Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW69: UN Women yakaribisha kupitishwa kwa azimio la kisiasa

Kundi la wanawake, baadhi wakiwa wamevaa hijabu, wakiwa wameketi kama wahudhuriaji katika tukio rasmi.
UN Photo/Manuel Elías Wawakilishi mbalimbali washiriki Kikao cha 69 cha Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

CSW69: UN Women yakaribisha kupitishwa kwa azimio la kisiasa

Wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Sima Bahous amekaribisha kwa dhati kupitishwa kwa Azimio la kisiasa juu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Wanawake uliofanyika Beijing, China 1995.

Amesema "kukabiliana na changamoto na fursa za usawa wa kijinsia kunahitaji hatua za pamoja na za uamuzi kutoka kwa nchi wanachama, wa UN hivi sasa zaidi ya wakati wowote ule.”

Kupitia taarifa iliyochapishwa leo Jumanne Machi, 11, kwenye wavuti wa UN Women, Bi. Bahous amesema wakati huu ambapo mafanikio ya usawa wa kijinsia yaliyopatikana kwa bidii yanashambuliwa, “jumuiya ya kimataifa imeungana kwa mshikamano kwa ajili ya wanawake na wasichana wote, kila mahali."

Bi. Bahous amesema, “hakuna taifa hata moja ambalo limefikia kikamilifu usawa wa kijinsia. Tamko hili lenye uthabiti linaweka wazi kuwa serikali zinatambua mwaka 2025 kama wakati muhimu, ambapo ahadi zilizotolewa miaka 30 iliyopita haziwezi tena kucheleweshwa.”

Amesema ni wakati wa kuhakikisha kuwa “tunatimiza ahadi zetu za usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote, kila mahali, na kwamba tunafanya hivyo kwa pamoja."

Azimio hilo lenye vipengele 22 lilipitishwa Jumatatu Machi 10 na Mawaziri na wawakilishi wa serikali wanaoshiriki mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69 jijini New York, Marekani.

Azimio pia linasisitiza umuhimu wa kulinda haki zote za binadamu na uhuru wa msingi kwa kila mwanamke na msichana, bila ubaguzi.

Pia azimio linazidi kuimarisha ahadi kwa wanawake, amani, na usalama, likieleza umuhimu wa kujumuisha sauti na uongozi wa wanawake katika hatua zote za kuzuia migogoro, ujenzi wa amani, na utatuzi wa migogoro.

Halikadhalka linaweka msisitizo juu ya umuhimu wa kutokomeza umasikini katika aina zake zote, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha haki ya wanawake na wasichana kupata elimu, hasa katika nyanja za STEM, na kuongeza uwekezaji wa umma katika mifumo ya huduma za malezi.

Kwa kutambua uwezo mkubwa wa teknolojia, linaangazia umuhimu wa kufunga pengo la kidijitali la kijinsia na linatoa wito wa uwekezaji mpya katika takwimu na data za kijinsia ili kusaidia utungaji wa sera unaozingatia ushahidi.

Tamko hili pia linathibitisha upya ahadi ya nchi wanachama kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, ikijumuisha aina mpya zinazojitokeza kama vile ukatili wa kidijitali, unyanyasaji mtandaoni, na uonevu wa kimtandao.

Halikadhalika linatambua kuwa kufanikisha maendeleo katika maeneo haya kunahitaji rasilimali kubwa na ufadhili wa kutosha. Linatoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya kitaifa, taasisi za wanawake, na mifumo ya kimataifa, ikiwemo kufufuliwa kwa Kamisheni ya Hali ya Wanawake (CSW), ili kuharakisha juhudi za kufanikisha usawa wa kijinsia duniani kote.