Sasa ni wakati wa kutimiza ahadi ya usawa wa kijinsia
Sasa ni wakati wa kutimiza ahadi ya usawa wa kijinsia
Katika kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8 leo hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kunafanyika hafla maalum ya kuadhimisha siku hiyo ambayo mwaka huu imebeba maudhui “Kwa wanawake na wasichana wote: haki, usawa, uwezeshaji.”
Usawa wa kijinsia haujawahi kuwa wa dharura kama sasa: UN Women
Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women Sima Bahous amesema ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo ndoto ya azimio la Beijing miaka 30 iliyopita la kufanya usawa wa kijinsi kuwa hali halisi, "Wito wa usawa wa kijinsia haujawahi kuwa wa dharura kama sasa, sanjari na changamoto zinazotukabili, lakini dhamira yetu haijawahi kuwa na nguvu kama sasa. Ni lazima sote tuchagize haki za wanawake, ni lazima tukabiliane na upinzani, lazima tuboreshe mbinu za kupambana na ubaguzi wa kimfumo na lazima tuwalinde watetezi wa haki za binadamu za wanawake. Kwa pamoja tunaweza kusonga mbele"
Bi Bahous ametoa wito wa ulinzi zaidi kwa wanawake na watetezi wa haki za wanawake.
Akitilia mkazo kwamba vikwazo njiani sasa vinaonekana zaidi, lakini “azma ya wanawake haijawahi kuwa thabiti zaidi”.
Akisherehekea usawa kwa wanawake na wasichana wote, kila mahali, Bi. Bahous ameongeza kuwa usawa ndio mabadiliko makubwa.
“Hatutakoma hadi usawa wa kijinsia uwe hali halisi yetu ya pamoja na thawabu yetu ya pamoja.”
“Kuanzia serikalini hadi kwenye vyumba vya bodi, kutoka darasani hadi majumbani, usawa wa wanawake ndio suluhisho kubwa zaidi.”
Bi. Bahous amewakumbusha wote kwamba “chaguo liwe la kutenda au la kutochukua hatua, ndilo linalotudhihirisha tulivyo.”
Dhamira bado haijatimia
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na kupongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kusongesha usawa wa kijinsia duniani amesema
“Hata hivyo, mafanikio haya yaliyopatikana kwa jitihada kubwa bado ni dhaifu na hayatoshi kabisa. Mateso ya muda mrefu, ukatili, ubaguzi na ukosefu wa usawa wa kiuchumi bado vinaathiri jamii zetu. Kila baada ya dakika kumi, mwanamke huuawa na mwenzi wake au mwanafamilia.”
Ameongeza kuwa wanawake na wasichana milioni 612 wanaishi chini ya kivuli cha migogoro ya silaha ambapo haki zao mara nyingi huchukuliwa kama zisizo na thamani.
Soko la ajira bado lina mfumo dume
Akitaja takwimu amesema chini ya theluthi mbili ya wanawake duniani wanashiriki katika soko la ajira na wale wanaoshiriki hulipwa mishahara ya chini kuliko wanaume.
Hivyo ameonya kwamba “Kwa kasi hii, itachukua miaka 130 kutokomeza umasikini uliokithiri kwa wanawake na wasichana. Na kama tunavyoshuhudia katika kila pembe ya dunia, kutoka kwenye upinzani hadi kurudi nyuma, haki za wanawake ziko mashakani. Karne za ubaguzi zinakuzwa na vitisho vipya.”
Kuhusu fursa za kidijitali kwa wanawake amesema “Zana za kidijitali, ingawa zina ahadi kubwa, mara nyingi zinanyamazisha sauti za wanawake, kuongeza upendeleo, na kuchochea unyanyasaji. Miili ya wanawake imekuwa uwanja wa vita wa kisiasa. Na ukatili wa mtandaoni unazidi kugeuka kuwa ukatili wa maisha halisi.”
Amemesema badala ya kuingiza usawa wa haki kama jambo la kawaida, dunia inashuhudia kuenea kwa ubabe na chuki dhidi ya wanawake.
Kwa muktadha huo amesistiza kwamba “Hatuwezi kukaa kimya wakati maendeleo yanaporudishwa nyuma. Lazima tupambane.”
Kizazi changu kinadai hatua zaidi: James Mumo Nyumu
Akizungumzia sauti za vijana kushiriki katika harakati za usawa na haki za wanawake, kwenye hafla iliyofanyika mjini Geneva Uswisi kuadhimisha siku ya wanawake mwanafunzi kutoka Kenya James Mumo Nyumu amesisitiza kuwa hakuna nchi yoyote iliyotekeleza ahadi yao ya dunia isiyo na ukatili dhidi ya wanawake.
Ameelezea kuhusu Azimio la kihistoria la Beijing la mwaka 1995, ambalo linatilia mkazo umuhimu wa usawa wa kijinsia na limeleta mabadiliko kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita, ikiwa ni pamoja na mageuzi zaidi ya 1,500 ya kisheria yaliyopitishwa duniani kote ili kuendeleza haki za wanawake na wasichana.
“Maono ya Beijing yalikuwa ramani ya siku zijazo ambazo bado hatujazifikia kikamilifu,” alisema akiongeza kuwa “Nguvu kwa wanawake si tishio ni zawadi kwa jamii.”
Bwana Nyumu amesisitiza kuwa mifumo inayotawaliwa na wanaume inawaumiza wanawake, huku pia ikiwadhalilisha na kuwanyima utu wanaume. Badala yake, wanaume wanapaswa kuonesha nguvu za kweli kwa kuwa na ujasiri wa kujifunza, kusahau na kujifunza upya.
Hivyo amesisitiza kwamba“Kizazi changu kinadai hatua zaidi,” akitoa wito wa kuchukua hatua zaidi ya Beijing kwani “Kazi yetu haijakamilika.”
Nilipigania Uhuru Wangu: Jaha Dukureh
Amesema “Ninasimama mbele yenu kama muathirika aliyenusurika katika mfumo ulioniambia kuwa thamani yangu ilihusiana na kimya changu, utiifu wangu, na uwezo wangu wa kuvumilia. Kuvumilia ukeketaji wa wanawake, kuvumilia kuozeshwa kutoka ndoa moja hadi nyingine nikiwa bado mtoto”.