Kizazi cha watoto wa Sudan chawekwa rehani na njaa na mgogoro unaoendelea: UNICEF
Kizazi cha watoto wa Sudan chawekwa rehani na njaa na mgogoro unaoendelea: UNICEF
Mamilioni ya watoto nchini Sudan wanakabiliwa na moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani, ameonya leo Mkurugenzi wa Mipango ya Dharura wa Shrika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Lucia Elmi katika taarifa yake kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi. Amesema “Mgogoro wa vita, ufurushwaji wa watu, na njaa vinaweka kizazi kizima hatarini, huku watoto zaidi ya milioni 16 wakihitaji msaada wa haraka.”
Kwa mujibu wa UNICEF mgogoro huu umesababisha watoto karibu milioni 17 kuwa nje ya shule kwa miaka miwili, na kuwafanya kuwa katika hatari ya kutekwa, ndoa za shuruti, na ukatili wa kijinsia.
Ripoti zinaonyesha kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto kila siku, ikiwa ni pamoja na kuingizwa katika makundi ya waasi, ajira kwa watoto, na msongo mkubwa wa mawazo.
"Kuwafikia watoto hawa kunazidi kuwa vigumu," amesema Elmi, akihimiza hatua za haraka kuwalinda walio hatarini zaidi.
Uhaba wa chakula na changamoto za kibinadamu vyaongezeka
Hali nchini Sudan imezorota kwa kasi, huku baa la njaa likizidi kuenea katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kambi za wakimbizi wa ndani huko Darfur Kaskazini na milima ya Nuba Magharibi limesema shirika la UNICEF.
Tangu Aprili 2023, idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula imeongezeka mara tatu.
UNICEF inakadiria kuwa watoto milioni 3.2 walio chini ya umri wa miaka mitano watapata utapiamlo mkali mwaka huu, huku 770,000 wakihatarishwa na unyafuzi hali inayoweza kusababisha vifo kwa urahisi.
Mbali na uhaba wa chakula, huduma muhimu kama vile afya, maji safi, na usafi wa mazingira zimeporomoka katika maeneo yaliyoathirika zaidi na njaa, na hivyo kuongeza vifo vya watoto.
Elmi ameonya kwamba "Bila maji safi, usafi wa mazingira, na huduma za afya, watoto hawataweza kuishi".
Hata hivyo, amesisitiza kuwa vikwazo vya kiutawala na vita vinavyoendelea vinazuia juhudi za kibinadamu, na kufanya iwe vigumu kwa mashirika ya misaada kuwafikia wanaohitaji msaada huo.
Matumaini katikati ya mgogoro
Licha ya changamoto nyingi, UNICEF imeshuhudia mnepo wa ajabu miongoni mwa jamii zilizofurushwa na zile zinazowahifadhi.
Elmi ameelezea jinsi alivyotembelea vituo vya kujifunza vya muda ambapo watoto wengi wao wakiwa wanahudhuria shule kwa mara ya kwanza, wana shauku ya kujifunza na kupata utulivu.
Shule hizi za muda siyo tu zinatoa elimu, bali pia hutoa usalama, matumaini, na utulivu wakati wa machafuko. amesema
Familia pia zimeanza kurejea nyumbani kwa tahadhari katika maeneo ambapo mapigano yamepungua, kama vile Seenja, Sennar, na Wad Madani.
Hata hivyo, UNICEF imesema wengi wao bado wako katika kambi za wakimbizi wa ndani, wasiweze kurudi kwa sababu vijiji vyao vimeharibiwa kabisa. Elmi ameongeza kuwa “Wamekwama bila matumaini ya mustakbali wao,"
Jitihada za UNICEF na wito wa hatua za dharura
Licha ya changamoto kubwa, UNICEF inaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha nchini Sudan.
Mwaka 2024 pekee, shirika hilo limeweza kuwafikia:
- Watoto na walezi milioni 2.7 kwa msaada wa kisaikolojia, elimu, na huduma za ulinzi.
- Watu milioni 9.8 kwa maji safi ya kunywa.
- Watoto milioni 6.7 kwa uchunguzi wa utapiamlo, huku 422,000 wakipatiwa matibabu ya dharura.
Katika mwaka wa 2025, UNICEF inalenga sio tu kuendelea na misaada ya dharura, bali pia kurejesha huduma muhimu na kujenga mnepo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Hata hivyo, UNICEF imesema vikwazo vikubwa bado vipo, na uingiliaji kati wa haraka wa kimataifa unahitajika.
Wito wa hatua kuwalinda watoto wa Sudan
UNICEF imetoa wito wa kimataifa kwa serikali, wafadhili, na pande zinazohusika na mgogoro nchini Sudan, ikiwahimiza,
- Kutoa hakikisho la upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo yenye mgogoro.
- Kulinda wafanyakazi wa misaada na vifaa vya misaada.
- Kuongeza ufadhili ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
- Kusitisha ghasia mara moja.