Miaka 14 ya Mgogoro wa Syria: Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa haki na maridhiano
Miaka 14 ya Mgogoro wa Syria: Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa haki na maridhiano
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika kumbukumbu ya miaka 14 ya mgogoro wa Syria ametoa wito wa haki, maridhiano, na kukomesha ghasia zinazoendelea.
Kupitia katika taarifa iliyosambazwa na Ofisi ya msemaji wake leo Machi 13 jijini New York, Marekani, akitafakari kuhusu mateso makubwa ambayo watu wa Syria wamepitia, Guterres amesisitiza madhara makubwa ya vita hivyo, ambavyo vimesababisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao na vifo vya mamia ya maelfu ya watu.
"Kile kilichoanza kama mwito wa mabadiliko ya amani kiligeuka kuwa moja ya migogoro mibaya zaidi duniani, ikiwa na gharama kubwa kwa binadamu," amesema Guterres akilaani ukandamizaji mkali uliofuata maandamano ya amani mnamo mwaka 2011, ambayo yalisababisha vita vikali vilivyojumuisha matumizi ya silaha za kemikali, mabomu ya kiholela, na njaa kwa jamii nzima kupitia mzingiro wa muda mrefu.
Licha ya changamoto hizo, Katibu Mkuu amesifu ustahimilivu na uthabiti wa watu wa Syria katika harakati zao za kutafuta uhuru, heshima, na haki. Pia ametambua matumaini mapya tangu Desemba 8 kwamba Syria inaweza kuchukua njia tofauti kuelekea amani na ujenzi wa taifa.
Hakuna kinachoweza kuhalalisha mauaji ya raia
Hata hivyo, Guterres ameonya kuwa ripoti za hivi karibuni kuhusu ghasia zinazoendelea dhidi ya raia zinatishia matumaini haya dhaifu. Amesisitiza kuwa "hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mauaji ya raia" na akatoa wito wa "uchunguzi wa kuaminika, huru, na usio na upendeleo" kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu. Amesema wale waliohusika lazima wawajibishwe.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa pia amewataka viongozi wa mpito wa Syria kutimiza ahadi zao za kujenga taifa jipya na jumuishi ambapo raia wote bila kujali kabila, dini, mwelekeo wa kisiasa, au jinsi wanaweza kuishi kwa usalama na heshima. "Sasa ni wakati wa kuchukua hatua. Hatua thabiti na za haraka zinahitajika," amesema.
Umoja wa Mataifa uko na Wasyria
Akithibitisha msaada wa Umoja wa Mataifa kwa watu wa Syria, Guterres ameahidi kujitolea kwa shirika hilo kusaidia katika mpito wa kisiasa wa kujumuisha wote. Amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na uponyaji wa kitaifa kama hatua muhimu kuelekea urejeshaji wa muda mrefu wa Syria na kuingizwa kwake tena katika jumuiya ya kimataifa.
"Tunasimama na watu wa Syria kuelekea ahadi ya Syria bora kwa Wasyria wote," amehitimisha Guterres, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi zinazohakikisha mustakabali uliojengwa juu ya heshima, utawala wa sheria, na ushirikishwaji wa wote.
Taarifa hii inakuja wakati ambapo Syria bado inakabiliwa na hali ya kutoelewana kisiasa, matatizo ya kiuchumi, na migogoro ya kibinadamu inayoendelea. Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, jumuiya ya kimataifa inafuatilia kwa makini maendeleo katika taifa hilo lililokumbwa na vita, ikitumaini kwamba amani hatimaye itachukua nafasi ya miaka ya uharibifu.