Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la Beijing limeleta manufaa kwa wanawake Côte d'Ivoire - Mwanasheria Francine

Francine Aka Epse Akaanghui, Rais wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini Cote d'Ivoire, akizungumza na kundi la wanawake katika tukio la nje.
UN News/Selina Jerobon Francine Aka Epse Akaanghui (mbele) Rais wa Chama cha wanasheria wanawake nchini Côte d'Ivoire huko Afrika Magharibi akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Azimio la Beijing limeleta manufaa kwa wanawake Côte d'Ivoire - Mwanasheria Francine

Wanawake

Kutana na Francine Aka Epse Akaanghui  Rais wa Chama cha wanasheria wanawake nchini Côte d'Ivoire huko Afrika Magharibi. Yeye anashiriki mkutano wa 69 wa Hali ya Wanawake duniani, CSW69 akisema taifa lake lina mengi ya kujivunia wakati huu wa kuadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji.

"Côte d'Ivoire ni bingwa kwenye masuala ya sheria, kwa sababu tangu Beijing, tumepitisha nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kumlinda mwanamke. Mathalani kwenye elimu. Hivi sasa elimu ni lazima kwa mtoto wa kike na wa kiume, » amesema huku akiongeza kuwa « pia masuala ya ukatili wa kijinsia. Tuna sheria inayolinda wanawake ambayo inawezesha wanawake kukemea na kuchukulia hatua wanaotekeleza ukatili."

Wagombea wa chaguzi asilimia 30 ni wanawake

Katika nyanja ya kisiasa hivi sasa asilimia 30 ya wagombea wa chaguzi ni wanawake. Na leo, katika ndoa, mume si mkuu wa familia tena. Ni usimamizi wa wanandoa wote wawili. Ni wazazi wote wawili walio na mamlaka juu ya watoto. Kweli, haya ni mifano ya kuwaonyesha kwamba tumetumia sheria zote zinazohitajika ili kumlinda mwanamke.

Hilo la usawa kwenye ndoa, alipoulizwa iwapo linatekelezeka, Bi. Aka Epse Akaanghui akasisitiza kuwa « kweli kabisa kuna usawa katika ndoa. Leo, hakuna tena mkuu wa familia. Mume na mke wako katika kiwango sawa, wanachukua maamuzi pamoja, iwe kuhusu mali yao au watoto wao.”

Francine Aka Epse Akaanghui, Rais wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini Côte d'Ivoire, akipiga picha na wanawake wengine wawili katika tukio la CSW69 Afrika Magharibi.
UN News/Selina Jerobon Francine Aka Epse Akaanghui (mbele) Rais wa Chama cha wanasheria wanawake nchini Côte d'Ivoire huko Afrika Magharibi akiwa na wanawake wenzake.

Umri wa kuolewa ni miaka 18 lakini bado kuna changamoto

Umri wa kuolewa ni miaka 18. Yaani 18 kwa mtoto wa kike au wa kiume bila ya ridhaa ya wazazi.  Kimsingi, hata kwa ndoa za kidini. Lakini kiukweli katika utekelezaji bado kuna ndoa za utotoni, lakini kisheria hilo hairuhusiwi.

Pamoja na changamoto hiyo ya ndoa za utotoni licha ya sheria kuweko, Rais huyu wa Chama cha Wanawake Wanasheria nchini  Côte d'Ivoire, akataja changamoto nyingine anayoona kubwa zaidi kuwa ni « uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi. Hakuna wanawake wa kutosha katika nyadhifa za kuchaguliwa ndani ya Bunge. Wabunge wa kike bado ni wachache, na hakuna wanawake wa kutosha katika nafasi za uongozi wa juu. »

Kuhusu jambo ambalo anajivunia na yuko tayari kuwajulisha washiriki wengine CSW69 amesema ni hatua dhidi ya ukatili.

“ Kidogo! Naweza kusema suala la unyanyasaji. Siku hizi kuna adhabu katika sheria za kazi au sheria ya makosa ya jinai. Yaani, ikiwa wewe ni mwathiriwa wa unyanyasaji wa kingono au wa kisaikolojia kazini, unaweza kufungua mashtaka dhidi ya mwajiri wako au kumpeleka kwenye mahakama ya jinai, na atahukumiwa.”

Sheria zimeanza kufanya kazi

Ametolea mfano kwamba ,“hivi karibuni tumepata hukumu kubwa katika nchi yetu. Wiki chache zilizopita, nilimtetea msichana mmoja mwanamichezo wa Taekwondo aliyefungua mashtaka dhidi ya kocha wake kwa unyanyasaji wa kingono, na kocha huyo alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani.”

Maoni yake baada ya kupitishwa kwa Azimio la Kisiasa CSW69

Katika siku ya kwanza ya CSW69 Mawaziri walipitisha Azimio la Kisiasa kuhusu miaka 30 ya Mkutano wa Beijing na Jukwaa la Utekelezaji. Bi. Aka Epse Akaanghui akasema, “tunaona kwamba aina hii ya azimio inatusaidia. Ni kama ramani ya njia. Mnaona, nilieleza kwamba tumepitisha sheria zote kwa sababu tumefuata Azimio la Beijing, mapendekezo kumi na mawili ya mada tuliyafuata."

Amesisitiza kuwa Kila kitu si kamili, kila kitu si timilifu, lakini hii inawezesha serikali kuwa na mwongozo wa kufuata, kufahamu wapi pa kuelekea ili kulinda na kuboresha haki za wanawake. "Kwa hivyo, ni jambo zuri sana, lakini bado kuna changamoto nyingi."