Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yakabidhi magari sita kwa serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki DRC

MONUSCO yakabidhi magari sita kwa serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki.
MONUSCO
MONUSCO yakabidhi magari sita kwa serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki.

MONUSCO yakabidhi magari sita kwa serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki DRC

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa unaendelea kumuunga mkono mshirika wake, serikali ya Jamuhuri ya Kidemokratia ya Kongo, katika kuwalinda raia. Ni kwa ajili hiyo ambapo Umoja wa Mataifa, kupitia ujumbe wake wa kulinda amani nchini DRC (MONUSCO), ulitoa magari sita kwa serikali ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi siku ya Alhamisi, Machi 13, 2025, ili kuwezesha uingiliaji wa haraka wa maafisa wa polisi ili kulinda raia. 

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hii leo, ujumbe wa Umoja wa MAtaifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umekabidhi magari 6 kwa polisi wa kitaifa mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini, lengo likiwa ni kuimarisha doria za usalama na ulinzi wa raia wakati huu ambapo mji huo umechukuwa jukumu la mji mkuu baada ya Goma kutwaliwa na waasi wa M23.

Abdourahmane Ganda, Mkuu wa ofisi ya MONUSCO mjini Beni ndiye aliyekabidhi magari hayo kwa Gavana wa Kivu Kaskazini Meja Jenerali Kakule Somo Evariste.

Akizungumza baada ya kukabidhi magari hayo aina ya Toyota Landcruiser, Bwana Ganda amesema magari mawili ni kwa ajili ya kituo cha polisi cha eneo la Lubero, mawili ya mji wa kibiashara wa Butembo na mengine mawili ya Oicha.

“Mtakumbuka kuwa tarehe 31 Disemba, 2024 tulikabidhi magari matano kwa ajili ya mji wa Beni, na katika tukio hilo hilo tuliahidi kuwa tutapatia magari mengine na ndio tumekabidhi leo,” amesema Ganda.

Meja Jenerali Kakule kwa upande wake amesisitiza kuwa magari hayo yatasaidia sana polisi kuhamishia kazi zao kwenye mji huo mkuu sasa wa jimbo la Kivu Kaskazini ili kulinda idadi ya watu na mali zao na kwamba “msaada huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali ya Jimbo na MONUSCO ".

Ameeleza kuwa “hi si mara ya kwanza kwa MONUSCO kutusaidia, kama ulivyosema, kwa polisi wetu. Katika suala la michango, na kujengea uwezo. Nina hakika kwamba kwa mwelekeo huu wa usaidizi unaoongezeka, uanzishwaji wa makao makuu ya kikosi cha MONUSCO hapa Beni utaendelea kuimarisha usalama. Na haya magari nitakabidhi kwa kamanda wa polisi wa jimbo la Kivu Kaskazini kwa maelekezo madhubuti ya kuyatumia vyema.”