Guterres afuturu na wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh
Guterres afuturu na wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh
Leo Ijumaa ikiwa ni siku ya 11 ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefuturu na wakimbizi wa Rohingya walioko kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Cox Baazar nchini Bangladesh kuonesha mshikamano na wakimbizi na wenyeji wanaowahifadhi.
Katika futari hiyo ambayo ameambatana na Mshauri Mkuu wa serikali ya Bangadesh Muhammad Yunus, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameanza kwa kuwaambia wakimbizi aliokutana nao akisema, “nimefika Cox’s Bazar katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa dhamira ya mshikamano.”
Guterres amepongeza uimara wa watu wa Rohingya, waliokimbia Myanmar baada ya miongo ya mateso na akaongelea haki yao ya kurejea kwa usalama na hiari, lakini akathibitisha kuwa hali ya nchini mwao Myanmar bado ni mbaya.
Akionya kuhusu upungufu mkubwa wa ufadhili, Guterres amesema, “tunakabiliwa na hatari kubwa ya kuwa na asilimia 40 pekee ya rasilimali zilizopatikana mwaka 2024 kwa ajili ya mwaka 2025. Hili litakuwa janga kubwa. Watu wataumia na wengine watapoteza maisha.”
Pia Katibu Mkuu amesifu ukarimu wa Bangladesh katika kuwahifadhi wakimbizi, lakini akasema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula, na kuongezeka kwa hali ya ukosefu wa usalama zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.
Aidha Guterres akigusia Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Hofu Dhidi ya Uislamu ambayo huadhimishwa kila tarehe 15 ya mwezi Machi ambayo ni kesho ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushikamana na kuongeza msaada ili kuhakikisha wakimbizi wa Rohingya hawasahauliki. “Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, naiomba jumuiya ya kimataifa ioneshe mshikamano huo kwa vitendo.” amesema.
Umoja wa Mataifa unaendelea kushinikiza suluhisho la kudumu kurejesha hali salama Myanmar ili wakimbizi wa Rohingya waweze kurudi nyumbani. Hadi wakati huo, Guterres amesisitiza kuwa msaada wa kibinadamu ni wa dharura na hauwezi kusubiri.