Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM na IHP waongeza kituo cha msaada wa kibinadamu Chad ili kusaidia watu 220,000 Sudan

Wafanyakazi katika kituo cha Farchana IOM huko Chad wakishusha paneli kubwa ya chuma kutoka kwa lori kama sehemu ya mradi wa upanuzi wa kukabiliana na migogoro ya Sudan.
IOM 2025/ Alnodji Freddy Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM na Ushirikiano wa Kibinadamu wa Kimataifa (IHP) kwa pamoja wamekamilisha upanuzi wa kituo cha kibinadamu kilichoko kwenye eneo la Farchana, jimboni Ouaddaï nchini Chad, eneo ambalo ni mpakani na Sudan.

IOM na IHP waongeza kituo cha msaada wa kibinadamu Chad ili kusaidia watu 220,000 Sudan

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM  na Ushirikiano wa Kibinadamu wa Kimataifa (IHP) kwa pamoja wamekamilisha upanuzi wa kituo cha kibinadamu kilichoko kwenye eneo la Farchana, jimboni Ouaddaï nchini Chad, eneo ambalo ni mpakani na Sudan.

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo huko Farchana na Geneva, Uswisi inasema hatua hii itawawezesha wakimbizi 220,000 zaidi walioathiriwa na janga linaloendelea Sudan kupata msaada muhimu.
 
“Kituo hiki kilichoboreshwa kitaimarisha shughuli za kibinadamu za mashirika mbalimbali kupitia Adré amba oni mpaka wa Chad kwenda Sudan, ambako mamilioni ya watu wanakabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa chakula, makazi, huduma za afya na ulinzi,” imesema taarifa hiyo.
 
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, karibu watu milioni 9 katika jimbo la Darfur nchini Sudan wanahitaji msaada wa haraka.

Watu 82,000 wameshafikiwa kupitia operesheni hii

"Kwa kuimarishwa kwa operesheni za mpakani, IOM tayari imefikia zaidi ya watu 82,000 huko Darfur, Sudan kwa msaada muhimu wa kibinadamu, na kwa upanuzi wa kituo cha Farchana, tuko tayari kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu wengine 220,000 katika miezi ijayo. Kituo hiki pia kinawezesha ushirikiano mkubwa kati ya wahusika wa kibinadamu, mashirika ya maendeleo na serikali, jambo ambalo ni muhimu kwa mwitikio wa kina na endelevu." Amenukuliwa Pascal Reyntjens, Mkuu wa IOM nchini Chad.
 
Vita nchini Sudan vimeendelea kuongeza mahitaji makubwa ya kibinadamu nchini humo na nchi jirani kama Chad, kwa hivyo kituo cha kibinadamu cha Farchana kimekuwa muhimu katika kuratibu na kusaidia juhudi hizi za mpakani.

Je nini kinahusika na upanuzi huu?

Upanuzi wa kituo hiki unajumuisha ujenzi wa ofisi, makazi, na miundombinu mengine ambayo yanaimarisha uwezo wa mashirika ya kibinadamu kufikiwa huko Sudan.
 
"Kuanzisha kituo kinachofanya kazi katika eneo hili la mashariki mwa Chad ilikuwa changamoto kubwa kutokana na hali ngumu ya hewa, vikwazo vya upatikanaji wa vifaa vya matumizi na umbali. Lakini kupitia ushirikiano wa wadau wa IHP na azma ya wataalamu wetu, tumefanikisha kuunda msingi salama na unaofanya kazi kwa ajili ya juhudi za kibinadamu mpakani," amesema Bram Krieps, kiongozi wa timu ya IHP.