FAO: Kilimo hifadhi na ufugaji bora wamwinua mwanamke Kigoma, Tanzania
FAO: Kilimo hifadhi na ufugaji bora wamwinua mwanamke Kigoma, Tanzania
Kutana na Hadija Alisido, mama huyu wa watoto wanne, mkulima kiongozi na mtoa chanjo ya ugonjwa wa kideri unaokumba kuku katika wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, kaskazini-magharibi mwa Tanzania.
Hadija ni mnufaika wa mradi wa Programu ya Pamoja ya Kigoma, KJP nchini Tanania, chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) tangu mwaka 2018.
Akiishi katika eneo ambalo changamoto za kilimo ni nyingi zikichangiwa na rutuba duni ya udongo pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, hali ya uzalishaji wa mazao ya kilimo ilionekana kuwa na matumaini kidogo mwanzoni. Lakini kupitia mafunzo ya FAO yaliyowezesha pia kupata mbegu bora na pia matumizi sahihi ya mbolea, maisha yake yalibadilika.
Nimeongeza mavuno
“Kwa maarifa niliyopata, nilibadilisha shamba langu la la ekari mbili, na kuongeza mavuno ya mahindi kutoka kilo 500 hadi 6,000. Kuongezeka kwa tija kuliboresha kipato changu kwa kiasi kikubwa na kuniwezesha kuwekeza katika maeneo mengine ya maisha yangu,” anasema Hadija akiwa anachambua maharage aina ya Jessica aliyovuna shambani mwake.
Hadija anasema, "nilipoanza, niliishi kwa mashaka, lakini sasa naona matunda ya juhudi zangu. Mavuno yangu ya mahindi yameongezeka, na hali ya familia yangu imeimarika. Hii ni zawadi kubwa kwa watoto wangu na kwa jamii yangu."
Eneo lao wanafuga kuku lakini kwa mazoea na hivyo kushambuliwa na magonjwa kama kideri. FAO ilimpatia Hadija mafunzo ya utoaji chanjo na sasa anatoa chanjo sio tu kwa kuku wake, bali pia wale wa jamii.
Kwa mujibu wa Hadija, juhudi zake za utoaji wa chajo zimesaidia kupunguza vifo vya kuku, kuongeza uchumi wa kijiji na kuboresha uhakika wa kupata chakula kwa familia nyingi kama litakavyo lengo namba mbili la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs la kuongeza uhakika wa kupata chakula bora.
Amejenga nyumba na kununua pikipiki
Kadri shamba lake lilivyokuwa na tija, ndivyo kipato cha Hadija kilivyoongezeka. Ametumia akiba yake kujenga nyumba ya vyumba viwili, kuboresha hali ya maisha kwa familia yake.
Amenunua pia pikipiki, ambayo sio tu imerahisisha ubebabaji wa mizigo lakini pia inamsadia kuongeza kipato zaidi. Njia hii mpya ya usafiri imemuwezesha Hadija kujiingiza katika fursa zingine za kibiashara, kupanua wigo wake wa ujasiriamali.
Naweza kukidhi mahitaji ya shule ya watoto wangu
Mafanikio ya kiuchumi yamemwezesha Hadija kuwa na hakikisho la elimu kwa watoto wake. "Kwa msaada wa kilimo hiki, sasa naweza kukidhi mahitaji ya shule kwa watoto wangu. Elimu ni muhimu sana kwangu. Ninajivunia kuona watoto wangu wakikua na ndoto zao."
Nafuga pia na mbuzi
Hadija awali alifuga mbuzi wa kienyeji lakini kupitia KJP alipatiwa mbuzi wa kisasa "Nilikuwa na mbuzi wa kienyeji, lakini nilikuwa na changamoto kubwa ya kuzalisha maziwa mengi. Hata hivyo, baada ya kupokea mbuzi dume wa kisasa, hali imebadilika kabisa. Mbuzi wangu wanakuwa haraka na kunipatia maziwa na samadi ambayo naitumia shambani,” anasema Hadija.
Mshindi wa tuzo
Safari ya mabadiliko ya Hadija haikupita bila kugundulika. Siku ya Wanawake wa Maendeleo ya Vijijini Duniani, Oktoba 15, 2023, alikabidhiwa Seti ya Vifaa vya kurahisisha shughuli za kilimo kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kubadilisha mifumo ya chakula na kukuza usawa wa kijinsia. Ujuzi wake katika kutumia mbinu endelevu na kuhamasisha jamii yake umeacha alama ya kudumu.
Kupitia kazi ngumu na kujitolea kwake, Hadija anaendelea kuchangia katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kama vile "Hakuna Umaskini" (SDG 1), "Hakuna Njaa" (SDG 2), na "Maisha Kwenye Ardhi" (SDG 15).
Ujumbe kwa wanawake
Kwa wanawake wengine Hadija ana ujumbe akisema, "Ni muhimu kujua kuwa hakuna kinachoshindikana ikiwa tutakuwa na malengo ya wazi na juhudi za kweli. Kilimo kinaweza kubadili maisha yetu, lakini lazima tuwe tayari kujifunza na kubadilika. Kila mmoja wetu ana nguvu ya kuboresha maisha yake na ya familia yake. Usikate tamaa, jifunze na tumia fursa zinazokuja mbele yako. Hakika, mabadiliko yanawezekana!"