Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna wasiwasi na mauaji ya raia Syria – Kamishna Mkuu Türk

Mvulana mdogo aliyevaa hoodie ya bluu na koti akitembea kwenye kifusi cha jengo lililoharibiwa huko Idlib, Syria, huku gari likiwa limeharibika nyuma.
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman Sehemu za kaskazini-magharibi mwa Syria ziko magofu kufuatia takriban miaka 14 ya vita.

Tuna wasiwasi na mauaji ya raia Syria – Kamishna Mkuu Türk

Amani na Usalama

Mauaji ya raia katika miji ya pwani kaskazini-magharibi mwa Syria yanapaswa kusitishwa mara moja, amesema hii leo Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Volker Türk kufuatia mfululizo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wanamgambo wa serikali ya zamani na vikundi vingine vyenye silaha nchini humo.

"Tunapokea ripoti za kushtusha sana kuhusu familia nzima, wakiwemo wanawake, watoto na wapiganaji waliokwishasalimisha silaha, wakilengwa na kuuawa," amesema Türk katika taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadam, OHCHR.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mapigano yamejikita katika miji ya pwani ya Tartus na Latakia ambako ni makazi ya watu wa madhehebu ya dini ya kiislamu ya Alawite, ambayo ni ya wachache na pia familia ya kiongozi wa zamani wa Syria, Bashar Al Assad ni waumini.

"Kuna ripoti za mauaji ya kiholela kwa misingi ya madhehebu ya dini yanayofanywa na wahusika wasiojulikana, wanachama wa vikosi vya usalama vya mamlaka ya mpito, pamoja na wale wanaohusishwa na serikali ya zamani,” amesema Kamishna huyo Mkuu.”

Vikundi vinavyotisha raia

Amesema kwamba tangazo la mamlaka ya mpito kuhusu nia yao ya kuheshimu sheria lazima lizingatiwe na hatua za haraka za kuwalinda wasyria, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zote muhimu ili kuzuia ukiukwaji wa haki na kuhakikisha uwajibikaji unafikiwa pale unapotokea.

"Ni lazima kufanyike uchunguzi wa haraka, wa wazi na usio na upendeleo kuhusu mauaji yote na ukiukwaji mwingine wa haki, na wale wanaohusika wafikishwe mbele ya sheria, kwa mujibu wa viwango na kanuni za sheria za kimataifa," amesema. "Vikundi vinavyotisha raia pia vinapaswa kuwajibishwa."

Matukio haya pamoja na ongezeko la kauli za chuki mtandaoni na nje ya mtandao yanaonesha kwa mara nyingine tena umuhimu wa haraka wa mchakato wa haki ya mpito unaojumuisha wote, unaomilikiwa kitaifa, na unaozingatia ukweli, haki na uwajibikaji, amesema Kamishna Türk.

TAGS: Amani na Usalama/Haki za binadamu/Mashariki ya Kati/Syria/OHCHR