CSW69: Tija ya Azimio la Beijing New Zealand, Uganda na Kenya
CSW69: Tija ya Azimio la Beijing New Zealand, Uganda na Kenya
Jambo kubwa tunalojivunia sisi kutoka New Zealand ni kwamba idadi ya wanawake bungeni ni zaidi ya asilimia 50 ya wabunge wote. Wabunge wanawake ni wengi kuliko wanaume, ni kauli ya mshiriki wa mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69 kutoka New Zealand.
Mele Wendt mjumbe wa Chama cha Wanawake wa Ukanda wa Pasifiki kutoka New Zealand amesema hayo akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano wa CSW69 ulioanza Jumatatuya Machi, 11 mwaka huu wa 2025 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijiin New York, Marekani.
New Zealand yavuka lengo la usawa wa kijinsia Bungeni
Bi. Wendt akiwa amevalia nguo nyekundu yenye maua ya rangi tofauti pamoja na taji la maua kichwani amezungumza kwa bashasha akisema anasubiri kwa hamu kuweza kuelezea wajumbe wengine kuhusu mafanikio hayo ya New Zealand kwa mujib uwa matakwa ya Azimio la Beijing na Jukwaa la Utelekezaji lililopitishwa mwaka 1995 huko Beijing China, wakati wa mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wanawake.
Bi. Wendt anasema mafanikio hayo ya wabunge wanawake zaidi ya asilimia 50 bungeni walifikia mwaka jana wa 2024. Na alipoulizwa anatarajia mjadala wa aina gani kwenye CSW69, amesema, “nadhani usawa wa wanawake kwa ujumla, na hili linajitokeza katika njia mbalimbali. Lakini nadhani kuweko kwenye meza ya mazungumzo, kuwa na uwakilishi sawa bungeni, serikalini na duniani kote, nadhani litakuwa ni lengo zuri.”
Mwingine akiwa amevalia mavazi sare na Bi. Wendt, ni Caren Rangi naye pia kutoka New Zealand yeye akasema ana hamu kubwa ya kukutana na wanawake kutoka sehemu mbalimbali duniani.”
Na kuhusu ni jambo gani lipatiwe kipaumbele akasema ni “kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, kufikia uwiano wa kijinsia kwenye uongozi, na wanawake na uongozi.”
Kutoka Uganda ni Joyce Wanda, huyu ni Muasisi Mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kiraia la Reach for Uganda lililoanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuboresha maeneo ya vijijini kupitia elimu, afya na maendeleo ya jamii.
Miaka 30 baada ya Azimio la Beijing, Bi. Wanda anasema “angalau kumekuweko na maendeleo kidogo kwenye suala la uwakilishi wa wanawake serikalini. Lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha mwanamke wa mashinani anasikika.”
Kubwa zaidi analotaka kuona ni wanawake wawe na haki ya kumiliki ardhi na zaidi ya yote, “kuhakikisha wanawake na wasichana wanawakilishwa kwani sauti zao ni muhimu, hasa mawazo yao.”
Azimio la Beijing latekelezwa kwa vitendo Kenya
Shirika la kiraia la Mama Doing Good kutoka Kenya, nalo pia lina uwakilishi kwenye CSW69, naye si mwingine bali ni Elizabeth Koskei, Afisa Mtendaji Mkuu. Nilipomuuliza ni kwa jinsi gani Azimio la Beijing linatekelezwa nchini Kenya, hakusita kujitajia mafanikio kwenye nafasi za uongozi kwa wanawake.
“Hivi sasa Kenya Jaji Mkuu na Naibu wake ni wanawake. Halikadhalika Mwanasheria Mkuu wa serikali. Na tangu Katiba imepitishwa tumeona mabadiliko kwenye kuongozeka kwa magavana wanawake,” amesema Bi. Koskei.
Amefafanua kuwa tangu Katiba mpya ianze kufanya kazi mwaka 2010, idadi ya magavana imeongezeka.
“Katiba ilisema kama kuna viongozi 10 lazima wanawake wawe watu. Na pia kwenye magavana, awamu ya kwanza baada ya katiba mpya hakukuweko na hata mmoja, awamu ya pili wakaweko 3, na muhula huu sasa tuna magavana 7.”
Mama Doing Good na uwezeshaji wanawake kiuchumi Kenya
Afisa Mtendaji huyu wa Mama Doing Good akanieleza kuwa shirika lao linatoa huduma katika kaunti 44 bado tatu tu wafike kila mahala.
“Na moja ya huduma tunazotoa ni uwezeshaji kiuchumi wanawake kupitia ‘table banking’ yaani wanakusanya fedha pamoja na kisha wanasaidia kwenye kuwekeza. Sisi pia tunawaongezea kiasi ili kuwa na fungu kubwa na hii imeleta maendeleo makubwa, sisi tunafurahi na wao wanafurahi,” amesema Bi. Koskei.
Akazungumzia pia mazingira akisema kuwa wanaelimisha wanawake upandaji wa miji, na wanawake hao pia wanafundisha watoto wao kwani “mazingira yetu ni jukumu letu.”