Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi za Azimio la Beijing hazipaswi tu kukumbukwa bali kutekelezwa: Mkuu wa UN Women

Mkurugenzi Mtendaji UN Women Sima Sami Bahous akihutubia Baraza la Usalama UN mjini New York.
UN Photo/Rick Bajornas Sima Bahous Mkjurugenzi Mtedndaji wa UN Women

Ahadi za Azimio la Beijing hazipaswi tu kukumbukwa bali kutekelezwa: Mkuu wa UN Women

Wanawake

Msichana aliyezaliwa leo:

  1. Atakuwa na umri wa miaka 39 kabla ya usawa kijinsia wa viti bungeni.
  2. Atakuwa na umri wa miaka 68 kabla ndoa za utotoni hazijakomeshwa.
  3. Atakuwa na umri wa miaka 137 kabla umasikini uliokithiri kwa wanawake na wasichana haujatokomezwa.
Kuelekea siku ya wanawake duniani itakayoadhimishwa mwishoni mwa wiki hii Mkurugenzi Mtendaji wa  shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawke UN Women, Sima Bahous, amesisitiza kwamba ahadi zilizowekwa chini ya Azimio la Beijing miaka 30 iliyopita kuhusu haki za wanawake hazipaswi tu kukumbukwa bali zinahitaji kutekelezwa kikamilifu.
 
Akizungumza wiki hii mjini Geneva Uswisi katika majadiliano ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha miaka 30 ya Azimio la Beijing (#Beijing30), Bi. Bahous amebainisha umuhimu wa kuharakisha maendeleo ya usawa wa kijinsia akiwataka viongozi wa dunia kuchukua hatua thabiti ili kuhakikisha haki za wanawake zinapewa kipaumbele wakati wa changamoto zinazoendelea duniani.
 
Amesema “Miaka 30 iliyopita dunia iliweka ahadi ya kusongesha fursa na utu wa wanawake na wasichana wote. Ahadi hiyo haikuwa maneno matupu kwenye karatasi, ilikuwa ramani ya njia na wito wa mshikamano . Na kwa miongo mitatu imechochea hatua, wasichana wengi sasa wako shule, wanawake wengi wako bungeni , kuna sheria nyingi zaidi zinawalinda wanawake dhidi ya ukatili, na mataifa mengi zaidi yanatambua usawa wa kijinsia ni lazima.”
Picha pana ya kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Binadamu UMOJA WA MATAIFA (HRC) huko New York, huku Katibu Mkuu akiwa jukwaani akihutubia mkutano mkubwa.
UN Photo/Elma Okic Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilikutana Geneva
Licha ya mafanikio hayo yote Bi, Bahous amesema ndio kwanza mkoko unaalika maua kwani safari bado ni ndefu “Hebu tuwe wakweli hatujafika tunapopaswa kuwa. Haki za wanawake na wasichana zinashambuliwa, fursa za wanawake kupaza sauti zinazidi kupungua na endapo tutaendelea na kasi hii msichana aliyezaliwa leo atakuwa na umri wa miaka 39 kabla wanawake hawaja na viti vingi bungeni kama wanaume, atakuwa na umri wa miaka 68 kabla ndoa za utotoni hazijakomeshwa, na atakuwa na umri wa miaka 137 kabla umasikini uliokithiri kwa wanawake na wasicha haujatokomezwa. Hatuwezi kulikubali hili.”
 
Mkuu huyo wa UN Women ameyahimiza mataifa yote kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha ndoto za azimio la Beijing hazisalii kuwa ndoto bali maisha halisi.