Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNICEF asema watoto Sudan wanabeba machungu yasiyoelezeka

Watoto wawili waliofurushwa na mapigano katika jimbo la Al Jazirah wamepumzika katika eneo la mapokezi kusini mashariki mwa Sudan.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdeen
Watoto wawili waliofurushwa na mapigano katika jimbo la Al Jazirah wamepumzika katika eneo la mapokezi kusini mashariki mwa Sudan.

Mkuu wa UNICEF asema watoto Sudan wanabeba machungu yasiyoelezeka

Amani na Usalama

Sudan sasa ndiyo janga kubwa zaidi la kibinadamu na linalosababisha uharibifu mkubwa zaidi duniani, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Catherine Russel wakati huu ambapo vita nchini Sudan inaingia mwaka wa pili tangu ianze.

Akihutubia Baraza la Usalama jijini New York, Marekani hii leo, Bi. Russell amesema tangu kuanza kwa mapigano kati ya jeshi la serikali ya Sudan, SAF na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, zaidi ya watu milioni 30 – zaidi ya nusu wakiwa watoto – wanaishi katika mazingira ya ukatili mkubwa, njaa, na magonjwa hatari.

"Hili siyo tu janga, bali ni janga lenye changamoto nyingi linaloathiri kila sekta, kutoka afya na lishe hadi maji, elimu na ulinzi," amesema Bi. Russell.

Tangu vita vilipozuka Aprili 2023 makumi ya maelfu ya raia wameuawa na zaidi ya milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao, takriban milioni 3.5 wakiwa wakimbizi katika nchi jirani.

Ardhi yenye rutuba imeharibiwa vibaya, baa la njaa imetangazwa katika maeneo kadhaa, na miundombinu muhimu – ikiwemo hospitali – imeharibiwa au kutelekezwa kutokana na mapigano.

Ukatili wa kijinsia unatumika kama silaha ya vita nchini Sudan.
© UNICEF/Tess Ingram
Ukatili wa kijinsia unatumika kama silaha ya vita nchini Sudan.

Wanawake, wanaume, wavulana, wasichana wanabakwa

Watoto ndio waathirika wakubwa wa ghasia hizi. UNICEF imepokea ripoti za kutisha kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto, ikiwa ni pamoja na mauaji, ukatili wa kingono, na kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha.

Kati ya Juni na Desemba mwaka 2024 pekee, zaidi ya matukio 900 ya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto yamerekodiwa, ambapo asilimia 80 vilihusisha mauaji au ulemavu wa kudumu.

"Watoto nchini Sudan wanapitia mateso yasiyoelezeka na ghasia za kutisha. Mara ya mwisho nilipokuwa Sudan, nilikutana na familia na watoto wanaoishi katika jinamizi hili. Hadithi zao zinasikitisha mno – na zinahitaji hatua za haraka," amesema Bi. Russell.

Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, akihutubia Baraza la Usalama.
UN Photo/Manuel Elías
Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, akihutubia Baraza la Usalama.

Amesimulia ushuhuda wa kushtua kuhusu ubakaji, akionya kuwa inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 12.1 – na hata wanaume na wavulana kwa kiwango kinachoongezeka – wako hatarini kufanyiwa ukatili wa kingono, ongezeko la asilimia 80 kutoka mwaka uliopita.

"Takwimu hizi zinatupa taswira ndogo tu ya kile ambacho tunajua kuwa ni janga kubwa zaidi na lenye uharibifu mkubwa."

Vizuizi vya misaada

Licha ya mahitaji makubwa, mashirika ya misaada ya kibinadamu yanakabiliwa na changamoto kubwa katika kuwafikia wahitaji.

Vikwazo vya kiutawala na urasimu, pamoja na maeneo ya mapigano yanayobadilika mara kwa mara, vimefanya ufikishaji wa misaada kuwa mgumu. Wahudumu wa misaada wanazidi kuwa wahanga wa unyang’anyi, mashambulizi, na hata kuuawa.

Zaidi ya watoto 770,000 wanatarajiwa kuathirika na utapiamlo mkali mwaka huu, wengi wao wakiwa katika maeneo yasiyofikika na misaada ya kibinadamu.

"Bila msaada wa dharura wa kuokoa maisha, wengi wa watoto hawa watakufa," amesisitiza Bi. Russell. Amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushinikiza pande zote kuruhusu upatikanaji wa misaada bila vizuizi, hasa kupitia mipaka muhimu.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakutana kujadili Sudan.
UN Photo/Manuel Elías
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakutana kujadili Sudan.

Hatua za haraka zahitajika

Bi. Russell amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza uharaka wa kuchukua hatua za kimataifa.

Ameitaka jamii ya kimataifa kuhakikisha ulinzi wa watoto na miundombinu muhimu wanayohitaji ili kuendelea kuishi, pamoja na kuwawajibisha wanaohusika na ukiukwaji wa haki, hususan ukatili wa kingono.

Pia amelitaka Baraza la Usalama kusaidia kufanikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila ucheleweshaji wowote na kusitisha msaada wa kijeshi kwa pande zinazopigana.

Mkuu huyo wa UNICEF amesisitiza hitaji la ufadhili wa ziada, akibainisha kuwa UNICEF pekee inahitaji dola bilioni 1 ili kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watoto milioni 8.7 walio hatarini.

"Bila hatua hizi za haraka, janga hili litaendelea kuangamiza jamii ya Sudan na mateso yataongezeka kwa kiwango cha kutisha, hali ambayo italeta maafa kwa kizazi kizima na kuhatarisha mustakabali wa Sudan, ukanda wa Afrika, na zaidi."

Christopher Lockyear, Katibu Mkuu wa shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) au  Madaktari Wasio na Mipaka) akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Sudan.
UN Photo/Manuel Elías
Christopher Lockyear, Katibu Mkuu wa shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) au Madaktari Wasio na Mipaka) akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Sudan.

Ukosefu wa utu katika hospitali ya MSF

Katika kikao hicho, Christopher Lockyear, Katibu Mkuu wa shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) au  Madaktari Wasio na Mipaka), alielezea alichoona wakati wa ziara yake Sudan.

Huko Khartoum, alishuhudia matokeo ya shambulio la RSF kwenye Soko la Sabreen, Omdurman. Hospitali ya Al-Nao inayosaidiwa na MSF, moja ya hospitali chache zinazofanya kazi katika eneo hilo, ilijaa wagonjwa waliopata majeraha makubwa.

"Hospitali ilikuwa uwanja wa mauaji yasiyoelezeka: mawimbi ya wagonjwa waliopata majeraha mabaya yalijaza kila pembe ya chumba cha dharura," amesema.

"Nimeshuhudia maisha ya wanaume, wanawake, na watoto yakiharibiwa mbele ya macho yangu," ameongeza, akieleza kuwa katika wiki hiyo hiyo, vikosi vya SAF vilishambulia kiwanda cha mafuta ya karanga na maeneo ya raia huko Nyala, Darfur Kusini, hali iliyosababisha hospitali inayosaidiwa na MSF kuzidiwa na wagonjwa.

Mashambulizi haya ni mifano michache tu ya jinsi vita hivi "visivyo na huruma" vinavyoendelea.

Mwanamke akipika kando ya makazi yake katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika jimbo la Kassala, Sudan.
© UNICEF/Proscovia Nakibuuka
Mwanamke akipika kando ya makazi yake katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika jimbo la Kassala, Sudan.

Mwitikio wa haraka na endelevu wahitajika

Bwana Lockyear ametumia hotuba yake kuomba wanachama wa Baraza la Usalama kutoa mwitikio wa haraka na endelevu kwa janga hili, akisisitiza kuwa mfumo wa misaada ya kibinadamu Sudan umesimama kwa sababu ya vikwazo vya kiserikali, ukosefu wa usalama, na vikwazo vya kisiasa.

Amesisitiza umuhimu wa "mkataba mpya wa kibinadamu" kwa Sudan ambao utahakikisha ulinzi wa raia, kutoa nafasi kwa wahudumu wa misaada kufanya kazi bila vikwazo, na kulazimisha pande zinazopigana kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu – yote yakiwa na msingi wa uwajibikaji thabiti.

"Hata hivyo, hata makubaliano yenye nguvu zaidi hayatafanikiwa bila ufadhili wa kutosha kutoka kwa wahisani na msukumo mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa," amesema.

"Kwa nchi wanachama: mwitikio huu lazima uongezwe kwa ufadhili endelevu na wa kutosha. Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa: urejeshaji kamili wa mashirika ya kibinadamu ya UN unapaswa kuidhinishwa katika Darfur na Sudan nzima."