CSW69 na Haki za Wanawake: Hakuna muda wa kusinzia, safari bado ni ndefu
CSW69 na Haki za Wanawake: Hakuna muda wa kusinzia, safari bado ni ndefu
Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani unaanza mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69, kusanyiko kubwa zaidi la kila mwaka la Umoja wa Mataifa linalomulika usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake mwaka huu washiriki wakiwa zaidi ya 25,000.
Muziki mororo uLifungua pazia la mkutano huo katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao umesheheni watu kutoka kila kona ya dunia waliojumuka hapa mahsiusi kujikita na ajenda na wanawake na usawa wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women maudhui ya mkutano huu unaoanza leo hadi tarehe 21 Machi ni “Tathmini na Mapitio ya Utekelezaji wa Azimio la Beijing na Mpango wa Utekelezaji baada ya miaka 30”
Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Bila shaka tulijua haki za wanawake hazitaweza kutimizwa kwa usiku mmoja au kwa miaka kadhaa , lakini karhe tatu baadaye ahadi hiyo inaonekana kuwa mbali kulivyotarajia. Haki za wanawake ziko katika mashambulizi,mfumo dume umerejea na umerejea kwa nguvu kubwa. Lakini kuna dawa, huu ni wakati wa wale tunaojali kuhusu haki za wanawake kusimama kitedete, kupaza sauti, ni wakati wa dunia kuchochea hatua na kutimiza ahadi ya Beijing,”
Kwa wiki mbili tathimini ya mkutano huu itajikita na
✅ Mapitio ya maendeleo katika kutekeleza Azimio la Beijing na Mpango wa Utekelezaji wa Beijing tangu kupitishwa kwake mwaka 1995.
✅ Tathmini ya matokeo ya kikao cha 23 cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambacho kilifanyika mwaka 2000 kwa lengo la kuimarisha hatua za kufanikisha usawa wa kijinsia.
✅ Uchambuzi wa changamoto zinazoendelea kuzuia maendeleo ya haki za wanawake na wasichana.
✅ Kupendekeza hatua madhubuti za kuharakisha utekelezaji kamili wa ahadi zilizowekwa na nchi wanachama.
Lengo Kuu
- Kuthibitisha upya ahadi ya dunia katika kufanikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
- Kupima mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji juhudi zaidi.
- Kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, na asasi za kiraia kwa ajili ya maendeleo jumuishi.
Wawakilishi hao zaidi ya 25,000 ambao ni wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wataalamu, wanaharakati kutoka kila kona ya dunia watajadili na kukubaliana juu ya hatua na uwekezaji ambao unaweza kumaliza umaskini miongoni mwa wanawake na hatimaye kusongesha usawa wa kijinsia.
Ni lazima tuhakikishe tunatimiza lengo la Azimio la Beijing: Philemon Yang
Rais wa Baraza Kuu Philemon Young kwa upande wake ameuambia Mkutano huo wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake CSW69 kwamba kwa miongo mitatu ya kupigania haki za wanawake dunia imeshuhudia baadhi ya mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongezeka idadi ya wanawake bungeni, wasichana wengi zaidi kupata elimu na wanawake wengi zaidi wafanyakazi leo kuliko miaka 30 iliyopita.
Hata hivyo ameonya kuwa huu sio wakati wa kusinzia kwani safari bado ni ndefu kutimiza lengo na lengo hilo litatimia tu endapo wanawake na wasichana hawatokataliwa kutimiza ndoto zao, kupata haki zao na kuthaminiwa sawa na wengine katika jamii. Ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha hili na kwa pamoja tunaweza kutimiza lengo
Kuwekeza kifedha kwa wanawake sio hisani ni haki: Francois Moudouthe
Mwenyekiti mtendaji wa mfuko wa mfuko wa maendeleo wa wanawake wa Afrika Bi. Francois Moudouthe akihutubia mkutano wa CSW609 amesema "miaka 30 iliyopita Azimio la Beijing lilidhihirisha kuwa haki za wanawake ni haki za binadamu. Wito wa kuhakikisha wanawake wanajikwamua kiuchumi na kifedha haujatimizwa. Hata hivyo kumekuwa nah atua zilizopigwa kuhakikisha wanawake wa Kusini mwa dunia kupata misaada ya ufadhili na mikopo, hata hivyo changamoto za kupigania haki za wanawake kifedha zinazidi kukita mizizi.
Hivyo amesisitiza “ Ni muhimu serikali na mashirika ya kifedha kuwekeza katika kuwaweza kwa kiasi kikubwa kwa wanawake kifedha na katika mashirika yanayopigania haki za wanawake , sio msaada wa hni haki na sio kazi ngumu kutekeleza ni suala la utashi wa kisiasa.”
Azimio la Kisiasa la Beijing30+
Wakati wa CSW69 kwenye kikao cha Mawaziri, na wawakilishi wa serikali, limepitishwa Azimio la Kisiasa juu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Wanawake uliofanyika Beijing, China 1995. Azimio hilo lina vipengele 22 ambapo katika baadhi ya vipengele;
- Linatambua kuwa mwaka 2025 ni fursa ya kipekee ya kuleta pamoja nchi wanachama ili kuchagiza hatua za kutekeleza Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji na kufanikisha usawa wa jinsia pamoja na kujengea uwezo wanawake na wasichana kupitia michakato ya majukwaa mbalimbali.
- Azimio linahamasisha nchi wanachama kuzingatia kuteua wanawake wagombea wa nyadhifa mbali mbali kwenye chaguzi zijazo kama vile Katibu Mkuu wa UN na vile vile nafasi ya Rais wa Baraza Kuu.
- Azimio linasisitiza kwamba usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote ni muhimu kwa maendeleo endelevu na kutimiza ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma,.
- Linasisitiza uhusiano wa kuimarishana kati ya kufanikisha usawa wa kijinsia na utekelezaji kamili, madhubuti na wa kasi wa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji, utekelezaji unaozingatia jinsia na Ajenda ya 2030, pamoja na matokeo ya mikutano mikuu na makongamano ya Umoja wa Mataifa.