Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya mtoto wa kike ni moja ya nguzo muhimu katika jamii

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi ya wasichana ya Shofco, Kibera nchini Kenya wakizungumza na mwalimu wao.
UN News/Thelma Mwadzaya
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi ya wasichana ya Shofco, Kibera nchini Kenya wakizungumza na mwalimu wao.

Elimu ya mtoto wa kike ni moja ya nguzo muhimu katika jamii

Utamaduni na Elimu

Elimu ya mtoto wa kike ni moja ya nguzo muhimu katika jamii ukizingatia malengo endelevu ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa.Wakati ulimwengu unaadhimisha miaka 30 tangu Azimio la Beijing na Jukwaa la Hatua za Utekelezaji kuwekwa bayana, serikali zimetangaza nia ya kisiasa ya kuheshimu, kudumisha haki, usawa na wanawake na wasichana kuwezeshwa.

Shule hii ya msingi ya wasichana ya Shofco iliyoko mtaani Kibera jijini Nairobi hapa Kenya, ni mfano wa kuigwa kwani watoto hawa wanasoma bila malipo na wafadhili wanahakikisha hakuna anayeachwa nyuma. Anne Mumbe ni Mwalimu Mwandamizi katika shule hii ya wasichana ya Shofco na anasisitizia kuwa ni muhimu wa wanafunzi kusalia darasani kwani,” Tunapata watoto ambao wanatoka kwenye familia ambazo hazijiwezi.Kwahivyo utapata hawalipi karo wanafanya kusaidiwa na SHOFCO na pia wanapokea mahitaji mengine yote ndio waendelee na masomo yao,”anaelezea.

Ofisi ya wakfu wa CIFF wa kutetea haki za watoto unaowekeza kwenye miradi ya kumnyanyua mwanamke, iliyoko huko Kibera nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Ofisi ya wakfu wa CIFF wa kutetea haki za watoto unaowekeza kwenye miradi ya kumnyanyua mwanamke, iliyoko huko Kibera nchini Kenya.

Viashiria vya UNDP vya unyonge

Ili kuwapa wanaostahili nafasi hii ya kusoma kwenye hii, waratibu wanatumia vigezo vya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP, vya kukadiria uhitaji. Angela Ngetich anayesimamia ushirikiano kati ya wafadhili wa wakfu wa haki za watoto CIFF anaelezea kwamba, "Kwenye mitaa ya mabanda, kuna watoto walio wanyonge kuliko wenzawao….viwango vinatofautiana.Viashiria vya unyonge vinatusaidia kuwatambua wale ambao wanahitaji zaidi usaidizi. Pia kuna mtandao wa mijini wa SHOFCO ambao wanafahamu na kumjua kila mtoto ambaye anahitaji msaada na kwa kiasi gani.Kwahiyo njia hiyo pia inatusaidia kuwajua wanaohitaji usaidizi.” anamalizia.

Wakfu wa haki za watoto wa CIFF ulio na miradi kwenye nchi 29 barani Afrika, unafadhili miradi ya elimu, maji safi na kilimo. Kwa Kenya, CIFF, inafadhili baadhi ya wasichana wanafunzi katika shule hii ya msingi ya wasichana ya Shofco iliyoko Kibera jijini Nairobi. Faustina FYNN Nyame ni Mkurugenzi Mtendaji wa wakfu wa haki za watoto wa CIFF na anasisitiza kuwa wakati wa kumnyanyua mtoto wa kike ni sasa kwavile,”Kuna mataifa mengi yanataka kutetea hili…..wanataka kuwa watetezi wa Afrika watakaotokomeza tamaduni potofu barani mwetu….na kuhakikisha wanawake na wasichana wanachukua nafasi yao kwenye bara letu na kutimiza malengo na maono yao. La msingi ni kutokomeza na kuupiga vita umasikini.Tukiwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika jamii yetu….uchumi wetu…. Kwa njia ya manufaa zaidi tunakuwa na mataifa imara zaidi na hilo ndilo tulitakalo barani Afrika."

Bi. Nyame wa CIFF ameratibiwa kuzungumzia suala la kuwekeza katika elimu ya wasichana wa kiafrika katika mazingira ya bora kwenye mkutano wa 69 wa Hali ya Wanawake duniani, CSW69 linalofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Mtaa wa mabanda wa Kibera, Nairobi Kenya iliko shule ya wasichana ya Shofco.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mtaa wa mabanda wa Kibera, Nairobi Kenya iliko shule ya wasichana ya Shofco.

SDGs za kutokomeza njaa, umasikini na elimu

Wasichana hawa wanapata elimu pasina malipo na pia mlo wa mchana kwa hisani ya wafadhili kama CIFF ili wasitatizike na kuacha shule. Leah Njeri ni mwalimu wa lugha katika shule ya Shofco na anaamini bila wafadhili mambo yasingetengemaa, ”Wazazi wa hapa ni wengi ni wale ambao wana uhaba wa hela.Kwahiyo watoto hawa wanapokuja shuleni wafadhili huwasaidia kwani wanapata chakula cha kufungua kinywa na cha mchana.Pia wanapewa kila wanachohitaji katika masomo yao kwa mfano hawanunui vitabu vya kusoma, kuandikia, sare na kila kitu wanapewa hapa shuleni.”

Wakfu wa CIFF wa haki za watoto uko mstari wa mbele kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa mataifa, SDGs ya kutokomeza njaa na umasikini kadhalika elimu na usawa kwa wote. Redemta Kinyaka ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasichana ya Shofco na anaamini wako kwenye mkondo sawa.

Maono na ndoto za maisha

Dhamira ya miradi ya kuwanyanyua watoto wa kike kwa kusalia shuleni ni kuwapa sauti na silaha za kupambana na maisha katika siku za usoni kwa manufaa ya jamii. Wasichana wenyewe wana matarajio yapi? Michelle Awuor ni mwanafunzi wa darasa la 9 na angependa kuwa mhadhiri atakapohitimu kwani,” Napenda kuwafundisha watu wanaojielewa na kutaka wanachokijua.Nikimalia shule ningependa kuwa mhadhiri na wazazi wananiunga mkono kuitimiza ndoto hiyo.”

Brenda Awuor ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya wasichana ya Shofco huko Kibera na msemaji wa wanafunzi anatazamia kuwa muandishi wa habari kwani, "Napenda kujifunza mengi tofauti na pia kuwafahamisha watu kinachoendelea.Uandishi ni tasnia ya kuvutia kwani napenda sana kuwa mstari wa mbele na kufahamu kinachoendelea kote ulimwenguni.Wazazi wanafarijika sana wakiona niko shule na nimetulia kwani walitatizika kulipa karo ila kwa sasa wamepumzika.”

Mipango hii ni baadhi ya mbinu za utekelezaji wa harakati na hatua za kudumisha Azimio la Beijing la haki za wanawake lilnalotimiza miaka 30 na ajenda ya kuimarisha hali ya wasichana.