Joto likizidi kuongezeka duniani, mwaka 2024 wathibitishwa kuwa ulikuwa wa joto zaidi
Joto likizidi kuongezeka duniani, mwaka 2024 wathibitishwa kuwa ulikuwa wa joto zaidi
Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu yameongezeka kwa viwango vya kutisha mwaka 2024, na baadhi ya athari hasi zinaweza kuwa zisizoweza kurekebishwa kwa karne nyingi – kama si milenia, imesema ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, (WMO).
Kubwa kabisa katika ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi ni kwamba mwaka 2024 ndio mwaka wenye joto zaidi tangu kumbukumbu zilipoanza miaka 175 iliyopita, na joto la wastani duniani likiwa nyuzi joto 1. 55 katika kipimo cha Selsiyasi, juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, ikivuka kwa mara ya kwanza kiwango kinachotakiwa kutovukwa cha nyuzijoto 1.5.
Ripoti inasema hili ni onyo linaloashiria umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Rekodi nyingi zimevunjwa kuanzia viwango vya hewa ya ukaa viko juu zaidi katika miaka 800,000, na kiwango cha maji ya bahari kinazidi kuwa cha juu kuliko kifani.
Zaidi ya hayo, vimbunga vya ukanda wa kitropiki, mafuriko, ukame, na hatari nyingine mwaka jana zilisababisha idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wapya kurekodiwa katika miaka 16, zikichangia kuzorota kwa uhaba wa chakula, na kuchochea hasara kubwa za kiuchumi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akinukuliwa kwenye taarifa hiyo anasema,licha ya mwenendo huu wa kutisha, malengo ya Mkataba wa Paris bado yanaweza kufikiwa na akawataka viongozi wa dunia kuongeza juhudi zao kujibu mgogoro unaoongezeka kwa kuelekea kwenye nishati mbadala.
Kwa Katibu Mkuu wa WMO Celeste Saulo, ripoti hii ni “wito wa kuamka kwani kiwango kinachoongezeka cha joto ni hatari inayokabili maisha ya binadamu, uchumi na sayari.