Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tupiganie uhuru wa wasichana na wanawake kote duniani: Jaha Dukureh

Wasichana wanapiga dole gumba katika shule moja nchini Ghana.
© UNICEF/Roger Yebuah
Wasichana wanapiga dole gumba katika shule moja nchini Ghana.

Tupiganie uhuru wa wasichana na wanawake kote duniani: Jaha Dukureh

Wanawake

Katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake ambayo kila mwaka ni Machi 8, hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kulifanyika hafla maalum ya ambayo mwaka huu imebeba maudhui “Kwa wanawake na wasichana wote: haki, usawa, uwezeshaji.

Akizungumza kwenye hafla hiyo katika Ukumbi wa Baraza Kuu, Bi. Jaha Dukureh, Balozi Mwema wa Kikanda wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika amesema “Ninasimama mbele yenu kama muathirika aliyenusurika katika mfumo, ulioniambia kuwa thamani yangu ilihusiana na kimya changu, utiifu wangu, na uwezo wangu wa kuvumilia. Kuvumilia ukeketaji wa wanawake, kuvumilia kuozeshwa kutoka ndoa moja hadi nyingine nikiwa bado mtoto”.

Ameongeza kuwa “Lakini, sikuvumilia tu na kunusurika, nilipinga. Nilipigania uhuru wangu, uhuru wa binti yangu na uhuru wa wanawake na wasichana wote wanaostahili zaidi ya kunusurika. Wanastahili haki ya kustawi.”

Kwa sababu kwa wanawake na wasichana wote, umaskini si ukosefu wa pesa tu, amesema “Ni ukosefu wa Madaraka”.

Ameeleza kuwa wakati msichana anakosa elimu kwa sababu familia yake haiwezi kumudu ada za shule, wakati mama hawezi kuondoka katika ndoa yenye unyanyasaji kwa sababu hana uhuru wa kifedha, wakati kazi za wanawake mashambani, majumbani, na masokoni hazitambuliki na hazilipwi, hii siyo tu ukosefu wa usawa wa kiuchumi. Ni kunyimwa utu, na kwa wanawake na wasichana wote, utu hauwezi kujadiliwa.

“Harakati za haki za wanawake na wasichana wote zinakabiliwa na upinzani, lakini hatutarudi nyuma,” amesema na “Hatutakaa kimya.”

Ameongeza kuwa “Kuanzia vijijini Afrika hadi kumbi za madaraka, kuanzia mashambani hadi kwenye vyumba vya bodi, kutoka madarasani hadi majukwaa ya kimataifa, wanawake na wasichana wote tupo hapa, na tutaendelea kuandamana kwa sababu utu hauwezi kujadiliwa, usawa si chaguo, na uhuru kwa wanawake na wasichana wote si ndoto. Ni madai, na hatutakoma hadi yatimizwe.”