Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni ‘mtikisiko mkubwa’ ufadhili wa misaada unapoakauka – Mkuu wa misaada ya UN

Tom Fletcher, Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu, akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Makao Makuu UN jijini New York.
UN Photo/Evan Schneider Tom Fletcher, Naibu Katibu Mkuu wa UN katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura (UNOCHA), akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika Makao Makuu ya UN.

Ni ‘mtikisiko mkubwa’ ufadhili wa misaada unapoakauka – Mkuu wa misaada ya UN

Msaada wa Kibinadamu

Tom Fletcher, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya Dharura(OCHA) amesema, “kasi na kiwango cha kupunguzwa kwa ufadhili ambacho tumekumbana nacho ni, bila shaka, mshtuko mkubwa” kwa sekta ya misaada ya kibinadamu.

Akihutubia wanahabari leo (12 Machi) jijini New York, Marekani, Fletcher amesema, “tayari tulikuwa na mzigo mkubwa, tukiwa na rasilimali chache, na tukishambuliwa moja kwa moja—mwaka jana ulikuwa mwaka hatari zaidi kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kuwahi kurekodiwa. Lakini bila shaka, ni ngumu zaidi kwa watu tunaowahudumia. Zaidi ya watu milioni 300 kwa sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu.”
 

Wengi watakufa

 
Amesisitiza, “wengi watakufa kwa sababu misaada hiyo inakauka. Na katika jumuiya ya misaada ya kibinadamu, programu zinakatizwa hivi sasa. Wafanyakazi wanapunguzwa kazi; nadhani asilimia 10 ya wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, NGO walifutwa kazi mnamo Februari. Na katika familia ya Umoja wa Mataifa na washirika wetu, tunafanya maamuzi magumu kila siku kuhusu ni maisha gani tunayopaswa kuyapa kipaumbele, ni maisha yapi tunayojaribu kuyaokoa. Kwa hivyo, nadhani kipindi kijacho—hasa katika wiki zijazo—kitafafanua jinsi tutakavyotoka kwenye changamoto hii kubwa kama harakati ya kibinadamu.”
 
Amesema, “mwisho wa wiki hii, Ijumaa, nitapokea mipango ya kina kutoka kwa waratibu wetu wa misaada ya kibinadamu. Maafisa wakuu wa misaada katika kila nchi yenye mgogoro, wakiongozwa na timu zao za misaada ya kibinadamu katika mashirika na NGO, watakuwa wameandaa mikakati ya jinsi watakavyobadilisha mbinu zao kukabiliana na changamoto hii mpya.”
 
Ameendelewa akisema, “lakini nyuma ya juhudi hizo za kujipanga upya, tutapaswa pia kufanya upya yale tunayoyafanya. Tutapaswa kujenga hoja mpya, kushirikiana na washirika wapya kwa kazi yetu. Tutahitaji kupata vyanzo vipya vya ufadhili.
 
Tutapaswa kupambana. Tutahitaji kufikiria upya jinsi tunavyofanya kazi—na hili ni jambo muhimu kusema, lakini gumu kutekeleza—tutapaswa kuhamisha mamlaka kwa viongozi wetu wa kibinadamu walioko mashinani na kwa watu tunaowahudumia, jamii tunazofanya nazo kazi katika mstari wa mbele wa mgogoro wa kibinadamu.”
 
Fletcher ameendelea kueleza akisema, “tunahitaji muongo wa misaada ya kibinadamu, ambapo tutalazimika kushinda hoja kwa upya kuhusu umuhimu wa misaada ya kibinadamu na mshikamano wa kimataifa. Hili ni jambo ambalo naamini ni kubwa kuliko mabadiliko ya mwaka hadi mwaka na mabadiliko ya kisiasa.”
 

Kuhusu ufadhili wa Marekani

 
Amesisitiza, “tumekuwa tukitegemea sana ufadhili kutoka Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Karibu nusu ya maombi yetu ya msaada yamefadhiliwa na walipa kodi wa Marekani. Ni muhimu kutambua kwamba hatupaswi kamwe kuchukulia hilo kama jambo la kawaida, hasa katika kipindi cha changamoto za kiuchumi na wakati ambapo serikali nyingi zinajiondoa katika masuala ya kimataifa.”
 
Akijibu swali, amesema, “siwezi kutoa idadi kamili ya athari za kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani, lakini ninachoweza kusema ni kwamba kwa miaka na miongo kadhaa sasa, Marekani imekuwa nguvu kubwa ya misaada ya kibinadamu, na ufadhili wake umeokoa mamia ya mamilioni ya maisha. Kwa hivyo, natumai kwamba kwa muda, tunaweza kueleza tena kwa nini kazi hii ni muhimu, na kuhakikisha kuwa ufadhili huo unarejeshwa ili tuendelee kuokoa maisha hayo.”