UN yalaani vurugu na kutaka uwajibikaji baada ya ukatili wa kutisha Pwani ya Syria
UN yalaani vurugu na kutaka uwajibikaji baada ya ukatili wa kutisha Pwani ya Syria
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesisitiza haja ya kuwajibisha wote waliohusika na uhalifu uliotekelezwa katika pwani ya Syria.
Akizungumza mjini Geneva Uswisi hii leo amepongeza tangazo la mamlaka ya mpito la kuunda kamati huru ya uchunguzi, akisisitiza kuwa uchunguzi huo unapaswa kuwa wa haraka, wa kina, huru, na usioegemea upande wowote.
Kamishna Mkuu pia amesisitiza umuhimu wa kuwachukulia hatua wale wote waliobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki, bila kujali uhusiano wao wa kisiasa, kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, amesema waathiriwa na familia zao wanastahili kupata haki, ukweli, na fidia.
Ili kuhakikisha kuwa ukiukwaji na uhalifu wa namna hiyo haujirudii, Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu amesema ni muhimu kwamba mchakato wa uchunguzi na ujumuishaji wa makundi yenye silaha katika vikosi vya jeshi la Syria unazingatia wajibu wa nchi hiyo chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu.
Pia amesisitiza kuwa wote waliohusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu wa zamani au wa hivi karibuni wanapaswa kuwajibishwa ipasavyo.
Wito wa kusitisha mashambulizi dhidi ya raia
Katika taarifa tofauti, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu nchini Syria, Adam Abdelmoula, amelaani vikali vurugu zilizosababisha vifo vya raia wengi hadi sasa. Amewataka wahusika wote kujizuia na kuacha kulenga raia na miundombinu ya kiraia.
Abdelmoula alifafanua kuwa Umoja wa Mataifa haujatuma ujumbe wowote wa uchunguzi au wa kutafuta ukweli katika pwani ya Syria, kinyume na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa.
Ameeleza kuwa uchunguzi wa aina hii hufanyika tu kwa mamlaka kutoka Baraza la Haki za Binadamu au Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa juhudi za Umoja wa Mataifa nchini Syria zinaendelea kujikita katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji zaidi, huku ukihakikisha usalama wa wafanyakazi wake, washirika wake wa kibinadamu, na familia zao. Pia amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kibinadamu ya kutoegemea upande wowote, uadilifu, na uhuru, huku ukihimiza matumizi ya taarifa zilizo sahihi na zilizothibitishwa kuhusu shughuli zake.
Raia 111 wameuawa
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR, imebainisha kuwa ripoti zinaendelea kupokelewa kuhusu kiwango cha kutisha cha vurugu zilizozuka katika pwani ya Syria tangu Machi 6.
Taarifa hizo zimebaini kuwa hadi sasa watu 111 wameuawa, ingawa mchakato wa uhakiki bado unaendelea, na idadi halisi ya vifo inadhaniwa kuwa kubwa zaidi.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva leo msemaji wa UNHCR, Thamin Al-Khaitan, amesema kuwa matukio mengi yaliyoripotiwa ni mauaji ya kiholela, ambayo yanaonekana kuwa yametekelezwa kwa misingi ya kimadhehebu katika majimbo ya Tartous, Latakia, na Hama.
Mauaji haya yanadaiwa kufanywa na watu wenye silaha wasiojulikana, wanachama wa makundi yenye silaha yanayodaiwa kuunga mkono vikosi vya usalama vya mamlaka ya mpito, na wapiganaji waliokuwa na uhusiano na serikali ya zamani.
Familia zinaendelea kuuawa
Katika visa vya kusikitisha, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ameripoti kuwa familia nzima, ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto, na wale waliokuwa wamejisalimisha, waliuawa, hasa katika miji na vijiji vinavyokaliwa na Waalawite.
Kwa mujibu wa ushuhuda uliokusanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, wahalifu walivamia nyumba na kuwauliza wakaazi iwapo ni Waalawite au Wasunni kabla ya kuwaangamiza au kuwaachilia kwa misingi hiyo. Baadhi ya manusura waliiambia UNHCR kuwa wanaume wengi walipigwa risasi mbele ya familia zao.
Kati ya tarehe 6 na 7 Machi, wanaume wenye silaha wanaoshukiwa kuwa waaminifu kwa vikosi vya usalama vya serikali ya zamani waliripotiwa kuvamia hospitali kadhaa katika Latakia, Tartous, na Banias.
Huko walikabiliana na vikosi vya usalama vya mamlaka ya mpito pamoja na makundi ya waasi yanayoyaunga mkono.
Ripoti zinasema kuwa mashambulizi haya yalisababisha vifo vya raia kadhaa, wakiwemo wagonjwa, madaktari, na wanafunzi wa udaktari, pamoja na uharibifu wa hospitali hizo.
Unyang’anyi wa kiwango kikubwa
Tume ya Haki za Binadamu ilibaini kuwa ukiukwaji mwingine wa haki ulioripotiwa katika siku za hivi karibuni ni uporaji mkubwa wa nyumba na biashara, hasa ukifanywa na watu wasiojulikana waliotumia machafuko yaliyopo kujinufaisha. Raia wengi walilazimika kukimbia makazi yao na kuelekea maeneo ya vijijini, huku wengine wakitafuta hifadhi katika kambi ya anga inayodhibitiwa na Urusi katika eneo hilo.
Mamlaka ya mpito ilitangaza kumalizika kwa operesheni za kiusalama katika maeneo ya pwani mnamo Machi 10, lakini ripoti za mapigano ya hapa na pale zinaendelea kuripotiwa.
Kauli za chuki zahatarisha umoja wa jamii
OHCHR imebainisha kuwa imekusanya ushahidi wa video na ushuhuda wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Hata hivyo, hali imezidi kuwa mbaya kutokana na kuongezeka kwa kauli za chuki, mitandaoni na nje ya mtandao, pamoja na kuenea kwa taarifa za kupotosha, ikiwemo video zilizochukuliwa nje ya muktadha, jambo linaloongeza hofu miongoni mwa wananchi.
Tume ya Haki za Binadamu imeonyesha wasiwasi wake kuwa ongezeko la kauli za chuki, pamoja na upotoshaji wa habari, kunaweza kuzidisha mgawanyiko wa kijamii na kuhatarisha mshikamano wa jamii ya Syria.