohudhuria mkutano wa mwaka jana aliona kuna jambo linahitaji kuboreshwa ili mikutano inayofuata iwe na tija zaidi kwa vizazi vya sasa na vya baadaye katika harakati za kumkomboa mwanamke.

Katika mahojiano haya na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Flora Nducha, Zahra Salehe anaeleza matamanio yake hayo na kwa namna ambayo ameanza kuyatekeleza katika mkutano wa mwaka huu.

Mjadala mkuu wa Mkutano wa sitini na tisa unahusu mapitio na tathmini ya utekelezaji wa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji, pamoja na matokeo ya kikao maalum cha 23 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mapitio haya yanahusisha tathmini ya changamoto za sasa zinazoathiri utekelezaji wa Jukwaa la Utekelezaji, kufanikisha usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake, na mchango wake katika kutimiza Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu kikamilifu.