Bei ya afyuni imepanda kwa kiwango cha kihistoria huku mitandao ya uhalifu ikinufaika: UNODC
Bei ya afyuni imepanda kwa kiwango cha kihistoria huku mitandao ya uhalifu ikinufaika: UNODC
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu UNODC leo imeonya kuwa dawa zenye nguvu zaidi zilizotengenezwa kufanana na mihadarati asilia au za sintetiki huenda zikapata mahitaji makubwa zaidi kufuatia marufuku ya kilimo cha mazao ya afyuni nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa ripoti ya UNODC, “Bei za afyuni nchini Afghanistan zimeongezeka mara kumi tangu mamlaka nchini humo zilipopiga marufuku dawa za kulevya mwaka 2022 baada ya kuchukua udhibiti wa Kabul, kulingana na takwimu mpya za Umoja wa Mataifa.”
Ripoti imesema kilo moja ya afyuni iligharimu dola 750 mwaka jana, kutoka dola 75 miaka mitatu iliyopita, hali inayowafidia wauzaji kwa hasara ya uzalishaji wa jumla na mashamba ya mazao ya afyuni.
"Idadi ya mihadarati ya heroini na afyuni ilizokamatwa imepungua kwa takriban asilimia 50 kwa uzito tangu 2021," iliripoti ofidi hiyo ya Umoja wa Mataifa, ikionyesha kuwa kupungua kwa uzalishaji wa afyuni baada ya marufuku hiyo kumesababisha kupungua kwa usafirishaji wa mihadarati hiyo.
Afyuni ni kiungo kikuu cha asili kinachotumiwa kutengeneza dawa za kulevya aina ya heroini, ambayo ni dawa yenye nguvu zaidi na ya sintetiki. Vyanzo vikuu vitatu vya afyuni haramu duniani ni Afghanistan, Colombia, na Myanmar kwa mujibu wa UNODC.
Kutokana na kupanda kwa bei, ofisi hiyo imesema “faida kubwa bado zinapatikana, hasa kwa wafanyabiashara wakuu na wauzaji nje walioko katika mitandao ya uhalifu wa kupanga.”
Kupungua kwa akiba
Ofisi ya UNODC inakadiria kuwa akiba ya opiati mwishoni mwa 2022 ilikuwa tani 13,200, kiasi kinachoweza kukidhi mahitaji ya mihadarati ya Afghanistan hadi mwaka 2027.
"Kuongezeka kwa bei ya afyuni na akiba kubwa kunamaanisha kuwa biashara ya mihadarati nchini Afghanistan bado ni sekta haramu yenye faida kubwa," amesema mkurugenzi mtendaji wa UNODC, Ghada Waly.
Ameongeza kuwa “Faida hizi zinaelekezwa kwa mitandao ya uhalifu wa kimataifa, hali inayozidi kudhoofisha uthabiti wa Afghanistan, kanda, na maeneo mengine. Tunahitaji mkakati wa pamoja wa kupambana na dawa za kulevya unaolenga mitandao ya usafirishaji haramu huku tukiwapa wakulima njia mbadala za kiuchumi ili kuhakikisha mnepo wa muda mrefu kwa Afghanistan na watu wake.”
Kabla ya kushuka kwa uzalishaji wa afyuni, akiba ya Afghanistan ilikadiriwa kuwa na thamani ya kati ya dola bilioni 4.6 na bilioni 5.9, sawa na asilimia 23 hadi 29 ya uchumi wa nchi hiyo mwaka 2023.
Hii huenda iliwasaidia baadhi ya Waafghani wa kawaida kustahimili matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyoshuhudiwa tangu kurejea kwa mamlaka halisi, UNODC imesema.
Changamoto za wakulima
Hata hivyo UNODC imesema, kwa kuwa asilimia 60 ya akiba huenda iko mikononi mwa wafanyabiashara wakubwa na wauzaji nje, huku asilimia 30 tu ya wakulima wakishikilia akiba ndogo au ya wastani mwaka 2022.
“Wakulima wengi waliokuwa wakilima afyuni huenda wanakabiliwa na hali ngumu kifedha,” limeonya shirika la Umoja wa Mataifa lilionya.
Kwa mujibu wa UNODC njia mbadala endeleu za kiuchumi zinahitajika haraka ili kuwazuia wakulima kurudi kwenye kilimo cha mazao ya afyuni, hasa ikizingatiwa kuwa bei ya afyuni iko juu kwa sasa.
UNODC pia imetoa onyo kwamba upungufu wa afyuni unaweza kuwashawishi wanunuzi na wauzaji kutafuta dawa mbadala ambazo huenda zikawa hatari zaidi kuliko heroini, kama vile fentanyl au opioidi na nyingine za sintetiki.